Ligi Kuu ya England (EPL) imefikia hatua ya ushindani mkubwa katika kuamua timu zipi zitafuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), huku Chelsea wakipewa nafasi zaidi kutwaa ubingwa.
Ushindi wao mwembamba wa 1-0 dhidi ya West Ham umeendeleza pengo la pointi tano dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City ambao pia walipata ushindi wa 2-0 dhidi ya Leicester.
Arsenal wamebaki nafasi ya tatu baada ya kuwafunga QPR 2-1 wakiwa ugenini ambapo wanapigania zaidi kuingia UCL kuliko kutwaa ubingwa, kama ilivyo falsafa ya kocha wao, Arsene Wenger.
Manchester United walikuwa nusura waende suluhu na Newcastle lakini walijitahidi dakika za mwisho na kupata bao moja muhimu kwa maana ya kujikusanyia pointi tatu na kuwa katika nafasi ya nne.
Liverpool waliobadilika na kuanza kuwa na kasi katika mwaka huu, wanafuatia nafasi ya tano wakipanda kutokana na kufanikiwa kuwafnga Burnley 2-0 na kumpa matumaini kocha Brendan Rodgers ambaye alishafikiriwa kufukuzwa. Mwaka huu hawajafungwa hata mechi moja, tofauti na mwaka jana walipokuwa wakioga vichapo mara kwa mara.
Katika matokeo mengine ya katikati ya wiki, Stoke waliwabamiza Everton 2-0. Tottenham Hotspur wakawafungwa Swansea 3-2, wakati Jumanne Aston Villa waliona mwezi kwa kuwashinda West Bromwich Albion 2-1, Hull wakaenda sare ya 1-1 na Sunderland huku Southampton wakiwafunga Crystal Palace 1-0.
Timu tatu za mwisho na zilizo kwenye hatari ya kushuka daraja ni Leicester wenye pointi 18, Burnley pointi 22 sawa na QPR. Villa wamefanikiwa kuchomoka humo na sasa wana pointi 25 lakini Sunderland pia wanatakiwa kujirekebisha kwani wana pointi 26 tu.