FAINALI za Kombe la Mataifa ya Ulaya zimetarajiwa kuanza kutimua vumbi wiki hii ambapo mchezo wa ufunguzi utachezwa jijini Rome nchini Italia, ambapo wenyeji watawakaribisha Uturuki ijumaa ya Juni 11.
Mosi, mashindano ya EURO 2020 yanafanyika mwezi Juni mwaka 2021 baada ya kuahirishwa mwaka jana kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona.
Pili, kwa mujibu wa shirikisho la soka la Ulaya, limeagiza kila timu inaruhusiwa kuwa na wachezaji 26 katika vikosi vyao kutoka idadi ya kawaida ya 23.
Idadi ya wachezaji itabidi kuwa 23 siku ya mchezo ambapo mwisho wa kuwasilisha majina ulikuwa tareje moja mwezi Juni mwaka huu. Hata hivyo timu zinaruhusiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji wa vikosi vyao kabla ya kuanza mashindano hayo, endapo kutakuwa na wachezaji walioumia wakati wa maandalizi hivyio kuondolewa kikosini na kuitwa wengine.
Tatu, mashindano ya Euro 2020 yanashirikisha timu 24 za barani Uropa. Timu hizo ni kama ifuatavyo; England, Italia, Uturuki, Wales, Uswisi, Denmark, Finland, Ubelgiji, Urusi, Croatia, Uholanzi, Ukraine, Austria, Macedonia kaskazini,Scotland,Jamhuri ya Czech, Hispania, Sweden, Poland, Slovakia,Hungary,Ureno,Ufaransa na Ujerumani.
Nne, timu hizo zimepangwa katika makundi mbalimbali. kundi A; Uturuki,Italia,Wales na Uswisi. Kundi B; Denamark,Finland,Ubelgiji na Urusi. Kundi C; Uholanzi,Ukraine,Austria, na Macedonia kaskazini. Kundi D; England,Croatia,Sctoland na Jmahuri ya Czech. Kundi E; Hispania,Poland,Slovakia na Sweden. Kundi F; Hungary,Ureno,Ufaransa na Ujerumani
Tano, bingwa mtetezi wa fainali hizo ni Ureno, ambao bado wapo na nahodha wao Cristiano Ronaldo. Urebno wamepangwa kutetea ubingwa katika kundi la kifo linalojumuisha vigogo Ufaransa na Ujerumani, huku ti y ya Hungary inachukuliwa kuwa kibonde ambacho kitatumika kutoa pointi kwa mataifa mengine matatu hayo.
Sita, waliotengwa wamerejeshwa vikosini. Karim Benzema amerejea katika kikosi cha Ufaransa baada ya kutengwa tangu mwaka 2015 kutokana na kashfa ya video ya ngono iliyomhusisha pia Mathieu Valbuena.
Inaonesha kocha wa Ufaransa Didie Deschamps hana chaguo lingine kwenye safu ya ushambuliaji hivyp anahitaji huduma ya Benzema katika mashindanohayo ili kufufua matumaini na hatimaye kunyakua taji hilo.
Naye kocha wa Ujerumani Joachim Low amewaita wakongwe Thomas Muller na Matt Hummels katika kikosi chake cha Euro 2020 ili kuwasaidia wachezaji chipukizi wa nchi hiyo. Inaonekana kocha huyo anakiri kuwa mipango ya kuendeleza chipukizi katika kikosi chake haijazaa matunda.
Saba, fainali kucheza miji tofauti. Mashindano ya Euro 2020 ni tofauti na mengine ya miaka ya nyuma ambako yalikuwa yanafanyika katika nchi moja mwenyeji kuanzia hatua ya makundi hadi fainali.
Michuano hii tofauti yake ni kwamba inashirikisha majiji tofauti, Rome (Italia),London (England), St.Petersburg (Urusi),Sevilla (Hispania) na mengineyo. Michezo ya nusu fainali na fainali yote itachezwa kwenye uwanja wa Wembley katika jiji la London.
Michuano hii imeshirikisha majiji ambayo yalitakiwa kuthibitisha uenyeji wao. Mtindo huuu umetajwa kuwa unasambaza mchezo wa soka katika maeneo mengi badala ya wengi kusubiri Telivisheni au kusafiri kwenye nchi mwenyeji kama ilivyokuwa zamni. Sasa ni mgawanyo wa majiji kuwapa wapenzi wa kandanda raha ya soka kote barani Uropa.
Nane, kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo timu zinatakiwa kuchagua magolikipa watatu. Makipa hao wanaweza kubadilishwa wakati mashindano yakiwa yanaendelea ikiwa kutakuwa na hali ya ugonjwa au majeraha yatakayomwondoa mashindanoni kipa yeyote.
Tisa, mashindano hayo yanatarajiwa kutazmwa na mamilioni ya mashabiki kote duniani, huku baadhi yao wakitarajiwa kutazama kupitia mitandaoni (Live streaming).
Kumi, fainali ya mashindano hayo itafanyika kwenye uwanja wa Wembley, ambako ni vigumu kubashiri timu gani itafanikiwa kutangulia kwenye mchezo huo na ipi itafanikiwa kunyakua ubingwa huo na kuzoa sifa kote Uropa.