*Man U walichangamkia biashara mapema
*Hawakutaka tena machungu ya Mei 2012
Nakumbuka Mei mwaka jana, Kocha wa Manchester United akiwa amekasirishwa kupokonywa kombe.
Alikuwa Stadium of Light, uwanja unaotumiwa na Sunderland, hata big g aliyokuwa akitafuna ilielekea kuwa na hatari ya kushuka na kumkwama kooni.
Kabla ya mchezo huo wa mwisho wa Ligi Kuu ya England, Mei 13, Man United na Manchester City walikuwa sawa kwa pointi, City wakiongoza kwa wingi wa mabao hivyo kuhatarisha ubingwa uliokuwa unashikiliwa na United.
Kwa hiyo, City waliokuwa wakipepetana na Queen Park Rangers (QPR) hawa hawa wa leo, walihitaji ushindi mnono ili wajihakikishie taji baada ya miaka zaidi ya 40.
Mambo hayakuwaendea vyema, na ilikuwa kana kwamba United wangetwaa taji la 20, maana Wayne Rooney alifunga bao dakika ya 20 na lilidumu hadi kipenga cha mwisho kilipopulizwa.
Ile mechi ya Man U na Sunderland iliisha mapema, ikawaacha City wakifurukuta na QPR waliokuwa wakipigania kushuka daraja.
Manchester United na washabiki wao walianza kushabikia, maana wakati wao wakiwa wameshajikusanyia pointi tatu, jirani zao mpira ukikaribia kuisha walikuwa wameshafungwa mabao 2-1, wakiendelea kupambana.
Ferguson na Man U yake walibakisha sekunde 100 tu wajihakikishie ubingwa, lakini kibao kiligeuka dimba la Etihad katika dakika za majeruhi, Edin Dzeko na Sergio Aguero walipotikisa nyavu za QPR dakika ya 92 na ya 94 na mechi kumalizika 3-2.
Mawasiliano yalikuwa ya hali ya juu kati ya Stadium of Light na Etihad, ambapo Man U walinyong’onyea isivyo kawaida kupata habari kwamba jamaa wa Etihad walisawazisha na kupachika bao la ushindi.
Huo ulikuwa mwisho wa sherehe zilizoanza kabla ya muda wake, na nakumbuka Ferguson akiwakusanya wachezaji wake kuwaelekeza waende vyumba vya kubadilisha, badala ya kusherehekea uwanjani ubingwa uliokuwa umeota mbawa.
Tangu siku hiyo, United wamekuwa wakiwasema wenzao wa City kuwa ni majirani wapiga kelele, kwamba kombe walilopata baada ya miaka 44, kelele za kushangilia zilikithiri.
Ferguson alisema kwa macho makavu kwamba lazima arejeshe kombe wakati baadhi ya wadau wa soka wakidhani angestaafu.
“Wanajua wazi kwamba siendi popote,” alisikika akisema, na kweli dhamira yake ya kurudisha kombe ilitimizwa kivitendo kwa kumsajili mfungaji bora wa ligi, Robin van Persie kwa milioni 24 kutoka Arsenal na ndiye amekuwa mfungaji bora kwao hadi sasa.
Ushindi na ubingwa wa Man United Jumatatu hii ni tuzo kwa kazi kubwa waliyofanya tangu mwanzo wa msimu kurejesha heshima waliyopoteza, wakihakikisha wanawaacha mbali jirani zao.
City walielekea kubweteka baada ya kutwaa kombe mwaka jana, na kocha Roberto Mancini alisikika karibuni akisema United wameshinda kutokana na timu nyingi kujilegeza zinapocheza nao.
Lakini msimamo wa ligi unaeleza mengi, tofauti ya pointi 16 kati ya bingwa huyu mpya na anayeshika nafasi ya pili – Manchester City, lakini pia tofauti ya pointi 60 kati ya United na timu mbili zinazoshika mkia.
Anachofurahia sana Fergie kwa sasa ni kile alichoshangilia kati ya muda mpira ulipomalizika Stadium of Light na habari za Aguero kufunga bao la tatu kusafiri kutoka Etihad hadi Sunderland.
Mla mla leo, mla jana kala nini? Ferguson amecheka mwisho, na ndiye anayecheka sana. Kicheko hicho kimechangiwa kwa kiasi kikubwa na Robin van Persie, aliyewapa lifti kubwa sana United msimu huu.
Alifuata nyayo za wenzake walioondoka Arsenal kama vile Gael Clichy, Emmanuel Adebayor, Kolo Toure na Samir Nasri kujiunga Manchester City. RVP naye alitakiwa Etihad, Wenger akataka kumpeleka huko au nje ya nchi, lakini mwenyewe akakataa na kwenda United.
Ferguson aliomba muda mrefu kumchukua RVP lakini Wenger na Arsenal waliminya mpaka Fergie akaeleza mshangao wake, kwani alikuwa amenuia kuhakikisha ubingwa uliokwenda Etihad ulikuwa wa muda mfupi tu, hatimaye akafanikisha. Kwa hiyo kombe lilipotelea Stadium of Light, likarejea wakiwa nyumbani Old Trafford, washabiki wangetaka zawadi gani zaidi ya hiyo?
RVP ameonesha ongezeko la thamani lililotakiwa na Ferguson hajutii kumnunua kwa pauni milioni 24. Van Persie anasema anataka astaafu soka akiwa United, lakini hilo si lake, ni la Fergie kuamua, akitaka aulize waliomtangulia na waliopendwa walikoishia baada ya miaka michache tu.
Bado Ferguson anaumia kwamba timu yake haikuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, na anahisi kwamba walinyimwa haki yao na mwamuzi, lakini ndivyo baadhi ya timu zinavyowaona United pia kwamba hupendelewa.
Bado United hawajafikia kiwango cha juu kabisa, maana wamekuwa na udhaifu mkubwa, hasa kwenye beki mwanzoni mwa msimu. Walikuwa wakishinda, lakini baada ya ama kutangulia kufungwa au matokeo ya jumla yaliishia kuwa na uwiano usio mzuri wa mabao.
Washabiki wa Man U wanaweza kubisha, lakini Fergie mwenyewe alipata kuandika:
“Je, tunatathmini vipi msimu huu – je ni wa kujutia au kushangilia? Kwangu kuna uzuri na ubaya; kuna tatizo lakini pia yanajitokeza mambo kadhaa mazuri ya kutunyanyua.”
Kadiri ligi ilivyosogea, United walijiimarisha na kuhakikisha wanatoka na ushindi, mara chache sare na wakaanza kusahau kufungwa.
Walipoteta na Jose Mourinho Old Trafford siku Real Madrid walipowatoa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wapo waliosema labda Mourinho anataka kuvaa viatu vya Sir Alex.
Lakini wengine mawazo yao yote yalikuwa kwa mchezaji wao wa zamani, Cristiano Ronaldo, ambaye baadhi ya watu wamekuwa wakisema atarudi, lakini bei yake na mkataba wake Real vikoje kwa sasa?
Ferguson hakuridhika na RVP, na japokuwa hajasema anamrejesha Ronaldo au kununua wakali wengine, amesajili makinda kama Wilfried Zaha kutoka Crystal Palace na ana mtu kama Nick Powell anayetajwa atakuwa bora msimu ujao.
Humwambii kitu babu Ferguson linapokuja suala la kubomoa na kukijenga kikosi chake; ana kauli na haoneshi dalili za kufika mwisho wa kazi yake, labda ndiyo maana Mourinho alisema Old Trafford ni himaya ya Fergie na angependa abaki hapo ‘daima’.
Ferguson haendi popote, hata baada ya United kutwaa ubingwa wa 20, na wa 13 tangu ajiunge hapo, kazi ya kulitetea kwa msimu ujao inaanza, na wapinzani wake wanajua hilo.