Kesho Jumamosi Chelsea walio kwenye nafasi ya 17 kwenye msimamo wa EPL watamenyana na Arsenal ndani ya dimba la Stamford Bridge kwenye mchezo wa mzunguko wa sita wa Ligi Kuu ya England msimu huu.
Itakumbukwa kocha wa Arsenal Arsene Wenger hakuwa amewahi kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Jose Mourinho kabla ya mchezo wa Ngao ya Jamii wa mwezi uliopita ambapo Arsenal waliibuka na ushidndi wa 1-0 dhidi ya Chelsea.
Nafikiri hili ni moja kati ya mambo yanayomfanya Mourinho sio tu kumuheshimu mpinzani wake bali pia kuwa kwenye presha ya kupitiliza kuelekea mchezo wa kesho. Mbaya zaidi Chelsea wakipoteza mchezo wa kesho watajikuta kwenye ukanda wa kushuka daraja iwapo yoyote kati ya Stoke City, Sunderland na Newcastle itashinda mchezo wake hapo kesho.
Hata hivyo pengine ushindi wa mabao manne kwa sifuri ambao Chelsea waliupata siku ya Jumatano kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Maccabi Tel-Aviv unampa nguvu na matumaini Jose Mourinho.
Kikosi cha kocha Arsene Wenger kilikutana na kipigo cha mabao mawili kwa moja dhidi ya Dinamo Zagreb siku ya Jumatano. Huenda hili linamfanya mwalimu Arsene Wenger pia kuwa kwenye presha.
Hata hivyo kocha huyo ameiongoza timu yake kushinda michezo yote miwili ambayo Arsenal imecheza ugenini kwenye EPL msimu huu. Hivyo nadhani ana matumaini ya kuiongoza Arsenal kuendeleza rekodi yake ya asilimia mia moja ya alama za mechi za ugenini kwenye dimba Stamford Bridge hapo kesho.
Kwa upande wa vikosi Chelsea kwenye mchezo wa kesho watawakosa golikipa Thibaut Courtois na kiungo Willian ambao ni majeruhi. Kuna wasiwasi pia huenda majeraha yatawafanya Oscar, Pedro na Falcao kushindwa kutumika kwenye mchezo wa hapo kesho.
Thomas Rosicky, Jack Wilshere na Danny Welbeck ni majeruhi wa upande wa Arsenal hivyo na wao pia hawatahusika na mchezo huo. Per Mertesacker huenda akarejea uwanjani baada ya kukosekana kwenye mchezo dhidi ya Dinamo Zagreb baada ya kupata ajali ya gari.
Tukitazama takwimu Chelsea mbaka sasa wamesharuhusu mabao 12 kwenye michezo mitano ya EPL na wamefunga mabao 7. Wastani wao wa idadi ya mashuti ni mashuti 15 kwa mchezo mmoja wakati wastani wa umiliki wa mpira ni asilimia 57. Kwenye wastani wa usahihi wa pasi wanazopiga kwa mchezo wana asilimia 83.
Arsenal wao wameruhusu mabao matatu tu mbaka sasa ambayo ni machache kuliko timu yoyote ukiwatoa Manchester City ambao bado hawajaruhusu bao na Manchester United walioruhusu matatu pia. Wastani wa idadi ya mashuti ya Arsenal ni mashuti 22 kwa mchezo mmoja.
Vijana hao wa Wenger wanaongoza kwa wastani wa umiliki wa mpira kwenye EPL wakiwa na asilimia 66. Wanaongoza pia kwenye wastani wa usahihi wa pasi ambapo wana asilimia 87.
Takwimu hizi huenda zinatoa onyo kwa Jose Mourinho na pengine zitamfanya adumishe mbinu zake za kupaki basi kwenye mchezo wa kesho. Hata hivyo kocha huyo hajawahi kupoteza michezo mitatu mfululizo kwenye michuano yoyote tangu alipoanza kazi ya ukocha. Kesho itakuwa ni kwa mara ya kwanza ikiwa atafungwa na Arsenal.
Hivyo Arsene Wenger pia anatakiwa kuwa makini kwa kuwa Mourinho ataelekeza nguvu zake zote mbaka za ziada kwenye mchezo huo ili rekodi yake hiyo isivunjike na kukiweka kibarua chake mashakani.