Menu
in , , , ,

FAINALI KOMBE LA FA:

Arsenal vs Villa hapatoshi

Arsenal wanarejea Uwanja wa Wembley katika fainali ya Kombe la FA kwa mwaka wa pili mfululizo, leo hii wakikabiliana na Aston Villa.
Msimu uliopita waliibuka kidedea kwa kuwafunga Hull 3-2 katika mechi ambayo vijana wa Arsene Wenger walianza kulala 2-0 kabla ya kuzinduka.

Kiungo wa Wales, Aaron Ramsey ndiye aliyetia bao la ushindi na anasema kwamba ameingia kwenye historia kwa kufunga bao hilo muhimu na leo anarudi tena pale pale.

“Natumaini kwamba safari hii itakuwa rahisi zaidi kidogo kuliko wakati ule na hatutakuwa na haja ya kuchezesha watu wengi ili kufikia lengo hilo.

“Villa ni timu nzuri, ngumu na hivi karibuni wameanza kuwa kwenye kiwango kizuri nasi tunafahamu hilo,” anasema Ramsey.
Arsenal hawatakuwa na mshambuliaji wao, Danny Welbeck ambaye anauguza jeraha la goti. Wengine waliokuwa majeruhi lakini wamerejea kwenye mazoezi ni

Alex Oxlade-Chamberlain na Mathieu Debuchy wote wakiwa na tatizo la misuli ya paja huku nahodha Mikel Arteta akiwa na tatizo la kifundo cha mguu.

Hata hivyo, wakikosekana wote hao bado Arsenal hawana tatizo, kwani wanao wachezaji wengi, wakiwamo wale waliopandishwa kutoka kikosi cha vijana.

Kwa mara ya kwanza mwaka huu, kwenye Ligi Kuu Wenger aliweza kupanga kikosi cha wachezaji wale wale kwa mechi karibu tano mfululizo, kitu ambacho hakikuwa kawaida misimu iliyopita.

Shay Given wa Villa yupo fiti kucheza mechi ya leo baada ya kuwa na majeraha, ambapo Villa wameingia fainali kwa mara ya kwanza katika miaka 15 iliyopita.

Wachezaji waliokuwa majeruhi, Aly Cissokho, Kieran Richardson na Jores Okore wameweza kufanya mazoezi lakini Ciaran Clark atakuwa nje kwa sababu ya tatizo la goti.

Arsenal wakishinda watakuwa timu ya kwanza kutetea kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu Chelsea walipofanya hivyo 2010.

Kocha mpya wa Villa, Tim Sherwood aliyewawezesha vijana wake kubaki Ligi Kuu, japokuwa walimaliza nafasi moja tu juu ya zile zilizoshuka daraja, ameipania mechi hii.

Beki wa kati wa Arsenal, Per Mertesacker, akicheza, atakuwa na wajibu wa kumkabili vilivyo mshambuliaji matata wa Villa, Christian Benteke ambaye anadaiwa kwamba atahama kiangazi hiki, akihusishwa na Liverpool.

Hata hivyo, Sherwood anaamini kwamba Benteke atabaki Villa na anatarajia pia kumwanzisha kiungo
Jack Grealish aliyeng’ara kwenye mechi ya nusu fainali na aliwafunga bao Liverpool, naye ni mtu wa kuchungwa sana na Arsenal.

Arsenal na Villa wamepata kukutana kwenye michuano hii mara 10, ambapo Arsenal walishinda mara saba na Villa mara tatu.

Hata hivyo, mara ya mwisho kwa Villa kuwafunga Arsenal kwenye michuano hii ilikuwa 1974 ambapo walikwenda 1-1 Highbury na katika mechi ya marudiano Villa walishinda 2-0 dimbani Villa Park.

Villa wameshinda mechi moja tu kati ya tisa zilizopita dhidi ya Arsenal kwenye mashindano yote, nayo ilikuwa mechi ya ufunguzi wa ligi Agosti 2013 walipowapiga Arsenal 3-1 dimbani Emirates.

Arsenal wanaoshikilia kombe hilo ndio waliofanikiwa zaidi katika historia ya Kombe la FA, wakiwa wamelitwaa mara 11 sawa na Manchester United.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version