ikadhaniwa kwamba bahati ingekuwa yao, wakiwa wamecheza mechi nyingi nyumbani.
Wengi waliwaza kwamba michuano ya Euro 2020 iliyomalizika majuzi ingekuwa fursa nzuri kwa England kurejesha heshima yake na kutwaa kombe kubwa baada ya muda mrefu.
Timu ya Taifa ya England – Three Lions walijipanga na kwa jinsi walivyoanza vyema hatua kwa hatua, ilionekana kwamba vijana wa kocha Gareth Southgate wangeweza kuchukua kombe kwenye michuano iliyoahirishwa mwaka jana kwa sababu ya janga la Covid-19.
Muda ukasonga huku vijana hao wakichanga mbuga hadi kuingia fainali – wadau wakawa wanawaza iwapo uwapo wao nyumbani katika Uwanja wa Taifa – Wembley ungewasaidia kuwapiga Timu ya Taifa ya Italia – Azzurri, chini ya kocha Roberto Mancini.
Wakaingia kwenye fainali yenyewe, wakaanza vyema kwa kupata bao la kuongoza mapema kabisa; watu wakaona ndio ubingwa unakaribia. Wakaingia kipindi cha pili wakiwa bado wanaongoza, ikadhaniwa kwamba bahati ingekuwa yao, wakiwa wamecheza mechi nyingi nyumbani.
Wakati watu wakiendelea na shughuli zao, waliweka macho na masikio kwenye mechi husika, anga la London na Wembley hasa likiwa limehanikizwa na mtanange uliokuwa ukiendelea chini yake.
Watu walijawa kihoro, huku washabiki wakijaa uwanjani kama ambavyo haikupata kutokea tangu kuanza kwa Covid-19 kulikosababisha washabiki wengi kuzuiwa uwanjani.
Homa ya pambano ikaendelea huku pumzi za washabiki Zaidi ya 60,000 zikiwa juu, hasa baada ya Italia kusawazisha bao lile hadi kufika muda wa cangamoto za mikwaju ya penati.
Three Lions na washabiki wao walikuwa katika kipindi kigumu wakati wa changamoto hiyo, kutokana na baadhi ya wachezaji kukosa mikwaju yao na ikaonekana bahati ile ilikuwa kana kwamba inayeyukia upande wa Wataliano.
Ikafika wakati wa kukaribia mwisho, mpira ukikaribia kutoka mguuni mwa kinda la Arsenal, Bukayo Saka, na baada ya hapo, hakuna tena kitu kilichoonekana cha maana kwa simba hao na washabiki wa England, kwani mkwaju haukuingia wavuni, na ulikuwa wa mwisho na kuashiria kwamba Italia walikuwa mabingwa kwa kuwazidi kupata kati ya penati tano tano ambazo kila timu ilipewa.
Ilibaki simanzi kubwa kwa wachezaji na washabiki wa England, waliokosa penati wakitulizwa lakini wasitulie bali kubaki kulia; hali iliyomzidia sana Saka.
Kwa matokeo hayo, haingejalisha kitu kwamba ilikuwa ni miaka 55 imepita tangu nchi ione siku kama hiyo, wala kwamba walikuwa na umiliki wa mpira wa jumla kwa asilimia 33, ikimaanisha Azzurri walikuwa juu. Nani wa England angehangaika na mambo kama kutazama idadi ya mashuti, Italia wakiwa juu kwa 14-4.
Ukweli ni kwamba taarifa za kina juu ya mechi husika zilitarajiwa kupotea katika historia kwa Waingereza; nani miongoni mwao angehangaika nazo baada ya kupigwa? Nani angetaka kujiongezea simanzi? Wanegekuwa wameshinda sawa – zingetangazwa na kuchapishwa sana, lakini sasa vichwa vyao vilikuwa chini.
Labda ni rahisi kukumbukia yale waliyoshuhudia ya aina chanya = kama vile mguu wa beki wa pembeni, Luke Shaw ulivyowapatia England bao la kuongoza mapema. Lakini hata hivyo, tangu hapo mwenye kujua mpira alitambua ni aina gani ya gemu walitakiwa kuonesha – kuongeza kasi kila idara na kushambulia pia na si kuegesha basi.
Kilikuwa kipindi ambacho walitakiwa kuwakomalia Wataliano na si kubaki kama wanyonge. Lakini, wakiwa wanaongoza kwa bao moja, huku wakiwa na baadhi ya washambuliaji wazuri zaidi wa Ulaya kama si dunia, England hawakuonesha uboara wao, na hiyo iliwapa hofu washabiki.
Wakaonekana kuelemewa na Wataliano na hakika hivyo ndivyo vitu vilivyoanza kuwatenganisha nyota hao wa England na utukufu uliotarajiwa kwao. Baada ya muda wa kucheza uwanjani, zikapa penati, na walikuwa jamaa watatu wazuri tu – Saka, Marcus Rashford na Jadon Sancho waliokosa penati zao.
Majanga hayo yalitarajiwa na wengine tangu mapema, hasa wachezaji walipoonekana kuwa wazito, wakiikalia gemu tu badala ya kutingisha na kupata mabao zaidi kuwachanganya vijana wa Manchini anayejulikana vyema hapa kwani amekuwa kocha England ngazi ya klabu.
Walikuwa wamejitahidi hatua kwa hatua hadi fainali, lakini siku ile hawakuonekana kama waliokuwa tayari kunyanyua kombe lile la Euro, kuupokea utukufu ule na kuirejesha heshima ya England kwenye soka baada ya madhila ya kuishia hatua kama za robo fainali kwenye mashindano makubwa kwa muda mrefu.
Dakika nyingi za mpira ule zilikuwa kwa England kama mtu anayetembea angani juu ya kamba, akiwa katika hatari ya kuanguka na kupoteza heshima, hakika kadiri mwisho ulivyokaribia, ndivyo wasiwasi, hofu na mkato wa tamaa vilivyowazidia wana England, mapigo ya moyo yakiwa hayaendi tena vizuri. Dakika za huzuni zilikuwa zikijongea kwa kasi.
Wachezaji walijaribu walichoweza, wakiwa watano pale nyuma na kujaribu kudhibiti fursa zote za Wataliano waliokuwa wakifungua nafasi kupokea mipira. England walishindwa kudhibiti boli lile baada ya kuwa wamefunga katika sekunde ya 116 tu.
Italia hawakuwa wakali kivile, lakini England wakashindwa kuwavurugia mpango wao wa mechi ile. Hawakuonekana kuwa na fursa ya bao la pili karibu nao. Italia walifanikiwa kuweka kambi kwenye nusu ya England uwanjani pale kirahisi.
Italia walijaribu kupata mabao kama ambavyo wachezaji Lorenzo Insigne na Federico Chiesa walivyoachia mikwaju ya chini chini langoni mwa England.
Jorginho alianza kuwanyanyasa England huku Marco Verratti akimpelekesha puta Mason Mount wa England.
Muda wa nyongeza washabiki walianza kuonesha kuchoshwa na wachezaji wao, wakitoa sauti kali na za wazi kwao, hasa kwenye zile dakika 15 za mwisho. Wachezaji hawakuwa na la kufanya, maana hakika walionesha kwamba walishachoka.
Dakika 120 zikamalizika na mwamuzi Björn Kuipers akawaelekeza kwenye changamoto ambazo ni pasua roho hasa – mikwaju ya penati. Southgate anasema kwamba nyakati za changamoto za mikwaju ya penati ni ngumu na kwa kawaida hazimtambulishi mtu. Na kweli, alimaanisha kwamba mchezaji mzuri zaidi anaweza kukosa, na golikipa mbaya akaokoa.
Mwenyewe anakumbukia kukosa kwake panati 1996; siku hiyo watatu wa vijana wake aliowaamini ikawa zamu yao. Ufalme wa soka ukawaponyoka na kwenda kwa Wataliano. Kwa hiyo kwa England ni mwendo wa kuendelea kusubiri tena lini watatwaa taji kubwa na kuipa falme yao heshima.