Utakapofika wakati na mechi 92 zilizobaki za Ligi Kuu ya England (EPL) kurejea kwa ajili ya kumaliza msimu wa 2019/2020, basi vitatumia viwanja huru na si mambo ya nyumbani na ugenini tena.
Na katika mechi na viwanja husika, inavyoelekea watakuwa ni wachezaji, makocha, madaktari, waamuzi na maofisa wengine wasiozidi mia kadhaa watakaoingia uwanjani, huku washabiki wakifuatilia majumbani mwao.
Kutokana na wazo la kutumia viwanja huru na si kila klabu kutumia wa kwake, inaelezwa kwamba vinatafutwa viwanja nane au 10 hivi ili vitumiwe na klabu zote kwa mechi zilizobaki. Viwanja vyote vinadhaniwa vitakuwa vya klabu za EPL lakini hakuna klabu hata moja itakayocheza mechi kwenye uwanja wake.
Hatua hiyo inatokana na ushauri wa polisi, lakini si klabu zote zinazounga mkono, japokuwa kwa ujumla ni wazo linaloonekana kuwa na mashiko na mantiki.
Viwanja vinavyochaguliwa vitakuwa vile vyenye leseni kutoka kwa mamlaka ya usalama wa viwanja – kwa ajili ya kuhakikisha watu wanakaa mbalimbali na kuhakikisha kwa nje kuna umbali wa kutosha kutoka kwenye makazi ya watu ili kuepuka maambukizi.
Upo uwezekano wa uwanja wa klabu ya Brighton – Amex Stadium kutumiwa jinsi hiyo kwani upo mbali sana na makazi ya watu. Uwanja mwingine ni Etihad wa Manchester City,
Klabu za EPL zilikuwa kama kitu kimoja kwenye mkutano wa saa tatu unusu kupitia video mwshoni mwa wiki, wakisema kwamba bado walikuwa wamesimama kidete na kudhamiria kwamba wahakikishe msimu unamalizika kwa emchi kuchezwa.
Mechi husika zilisitishwa tangu Machi kwa sababu ya kuzuka kwa janga la kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu. Hata hivyo, muungano huo wa klabu haujawa timilifu, kwani inaelezwa kwamba klabu walau zaidi ya moja zinataka msimu ufutwe kwa sababu ya vigingi kwa ajili ya kurudia soka ni vikubwa mno.
Angalizo muhimu linaloumiza vichwa vya wachache ni iwapo kucheza hakuwezi kuziweka afya za wachezaji, wafanyakazi wa klabu na viwanja husika katika hatari, na vivyo hivyo familia zao.
Mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero anasema kwamba bado anaogopa kurejea uwanjani kumaliza msimu kwa sababu ya kuhofu anaweza kuambukizwa kisha akaenda kuambukiza wanafamilia wake na kuteseka kwa Covid-19. Wapo wachezaji wengine waliojawa hofu hii pia.
Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) kimeweka bayana kwamba afya ya wachezaji na usalama wao ndicho kipaumbele kuliko jambo jingine lolote. Kinasema kwamba, kwa sababu hiyo, hakiwezi kuwaweka katika hatari.
Baadhi ya wachezaji, inaeleweka, wanataka PFA itoe tamko kwa niaba yao, kwamba hawataki kuingizwa kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo unaoua maelfu ya watu kila siku katika nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Uingereza ambayo imeamuru watu wasalie majumbani mwao kwa zaidi ya mwezi sasa.
Kwa upande mwingine, wapo wachezaji wengine – ambao ni wengi zaidi, na kwa sababu nyingine nyingi sana, wanataka ligi iendelee na imalizike. Mwafaka utafikiwa? Pengine lakini ni wazi kuna klabu zitakosa wachezaji wake kwenye timu zao iwapo zitaanza kucheza, kwani hawatakuwa sawa kisaikolojia na hivyo utimamu wa mwili.
Bodi ya EPL imetoa taarifa ndefu baada ya mkutano huo na kusema kwamba ilikubaliwa kwamba PFA, LMA, wachezaji na makocha ni watu muhimu katika mchakato huo na hivyo wataendelea kufanya nao mawasiliano ili hatimaye kufikia uamuzi mzuri.
PFA inatambua kwamba serikali na Bodi ya EPL wanalotaka ni la msingi – kwamba soka irejee mapema iwezekanavyo wakati ikiwa ni salama kufanya hivyo. Ijumaa hii serikali ilianza jozi za mikutano na taasisi za michezo kwa ajili ya kuchora ramani ya kurejea kwenye mechi za soka na nyinginezo.
Kuna baadhi ya wachezaji na wafanyakazi wa klabu mbalimbali wanaoona kwamba suala la ligi kurejea tena kuchezwa msimu huu ni watu kujipa moyo tu na wala halitatokea. Hawaoni ni kwa jinsi gani kiwango cha maambukizi kinaweza kushuka hadi katika ngazi ya kudhibitiwa haraka na kisha shughuli kurudia kawaida.
Kwa sasa, wanasema, ni mchezo wa kusubiriana na haijulikani subiria hiyo itaendelea hadi lini, kwani miezi inakatika na itafika mahali haitawezekana tena, kwani kuna msimu ujao unaotakiwa pia kuandaliwa kwa ajili ya kuanza, achilia mbali masuala ya usajili. EPL watakutana tena Ijumaa ijayo kuona mambo yanakwendaje.