* Serge Aurier kuchukua nafasi ya Sagna
KIPA namba mbili wa Arsenal aliyedaka mechi zote za Kombe la FA hadi kutwaa taji hilo, Lukasz Fabianski amekataa ofa ya dakika ya mwisho ya Arsenal kubaki Emirates.
Fabianski ambaye hukaa benchi mbele ya raia mwenzake wa Poland, Wojciech Szczesny ameamua kuondoka baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu.
Fabianski ni kipa mzuri na hata Szczesny aliposhuka kiwango na kutupwa benchi ndiye alidaka mechi zote, hata baada ya mwenzake huyo kupewa kadi nyekundu kwenye mechi dhidi ya Bayern Munich katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Amewadakia The Gunners kwa miaka saba lakini inaelekea hafurahishwi na kukaa kwake benchi miaka yote hiyo akiwa namba mbili. Kipa namba tatu, Vito Manonne naye aliamua kuondoka msimu uliopita akajiunga na Sunderland ambako ni tegemeo.
Fabianski (29) anatarajiwa kujiunga na klabu za Ujerumani, ama Schalke au Borussia Dortmund, nchi ambayo ni jirani na Poland. Kocha Arsene Wenger anamhusudu Fabianski lakini alishindwa kumuamini kumpa nafasi ya kwanza mbele ya Szczesny.
SERGE AURIER KUMBADILI SAGNA?
Katika hali ile ile ya watu wa taifa moja, beki wa kulia kutoka Senagal, Serge Aurier anayecheza Toulouse ya Ufaransa anatarajiwa kusajiliwa na Arsenal kuziba nafasi ya Msenegali mwenzake, Bacary Sagna aliyemaliza mkataba na anafanya mazungumzo kujiunga Manchester City.
Aurier anayethaminishwa kwa pauni milioni saba amesema wazi kwamba hawezi kukataa ofa kutoka klabu yoyote ya Ligi Kuu England, hata zilizopanda daraja msimu huu kwa sababu ni ligi kubwa.
Arsenal wameshaanza mazungumzo na klabu yake, ambapo watalazimika kutoa fungu huku Sagna, kama akiondoka, atasajiliwa na klabu yoyote pasipo kuwalipa Arsenal ada, kwani sasa ni mchezaji huru.