Wachezaji Jonny Evans wa Manchester United na Papiss Cisse wa Newcastle wamekiona cha moto kwa tabia chafu ya kutemeana mate uwanjani.
Chama cha Soka (FA) kimechukua uamuzi wa kumfungia Evans mechi sita na Cisse mechi saba kwa makosa yao.
Wakati Evans (27) alikana kosa huku akitetewa na kocha wake, Louis van Gaal, upande mwingine Cisse (29) alikiri kosa lake na hakutaka kupoteza muda.
Cisse, ambaye ni mshambuliaji amepewa adhabu ya mchezo mmoja zaidi ya mlinzi wa Man U, Evans, kwa sababu ni Desemba tu alipewa adhabu kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Everton, Seamus Coleman.
Kwa wachezaji wawili hawa, hakuna ruhusa ya kukata rufaa na adhabu zinaanza mara moja, ikimaanisha kwamba Evans atakosa mechi ya Jumatatu ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Arsenal.
Kadhalika Evans ambaye ni raia wa Ireland Kaskazini atakosa mechi za Ligi Kuu ya England (EPL) dhidi ya Tottenham Hotspur, Liverpool, Aston Villa, Manchester City na Chelsea.
Cisse hatakuwa dimbani kwenye mechi za EPL dhidi ya Everton, Arsenal, Sunderland, Liverpool, Spurs, Swansea na Leicester.
Taarifa ya FA imesema kwamba licha ya Evans kukana kosa na kutaka kupinga mashitaka, ukweli umethibitika dhidi yake.
Mwamuzi Anthony Taylor wala wasaidizi wake wanasemwa kwamba hawakuona kutemeana mate baina ya wachezaji hao wawili, lakini video inaonesha wazi wakitemeana mate.
Jopo la watu watatu lililoundwa na waamuzi wa zamani lilipitia mkanda wa video Alhamisi hii na kukubaliana kwamba walifanya makosa hayo, walitakiwa kutolewa nje na kupewa adhabu zaidi, ndiyo maana wamepewa kifungo hicho.
Katika taarifa take, Evans alisema: “Napenda kuweka wazi kwamba sikumtemea mate Papiss Cisse. Baada ya kuamka asubuhi ya leo (Alhamisi) nimeshitushwa kuona vyombo vya habari vikinizungumzia juu ya mechi ya usiku uliotangulia.”
Kocha wa Man United, Van Gaal akasema: “Sidhani kwamba Jonny Evans hutemea watu mate. Hakujua kwamba alikua akimtemea mate. Amesema hivyo pia. Namwamini. Kwangu, suala hili limemalizika.”
Baada ya kukubali kosa lake, Cisse anayetoka Senegal aliomba radhi, akisema kwamba alifanya hivyo akiwa anatoa mwitikio kwa jambo ambalo halikumpendeza alilofanya.