Siku moja baada ya Everton kukung’utwa nyumbani kwao Goodison Park
mabao 5-2 na Arsenal, wamemfukuza kazi kocha wao, Ronald Koeman.
Mdachi huyu aliyeingia hapo akitoka Southampton na akiwa na rekodi
nzuri aliwaimarisha sana Everton hadi mwishoni mwa msimu uliopita
lakini mwanzo wa huu wa sasa haukuwa mzuri.
Kichapo cha Jumapili hii kiliwashusha hadi kwenye eneo la kushuka
daraja, Koeman akanukuliwa akisema kwamba bado angeweza kurekebisha
mambo kwenye kikosi ambacho kinaye nahodha wa zamani wa Manchester
United na Timu ya Taifa ya England, Wayne Rooney.
Taarifa ya klabu imeeleza kwamba menejimenti wanamshukuru kocha huyo
kwa kufanya nao kazi kwa miezi 16 hivi. Wanashika nafasi ya 18 kwenye
msimamo wa ligi wakiwa na alama nane tu kutokana na mechi tisa.
Koeman anakuwa kocha wa tatu katika Ligi Kuu ya England (EPL) kufutwa
kazi msimu huu, akiwafuata Frank de Boer aliyekuwa Crystal Palace na
Craig Shakespeare aliyefutwa kazi Leicester baada ya kuwa amemrithi
Claudio Ranieri aliyewapa ubingwa misimu miwili iliyopita.
Koeman (54) aliwaongoza Everton kumaliza katika nafasi ya saba msimu
wake wa kwanza hapo anaondoka kama mshahara wa kufanya vibaya kwneye
ligi inayoendelea licha ya kupewa na kutumia pauni milioni 140 msimu
wa kiangazi kwa ajili ya kusajili.
Siku karibu 10 zilizopita, mwanahisa mkubwa zaidi wa Everton, Farhad
Moshiri alimhakikishia Koeman kwamba yu naye na anamuunga mkono
kuendelea na kazi hapo na wana Tofees baada ya kuwa wamefungwa 1-0 na
Burnley, wakaja kutoshana nguvu na Brighton kabla ya kufungwa na Lyon
kwenye michuano ya Ligi ya Europa.
Wapo na Arsenal kwenye Ligi ya Europa ambapo wenzao wameshinda mechi
zao zote humo na wakaja kuwaangushia kisago mbele ya washabiki wao
Goodison Park. Vijana hao wanaotoka eneo la Merseysiders wana nafasi
finyu ya kusonga mbele kwenye mashindano ambayo msimu jana Manchester
United walikuwa mabingwa, kwa sababu wanashika mkia baada ya kuwa
wamefungwa pioa na Atalanta na kwenda sare na Apollon Limassol.
Kupitia mtandao wa Twitter Jumapili Koeman alisema haingewezekana
wawashinde Arsenal ambao wakiwa mbele kwa mabao 2-1 wao Everton
walipungukiwa wachezaji na kubaki 10 kutokana na mmoja wao kupewa kadi
nyekundu.
Aliwasili klabuni kwa ajili ya mazoezi kwenye viwanja vya Finch Farm
kama kawaida leo Jumatatu lakini ghafla na pasipo kutarajiwa,
Mwenyekiti Bill Kenwright na Ofisa Mtendaji Mkuu Robert Elstone
waliwasili hapo na baada ya muda ikatangazwa kwamba Koeman alikuwa
amefukuzwa kazi.
Klabu wanajiandaa kwa ajili ya mechi ya Kombe la Ligi, maarufu msimu
huu kama Carabao Cup na wanacheza dhidi ya Chelsea Jumatano hii.
Makocha waliopata kufanya kazi Everton ni pamoja na Howard Kendall
(1990-93), Mike Walker (1994), Joe Royle (1994-97), Howard Kendall
(1997-98), Walter Smith (1998-2002), David Moyes (2002-13), Roberto
Martinez aliyerithiwa na Koeman.
Zipo tetesi kwamba kocha wa zamani wa klabu hiyo, David Moyes atarudi
hapo. Huyu alichukuliwa kwenda Manchester United ambako alishindwa
kazi ndani ya mwaka mmoja na kufukuzwa. Kenwright alichukua muda
mwingi kujadiliana na Moyes hatimaye kukubali kuondoka kwake wakati
huo, kutokana na mchango wake mkubwa hapo Goodison Park.