Menu
in , , ,

EPL na moto wake

Ligi Kuu ya England (EPL) imeanza na makali yake, ambapo moto
unaonekana kutoka kwa timu nne katika mizunguko miwili, tatu zikiwa na
moto wa wastani, tano zina moto mdogo, tano zinasuasua na tatu zipo
kwenye pointi sifuri kabisa.

Walioshinda mechi zote mbili ni Manchester City, Manchester United na
Chelsea lakini pia wamo ambao hawakutarajiwa na walilalamikiwa kwa
kutosajili licha ya kupanda daraja msimu huu, wakiwa pia na majeruhi
na kuuza mchezaji muhimu – hao ni Hull.

Wote hawa wanajivunia kazi nzuri kwa asilimia 100 hadi sasa,
ikimaanisha kwamba wameshinda mechi zote na hivyo wana pointi sita.
Kwamba huo ndio utakuwa mwelekeo wa muda mrefu si suala linaloweza
kusemwa sasa hivi, lakini Waswahili husema aheri ndege mmoja mkononi
kuliko sita mwituni.

Kujikusanyia pointi mapema ni jambo la muhimu sana kwa timu yoyote.
Everton, Middlesbrough na Tottenham Hotspur wanazo pointi nne kila
moja, ikimaanisha walishinda mechi moja na kutoshana nguvu nyingine
kila moja. Ni kazi nzuri hiyo hadi sasa.

Kundi jingine ni la wenye pointi tatu kila mmoja, ikimaanisha
wameshinda mechi moja na kufungwa moja; Burnley, West Bromwich Albion,
Liverpool na Swansea. Hawa kazi yao hadi sasa imefanyika kwa asilimia
50. Ndio hawa wanaokaa karibu na katikati ya msimamo wa ligi.

Kundi linalofuata ni la wanaosuasua; wameanza ndivyo sivyo na baadhi
wanaweza kujilaumu wenyewe kwa kushindwa kwao kufanya usajili mzuri,
kubweteka na mafanikio ya nyuma au kutojipanga sawa tu.

Hawa wana kapointi kamoja tu kutokana na michezo miwili nao ni
Arsenal, Watford, Leiceter, Southampton na Stoke. Ingekuwa ligi
inamalizika leo basi tungekuwa na washuka daraja watatu walio hoi
kwenye pointi sifuri kama wafanyakazi au wanafunzi hewa. Hawa ni
walionusurika kushuka msimu uliopita – Sunderland, waliokuwa wazuri
kiasi – Crystal Palace na wanaofundishwa na kocha kijana zaidi
England, Eddie Howe, yaani Sunderland.

Joe Hart
Joe Hart

Mchezaji na nahodha wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira amemchana
kocha Arsene Wenger akisema kwamba Arsenal wamekuwa walaini mno na
hivyo kuwapa ugumu kupambana na timu nyingine kuwania ubingwa wa
England.

Arsenal wameonekana kupwaya mbele na kwenye ulinzi kadhalika, maeneo
ambayo Wenger anajua kwamba wanahitaji kuongeza wachezaji, ila anadai
kwamba hajapata mtu na kuwa angekuwa tayari kutumia hata pauni milioni
300 lakini si kununua ili mradi tu aonekane kwamba anasajili.

Vieira pia amemnanga Mfaransa mwenzake huyo kwa kutowapa wachezaji wa
zamani wa Arsenal nafasi ya ukocha hapo. Hata hivyo, Vieira amekuwa na
kundi la kampuni za Manchester City wakati Thierry Henry aliondoka
Emirates baada ya Wenger kumtaka awepo hapo muda wote ikimaanisha
aachane na kazi ya uchambuzi wa soka kwenye televisheni. Nahodha wa
zamani wa Arsenal, Mikel Arteta naye aliruhusiwa kuondoka mwishoni mwa
msimu na sasa ni kocha msaidizi wa Manchester City.

Man City wanaofundishwa na Pep Guardiola wanaoneana kufanya vyema na
kocha huyo amekuwa akiwamwagia sifa vijana wake kwa jinsi
wanavyocheza, kushambulia na kufunga mabao mengi.

United nao wapo vizuri chini ya Jose Mourinho na wachezaji wao wapya,
Paul Pogba aliyevunja rekodi ya dunia kwa usajili na Zlatan
Ibrahimovic anayeongoza mashambulizi hapo Old Trafford.

Chelsea wa Antonio Conte wapo vizuri japokuwa inaonekana bado kujenga
kikosi sawa na ushindi wao umekuwa si mkubwa wala wa kutabirika, huku
mshambuliaji wao, Diego Costa akionekana kuendelea na tabia mbovu
uwanjani huku akinusurika kadi nyekundu kwenye mechi zote mbili naye
akilalamika kwamba anawindwa na wachezaji wapinzani na waamuzi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version