Hali ya soka ya England ni ngumu kutokana na kuibuka, kusambaa na kuathiri watu wengi virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
Kati ya waliokuwa wanapata kima kikubwa cha fedha kutokana na soka ni klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) pamoja na bodi inayosimamia ligi hiyo.
Licha ya kwamba wote wamepata hasara kutokana na janga la maradhi hayo, ukweli ni kwamba bado wana kiasi kikubwa cha fedha, wakati klabu za madaraja ya chini zina hali mbaya na baadhi zinaelekea kufilisika.
Ni kutokana na hali hiyo pamekuwapo miito kwa EPL kuzitazama kwa jicho la tatu klabu za chini na hata wachezaji wa kwenye ngazi hiyo ya juu walikuwa wakishauriwa kukubali kukatwa asilimia fulani ya mishahara yao mikubwa ili kufidia janga hili kubwa.
Na sasa kuna mjadala juu ya kubadili mfumo wa fedha wa klabu husika zilizozoea kutumia mamilioni ya pauni katika usajili, kulipa mishahara na matumizi mengine mbalimbali huku baadhi zikisigishana mabega kuonesha nani zaidi kifedha.
Hata kabla ya soka kutumbukia kwenye madhila haya ya COVID-19, watu wenye ushawishi mkubwa kwenye gemu walipata kujadili haja ya mapato ya kwenye klabu hizi kutumiwa kwa ushirika zaidi na usawa badala ya baadhi kufaidika sana na wengine kupwaya.
Klabu ndogo za kwenye madaraja ya chini na zile zisizo za kulipwa zimebaki katika hali kama ya uvuli wa mauti na hali ya janga hili inazidi kuzisindikiza katika kufilisika au kufa kabisa, hali ambayo haikubaliki na hivyo EPL wanatakiwa kuweka mkono wao kusaidia.
Ni kutokana na klabu hizo ndogo ndogo kwamba klabu kubwa za EPL huchota na kupata wachezaji wake mara nyingi, lakini pia kukua kwa klabu hizo ndogo ni faida kubwa kwa familia ya soka kwa ujumla.
EPL bado wanahangaika jinsi ya kuumaliza msimu wa soka wa 2019/2020 ili kuhakikisha hawapotezi fedha za kutokana na haki ya matangazo ya televisheni. Wanahaha kuona kwamba mamilioni ya pauni hayapotei, bodi inapata na klabu kadhalika.
Klabu kubwa zinachukua asilimia 93 ya mapato ya msimu kuanzia 2019-2022, ambayo ni £8.65bn kutokana na dili za televisheni, hivyo kwamba wanatumia kima kikubwa sana kulipa mishahara na kufuru kwenye usajili. Janga hili limewaangaza na kuwaonesha kwamba matumizi ya ufujaji hayawezi kuwa endelevu na wanaweza kuingia hasara na madeni makubwa.
Watu walinyanyua kope za macho yao pale Mwenyekiti wa EPL, Rick Parry aliposema hivi karibuni kwamba matumizi makubwa kupita kiasi ya fedha miongoni mwa EPL ni uovu na kwamba wanatakiwa wabadilike ili kuondoa kabisa uovu huo.
Hoja ya Parry ni muhimu kuzingatiwa, si kwa wakati wa janga hili tu bali kwa ujumla katika soka, kwa sababu hali hubadilika na mtu hawezi kujua kesho inakuja na nini ndani mwake. Kuna jumla ya klabu rasmi 72 katika ligi ya soka, lakini ni hizi 20 za EPL zinazovuna na kutafuna kiasi kikubwa cha fedha, jambo ambalo halikubaliki.