*Man United wakong’ota, Arsenal wapigwa
Ligi Kuu ya England (EPL) imeanza kwa mapigo tofauti, ambapo mabingwa watetezi wamefanikiwa kushinda mechi ya kwanza dhidi ya Swansea City.
Vijana wa David Moyes walifanikiwa kupata mabao 4-1 dhidi ya wale wa Michael Laudrup, na kuweka alama nzuri katika mwanzo wa EPL.
Moyes alikuwa na mwanzo mgumu, baada ya klabu kuwa chini ya kocha Alex Ferguson kwa miaka 26, lakini akiwa ugenini katika uwanja wa Liberty, alifanya kweli, kwa Robin van Persie na Danny Welbek kufunga mabao mawili kila mmoja.
Liverpool walio kwenye vita ya kuhakikisha wanabaki na mshambuliaji wao namba moja, Luis Suarez, walifanikiwa kuwashinda Stoke Cit bao 1-0, lenyewe likifungwa na mpachika mabao aliyotoka Chelsea msimu uliopita, Daniel Sturridge.
Katika mechi hiyo, Stoke walishindwa kusawazisha licha ya kupatiwa penati , ambayo kipa mpya wa Liverpool, Simon Mignolet aliipangua.
Arsenal wameanza ligi kwa simanzi kubwa, baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 nyumbani Emirates kutoka kwa Aston Villa ambao mwaka jana nusura washuke daraja.
Mshambuliaji wao mahiri, Christian Benteke alifunga mabao mawili na Antonio Luna akaongeza la tatu, ambapo kwa Arsenal Olivier Giroud alifunga mapema kabla ya kipa wa Arsenal, Wojciech Szczesny kuokoa penati.
Yatakuwa matokeo yaliyowakasirisha wadau wa Arsenal, kwa kuwa hawajasajili mchezaji nyota, licha ya kuwa na fedha na pia kuuza wachezaji kadhaa.
Katika mechi nyingine, Norwich na Everton walitoka sare ya mabao 2-2, Fulham wakawakanyaga Sunderland 1-0 kama walivyofanya Southampton kwa West Bromwich Albion.
Wageni katika EPL Cardiff waliugulia kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa West Ham United, ambapo Jumapili hii Chelsea wanawakaribisha Hull, Tottenham Hotspur wakiwa wageni wa Crystal Palace na Jumatatu Manchester City watakuwa wenyeji wa Newcastle.