*Tottenham washinda, nafasi ya saba
*Liverpool, Man City na Arsenal vinara
Emmanuel Adebayor ameanza mechi ya kwanza katika msimu huu wa Ligi Kuu ya England (EPL) na kuwawezesha kupata ushindi wa kwanza tangu matatizo yaliyowakumba.
Adebayor alifunga mabao mawili kati ya matatu yaliyowawezesha Tottenham Hotspur kupata ushindi dhidi ya Southampton waliojituliza kwa mabao mawili.
Adebayor alieleza baada ya mechi kwamba amepata afueni baada ya mwaka wa tabu, ambapo alifiwa na kaka aliyekuwa mtu muhimu sana kwake na kisha kutengwa kwenye kikosi cha kwanza.
Ndio kwanza alipangwa kuanza mechi tangu msimu uanze, ambapo kocha Andre Villas-Boas alifikiria kumtoa kwa mkopo au kumwacha, lakini kaimu kocha aliyemrithi, Tim Sherwood alimanzisha, akimwambia anamtambua alivyo mchezaji mzuri tangu Arsenal na Manchester City.
Bao jingine la Spurs lilisaidiwa kuwekwa kimiani na mchezaji wa Saints, Jos Hooiveld katika jitihada zake za kuokoa majalo ya Danny Rose.
Mabao ya Saints yalifungwa na Rickie Lambert na Lalana.
Hata hivyo, Southampton walionesha udhaifu mkubwa katika kudhibiti mashambulizi, kuokoa mipira iliyokuwa ikipita na pia walikuwa wabovu katika utoaji pasi, vinginevyo wangeweza kuibuka washindi kwenye mechi hiyo ya kuvutia.
Ushindi wa Jumapili hii umeonekana kumpa kocha wa muda, Sherwood kiburi, ambapo ameshasema anaitaka kazi hiyo, lakini si kwa muda bali moja kwa moja, japokuwa amesisitiza ni juu ya Spurs kuona kama anafaa.
Kwa matokeo hayo Spurs wamefikisha pointi 30 na wanashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, wakati Southampton wapo nafasi ya tisa, ya nane ikishikwa na mabingwa watetezi, Manchester United.
Katika mechi nyingine ya vuta nikuvute, Everton wakicheza ugenini Liberty Stadium walifanikiwa kuwakandamiza Swansea 2-1, katika mechi ambayo nusura iishe kwa sare ya 1-1 kutokana na mvutano uliokuwapo.
Everton wapo vizuri, ambapo wamefikisha mechi 10 bila kupoteza hata moja na sasa wanashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Kocha wa Everton, Roberto Martinez amepata kuwachezea Swansea kabla ya kuwa kocha wao na kuwawezesha kupanda daraja – League One – mwaka 2008, na amesema kurudi hapo kusini mwa Wales kulimpa hisia kali.
Everton wana rekodi kubwa katika Ulaya, kwa sababu katika bara lote, ni Roma ya Italia na Bayern Munich wa Italia waliopoteza mechi chache zaidi kuliko Toffees, hivyo wanaingia msimu wa sikukuu za Krismasi wakiwa wanajiamini.
Kwa matokeo ya Jumapili hii, Liverpool wanaongoza ligi wakiwa na pointi 36 wakifuatiwa na Manchester City wenye pointi moja pungufu wakifungana na Arsenal katika nafasi ya tatu.
Hata hivyo, Arsenal na Chelsea wana mchezo mmoja mkononi na ni baina yao Jumatatu hii, tofauti na wenzao wenye mechi 17 walizocheza tayari.
Everton wana pointi 34 wakati Chelsea wana 33, Newcastle na Spurs (30), Man United 28, Southampton 24, Stoke 21, Swansea na Hull 21, Aston Villa na Norwich 19, Cardiff 17, West Bromwich Albion 16, West Ham 14, Crystal Palace na Fulham 13 kila moja na Sunderland 10.