Menu
in , , ,

EPL, Liverpool, kuhusu kipaji cha Federico Chiesa

Tanzania Sports

NDANI ya mechi nne tu tangu alipokabidhiwa kibarua ya kuifundisha Manchester United, Ruben Amorim aligundua kitu tofauti na alikotoka. Amorim anatokea Ligi Kuu Ureno, ambako alikuwa kocha wa Sporting Lisbon. Kwa wareno neno Lisbon wanaliita “Lisboa”, ila Lisbon ni kwa lugha ya kiingereza. Katika mechi hizo Ruben Amorim alisema Ligi England imeundwa katika matumizi makubwa ya nguvu huku ufundi likiwa jambo la pili tofauti na anakotoka, ama ligi zingine kama Ureno na Hispania. Amorim alifichua kuwa matumizi ya nguvu yamechukua nafasi ambayo inawafanya wachezaji wawe wanahangaika sana kwenye masuala ya utimamu wa miili ili kuendana na hali ya EPL. 

Maoni ya Amorim sio mapya lakini yanaonesha jinsi ligi ya EPL ilivyo. Uchezaji wake umetawaliwa na nguvu nyingi sana, angalia Arsenal ya msimu uliopita ilicheza kandanda safi na kuburudisha mashabiki duniani, lakini walikuwa wanasemwa hawana nguvu nyingi. Msimu wa 2024/2025  Arsenal wana matumizi makubwa ya nguvu kuliko msimu uliopita. Mechi yao dhidi ya Chelsea wikiendi iliyopita ilionesha namna ambavyo wamepambana hadi kukabiliana na mabavu ya EPL. Katika mazingira hayo Amorim amenikumbusha namna kipaji cha Federico Chiesa kinavyoozea benchi pale Liverpool.

Kwanini Federico Chiesa?

Huyu ni winga mzuri sana kwa upande wa kulia au kushoto. Pia anaweza kucheza kama mshambuliaji wa pili yaani nambari 10. Federico Chiesa aliwasili Liverpool akiwa staa wa mpira, ingawaje alikuwa majeraha kidogo. Hata hivyo licha ya kupona hakupata nafasi nyingi za kucheza. Ikaonekana kama vile Federico Chiesa amepoteza mwelekeo. Kila ukifikiria Chiesa yule aliyekuwa wakizichachafya timu za Ligi Kuu Italia kisha angalia hali yake ya sasa, unabaki kushangaa. 

Chiesa ni mchezaji ambaye anakupa vitu vitatu vya msingi; kasi, uwezo w akupangua ngome ya wapinzani na kupachika mabao. Uchezaji wake ndiyo uliwavutia Liverpool hadi kumkabidhi jezi namba 14 mgongoni. Chiesa ni wale mawinga wanaopenda kucheza kama Luis Figo. Chiesa anaupenda mpira, anauchezea kadiri anavyojisikia. Kuna uhusiano mkubwa kati ya mpira na miguu ya Chiesa. 

Kuna uhusiano mkubwa kati ya usongo na ari ya Chiesa na miguu ya Chiesa katika kutafuta matokeo cha mchezo. Kuna uhusiano mkubwa kati ya maarifa ya Chiesa na miguu yake yote miwili. Uzuri moyo na mapafu yake vyote vinamtii, hakuna kiungo ambacho kinaweza kumsaliti, mbali ya majaliwa na Muumba. 

Katika mashindano ya Euro Federico Chiesa alikuwa wakitandaza soka maridadi. Alitawala winga za Italia na kuwapa furaha mashabiki wake. mbele ya wachezaji wenye viwango vikubwa, Chiesa alikuwa akipambana na mabeki bora barani Ulaya na akaandika jina lake.

Dakika 15 za Chiesa  kwenye Wembley

Kwenye kikosi cha Liverpool hasa safu ya ushambuliaji, kocha Arne Slot anampanga Diogo Jota kama mshambuliaji anayeshikiriana na Luis Diaz na Moahmmed Salah. Nimeitazama fainali ya Kombe la Carabao jinis Liverpool ilivyokuwa ikicheza dhidi ya Newcastle United, ilionesha wazi walikosa mtu aina ya Federico Chiesa. Safu ya ushambuliaji ilikuwa na wabunifu wawili, Luis Diaz na Mohammed Salah, kisha nambari 9 alipangwa Diogo Jota. 

Kama unaangalia maarifa, basi Liverpool walihataji maarifa ya Federico Chiesa mapema sana. kwa muda wa dakika 15 alizopewa kwenye mchezo wao dhidi ya Newcastle United unaona bayana anautaka mpira, anaucheza, ana uchu nao, anapanga na kupangua safu ya ulinzi. Alipangwa kucheza eneo la kushoto hasa kwenye kona ya 18 (kushoto) ambako alitakiwa kuanzia hapo kuingia dimbani. Muda aliokuwa nao Federico Chiesa haukutosha, kwani mwingi aliutumia Diogo Jota. 

Tanzania Sports
Federico Chiesa

Lakini Federico Chiesa aliwaita wachezaji wenzake, akawapa ari, akawaongezea hamu ya kusaka bao. Alimkimbiza zaidi Kieran Trippier ule upande wa kulia, na kumfanya arudi nyuma zaidi. Kwa kawaida Newcastle United wanapenda kucheza mpira wa kibabe, wanapenda vurugu zisizoumiza na zaidi wanacheza kwa kuvuruga wapinzani kwa buatua butua zao. Lakini kwa vile Liverpool walikosa mchezaji mbadala wa kupangua safu ya ulinzi ya Newcastle wakajikuta mipango yao yote inaishia kwenye 18 za wapinzani wao. Haikuwa kwa Mo Salah wala Diaz. Lakini ingizo la Federico Chiesa liliwapa uhai. Liverpool waliamka, wakainuliwa na Chiesa hata kabla hajapachika bao. Ingizo la Federico Chiesa na jinsi alivyoonesha hamasa iliwaamsha mastaa wa Liverpool na kujaribu kusaka mabao. 

Hakuwa peke yake, bali alisaidiwa na Curtis Jones kiungo mgumo wa kiingereza. Chiesa alitandaza mpira, alicheza kwa kasi, akawakimbiza na kuwapangua mabeki wa Newcastle. Shangwe la mashabiki wa Liverpool liliamka vizuri na wakaamini kuwa watasawazisha mabao. Chiesa akawapa nafasi katika imani yao pale alipofanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na wenzake hadi alipopachika bao la kwanza la Liverpool. Ingawaje kulikuwa na matatizo ambayo yalidhaniwa mfungaji alikuwa ameotea, lakini VAR ikasema hapana. Federico Chiesa alifunga bao safi lililowaongezea ari Liverpool. 

Lakini wakati bao hilo likiingia wavuni mwa Newcastle muda ulikuwa umeyoyoma. Federico Chiesa hakuwa na miujiza tena ya kuongeza muda. Kwani ndani ya dakika 15 aliwapa Liverpool bao la matumaini. Wakati akili yake ikimtuma kuanza kulitafuta bao la pili ili ubao usomeke 2-2, muda ulikuwa umekwisha. 

Mashabiki wa Newcastle United wakawa wanalia kwa furaha wakati wale wa Liverpool walikuwa wanasikitika. Na yote hayo yalikuwa mikononi mwa Arne Slot. Ni dhahiri tunadanganya mashabiki wa soka wa EPL na dunia kwamba Federico Chiesa anastahili kukaa benchi na eti Diogo Jota anatakiwa kuanza kikosi cha kwanza. Labda kwa vile Jota ana uzoefu na EPL, lakini kiufundi hamfikii hara robo Federico Chiesa. Ni zao la mpira wa kiufundi toka mguuni mwake hadi kichwani. Federioco Chiesa anajua mpira jamani, anajua hadi basi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version