*Vita ya kushuka ni Wigan, Sunderland, Villa
Hafla ya kukabidhiwa kombe na kumuaga kocha Sir Alex Ferguson imefana baada ya Manchester United kuwafunga Swansea 2-1 na kufikisha pointi 88 dhidi ya 75 za Manchester City wanaoshika nafasi ya pili.
Fergie ameamua kustaafu baada ya kuitumikia klabu kwa miaka karibu 27 na kuwapatia ubingwa wa EPL mara 13. Alitoa hotuba na kushangiliwa vilivyo na mashabiki waliofurika Old Trafford, akaomba mrithi wake, David Moyes apewe ushirikiano mkubwa.
Swansea wamebaki na pointi zao 46 wakiwa na uhakika wa kucheza EPL msimu ujao, kwani wapo nafasi ya tisa.
Vita ya kuwania nafasi mbili za uwakilishi Ligi ya Mabingwa Ulaya imeendelea, baada ya Tottenham Hotspurs kuwafunga Stoke City kwa tabu 2-1, baada ya kutangulia kulala dakika za mwanzo.
Ushindi huo unampa Andres Villas-Boas jeuri ya kukaa nafasi ya nne, akiwasubiri Arsenal Jumanne wanaokipiga na Wigan Athletic waliotwaa Kombe la FA Jumamosi hii dimbani Wembley. Spurs wanawazidi mahasimu wao wa London Arsenal kwa pointi mbili, lakini Arsenal wana mchezo mmoja mkononi. Chelsea wapo nafasi ya tatu kwa pointi 72 baada ya ushindi wa Jumamosi dhidi ya Aston Villa.
David Moyes aliwaongoza Everton katika mechi ya mwisho nyumbani kwa kuwafunga West Ham United 2-0, ambapo Moyes alishangiliwa, tofauti na alivyosema awali hangeshangaa akziomewa na wana Everton kwa uamuzi wake wa kuwakimbia na kujiunga United.
Everton kwa ushindi huo wanashika nafasi ya sita, wakiwa na pointi 63, wakitarajia kucheza Ligi ya Europa, wakati wanaposubiri kujua kocha gani atawafundisha msimu ujao, baada ya kuwa na Moyes kwa miaka 11.
Mashaka ya Newcastle United walioonesha uchovu wa aina yake msimu huu yameisha, baada ya kujihakikishia watabaki EPL msimu ujao, kutokana na kuwafunga QPR 2-1 katika mechi waliyoanza kufungwa Loftus Roas.
Alan Pardew alinukuliwa akisema majuzi kwamba hajui hatima yake wala timu kwa msimu ujao, ambapo licha ya kupewa mamilioni ya pauni na kusajili wachezaji dirisha dogo Januari, waliendelea kuvurunda.
Hata hivyo ushindi wa Jumapili hii umewavusha kwenye kingamo la kushuka daraja, kwa sababu wana pointi 41 zisizoweza kufikiwa na Wigan, Sunderland wala Aston Villa wanaoikwepa nafasi moja iliyobaki ya kushuka daraja kuungana na QPR na Reading.
Norwich walioanza ligi vizuri na kupoteza mwelekeo kwenye mzunguko wa pili kwa kuzoea kufungwa, wamejinasua pia kushuka daraja, baada ya kuwapa West Bromwich Albion kipigo cha mbwa mwizi kwa mabao 4-0.
Norwich wanakuwa nafasi ya 12 kwa pointi 41 wakati West Brom watakaojiuliza sana juu ya aibu ya kichapo hicho wapo nafasi nzuri ya nane baada ya kujikusanyia pointi 48.
Sunderland ya Paolo Di Canio imeshindwa kujinasua kabisa kwenye kizingiti cha kushuka daraja baada ya kwenda sare ya 1-1 na Southampton na kujiweka katika nafasi ya 17 wakiwa na pointi 39, na itabidi waombe Wigan wafanye vibaya katika mechi mbili walizobakisha, kwani Wigan wana pointi 35 na mchezo mmoja mkononi.
Liverpool nao wameuonesha ulimwengu wa soka kwamba wanaweza bila Luis Suarez aliyefungiwa kwa kosa la kumng’ata mchezaji mwenzake wiki kadhaa zilizopita. Liverpool waliwakung’uta Fulham 3-1, Daniel Sturridge akipata hat trick yake ya kwanza kwa kuwapa zawadi ya mabao hayo Liverpool na kocha Brendan Rodgers aliyemwamini na kumsajili kwa mamilioni.
Liverpool wanashika nafasi ya saba baada ya kujikusanyia pointi 58.