Mwishoni mwa mwezi uliopita bondia wa Tanzania Ibrahim Class alipanda ulingoni kupambana na mpinzani wake Simon Ngoma raia wa Zambia katika uzani wa Junior Lightweight wa GBC.
Kwenye mchezo huo Ibrahim Class alitwaa ubingwa wa Dunia wa GBC kwa ushindi wa majaji wote watatu. Jaji wa kwanza alimpa pointi 95 dhidi ya 91 za Mzambia. Jaji wa pili alimpa Class pointi 98 dhidi ya 88 za Mzambia.
Jaji wa tatu alimpa Classa pointi 98 dhidi ya 88 za Mzambia katika pambano kali lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es salaam. Licha ya ushindi huo kuna mambo matano muhimu ambayo bondia huyo,makocha na wadau wa mchezo huo wanatakiwa kuyafahamu.
1. Kocha mpya kuboresha ufundi.
Ibrahim Class anahitaji maarifa mapya kutoka kwa mwalimu mpya. Mtindo wake wa upiganaji ni mzuri, lakini amekuwa na kasoro mbalimbali katika upiganaji. Inawezekana bondia wa Zambia akalaumiwa kwa mtindo wake wa upiganaji wa ngumi za holela na kupiga popote kiasi cha mwamuzi Pendo Njau kumuonya mara kadhaa, lakini Class anahitaji walimu ambao watakuza kipaji chake na kuongeza maarifa. Kifundi Ibrahim Class anategemea zaidi kipaji, hivyo kujikuta akishindwa kumdhibiti mpinzani anayeshambulia muda wote kwa kasi na ngumi za kila upande. Kocha mpya atamwezesha kuimarisha upungufu unaojitokeza kwenye mapambano mengine.
2. Stamina
Class alianza pambano hilo kwa kasi na kumdhibiti mpinzani wake katika raundi ya kwanza, ambapo alifanikiwa kumkalisha chini Mzambia huyo. Hata hivyo uhodari na uwezo wa bondia huyo ulichangia pambano kuendelea hivyo kumpa wakati mgumu Class.
Katika raundi ya tatu bondia Ibrahim Class aliangushwa chini kutokana na ngumi kali za mpinzani wake. Hata hivyo suala la kuanguka chini mara kwa mara lilikuwa jambo la kawaida kwa mabondia wote. Class alikuwa anakosa balansi au
uwiano katika kupambana na kulinda stamina yake kwenye mchezo. Kukwepa konde na mpinzani kisha kupepesuka na kuanguka chini ni kukosa balansi.
Hivyo anatakiwa kuimarisha kiwango chake cha stamina. Jinsi anavyoangushwa angushwa kirahisi ni hatari kwake. Kuwa bondia wa kimataifa kitendo cha kuangushwa angushwa kina madhara kisaikolojia. Sio wote wanaweza kurudi mchezoni kama alivyofanya Antony Joshua dhidi ya Vladimir Klitscho pale Wembley.
Lennox Lewis alipigwa ngumi ya taya pale Afrika kusini na Hashim Rahman akapoteza balansi na kuanguka, hakuyrudi tna mchezoni. Kwahiyo Ibrahim Class anatakiwa kujua mabondia wa kimataifa wanatakiwa kuondokana na mianya kama kukosa stamina ili kuwa na ubora.
3. ‘Focus’ yake iko chini.
Mfano mpinzani wake alikuwa anatafuta nafasi ya kumpiga makonde ya ‘Upper cut’ yaani kutokea chini ya kidevu, ili kumaliza mchezo. Kwa upande wake Ibrahim Class hakuwa na makonde yale yanayolenga sehemu moja, yaani yenye ‘focus’ mahali fulani penye udhaifu wa mpinzani wake.
Kwa mfano anapokuwa amemuumiza bondia iwe juu ya jicho,jichoni au akiwa amempasua sehemu inabidi awe anapalenga zaidi hapo kuongeza maumivu na kichapo. Tunaweza kumsifia Ibrahim Class kwa uwezo wake mzuri wa kukwepa makonde, na mojawapo ni yale ya ‘Upper cut’ kwani yangetua barabara mambo yangekwua mabaya zaidi kwake.
Hiyo ni ishara kuwa bondia anatakiwa kuwa na ‘focus’ya eneo au mbinu fulani ili kummaliza mpinzani wake. Hata kwenye ,mpira wa miguu iko hivyo, ukiona udhaifu kwa mabeki wa pembeni basi unatakiwa kutumia mianya hiyo kupitia maeneo hayo na kuwachapa mabao wapinzani.
4. ‘Timing’ ni nzuri
Hili ni eneo analostahili sifa bondia wetu Ibrahim Class kwa sababu ana makonde mazuri, anaweza kukwepa na kumzunguka mpinzani. Ngumi za ana kwa ana nazo anatakiwa kuzimudu na aongezewe ufundi. Ingawaje wengi wanaziita ngumi za
kuvizia, lakini ukweli Ibrahim Class alikuwa anapiga ngumi za kiufundi zaidi, badala ya kuhangaika kupigana kama ngumi za mitaani alizofanya mpinzani wake.
Kupiga ngumi kimahesabu ndiko anakotakiwa kuboresha zaidi. alifanya ‘timing’ nzuri kwa kumchapa makonde katikati ya uso wa mpinzani na kichwani. Zilikuwa ngumi nzuri na hili eneo anaweza kuongezewe maarifa kwa vile ameonesha uwezo mzuri.
5. Kapeti la Ulingoni
Miongoni mwa sababu zinazolalamikiwa ni ubaya wa ulingo waliotumia mabondia hao. Ulingo huo ulikuwa kikwazo kwa Ibrahim Class katka ruandi za 8,9, na 10 ambako angeweza kushinda kwa KO kama siyo kapeti la ulingoni kuteleza. Mabondi wote wawili walipatwa nah ii shida ambao waandaaji wanatakiwa kubeba mzigo wa lawama kuweka kapeti linaoharibu mchezo.
Mwisho aapenda jitihada za bondia Ibrahim Class lakini lazima pafanyike kitu. Pengine ni kwa sababu ya pambano kuhwa la kwanza kwake kimataifa, hivyo anaweza kutafuta uzoefu kutokana na mchezo huo.