Ligi Kuu ya England (EPL) imeanza kwa kishindo, baadhi ya vigogo wakipigwa kwenye raundi ya kwanza isivyotarajiwa.
Mambo yalichacha kwa ‘The Only One’ Jose Mourinho na timu yake ya Tottenham Hotspur.
Raha zimeanza tena, siku 48 tu tangu kumalizika kwa msimu ulioshuhudia Liverpool wakitwaa ubingwa, lakini pia dirisha la usajili la majira haya ya joto halijachangamkiwa kutokana na ukata wa klabu uliosaabishwa na athari a virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
Wakati dirisha la usajili likibaki wazi hadi Oktoba 5, tayari wachezaji wapya kwenye klabu zao wameanza kutema cheche, huku wengine wakiwa bado wanajaribu kuzoea mazingira mapya.
Gabriel na Willian – wachezaji wapya wa Arsenal waling’ara kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Fulham, ambapo Washika Bunduki wa London waliibuka kwa ushindi wa 3-0 ugenini, jambo ambalo si kawaida kwao kwa misimu kadhaa kushinda mechi za mwanzo. James Rodriguez alianza vyema kwa Everton ambao ndio waliowachapa Spurs 1-0.
Vijana wa Mourinho walionekana ama kuchoka au kutokuwa na mpango kamili wa mechi, tofauti kabisa na walivyozoeleka, wakikosa makali kwenye karibu maeneo yote uwanjani.
West Bromwich Albion waliorejea EPL msimu huu walianzia mguu mbaya baada ya kuchakazwa na Leicester 3-0, kichapo kama hicho kikitolewa na Arsenal kwa Fulham waliopanda daraja msimu huu pia. Southampton nao waliangukia pua baada ya kucharazwa na Crustal Palace kwa 1-0.
Kwingineko mabingwa watetezi Liverpool waliwashinda Leeds kwa tabu 4-3 huku West Ham wakipoteza 0-2 mkononi mwa Newcastle.