Menu
in ,

EPL hawataki Ligi ya Mabingwa Ulaya

Wanahisa wa Ligi Kuu England walikutana hivi karibuni kujadili mpango mpya wa kuendesha mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya uliowasilishwa na Shirikisho la Soka barani humo. UEFA wanataka kupanua muundo wa mashindano hayo kutoka timu 32 hadi 36 kuania mwaka 2024 na kuendelea. Idadi ya mechi itaongezeka kwa asilimia 100 kutoka mechi 125 za sasa hadi 225 kwa muundo mpya.

Pia wanataka mechi hizo kuchezwa kila mwezi wakati Ligi za ndani zikiendelea. Klabu za EPL zimekataa mpango mpya wa UEFA kwa sababu wanahofia endapo utakubaliwa na kutekelezwa maana yake utashusha thamani ya Ligi Kuu za ndani ikiwemo Ligi Kuu Uingereza.

Katika kikao kilichofanyika kwa njia ya video maofisa watendaji 20 wa timu za Ligi Kuu England wameuchambua mpango wa UEFA kupanua muundo wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuongeza timu timu mwaka 2024, wamedai utapunguza thamani ya matangazo na mapato ya yaliyopo ya timu za Ligi Kuu.

Kwa nyongeza, wanahisa wa EPL waliambiwa endapo mpango wa UEFA utapitishwa maana yake hakutakuwa na nafasi ya mashindano mengine ya ndani kama Kombe la Carabao, ambalo thamani yake ni zaidi ya pauni milioni 100 kwa timu za Ligi Kuu Uingereza.

Tanzania Sports
Ligi ya Mabingwa Ulaya

Timu kama Arsenal inatarajiwa kunufaika na mpango mpya wa UEFA, pia timu zilizopata mafanikio katika mashindano ya Ulaya historia zao zitalindwa.

Chini ya muundo mpya wa UEFA, timu mbili kila msimu zitatoka Europa League na hatua za awali za nafasi za kufuzu Europa zitapelekwa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Utaratibu huo utatumika kote Ulaya, lakini ukweli ni kwamba utahusisha timu 400 zile zilizoko kwenye orodha ya ubora inayotolewa na UEFA.

Kwa EPL, hilo litakuwa na maana timu zinazomaliza Ligi Kuu zikwa nafasi ya tano,sita au saba zitaingizwa daraja la timu za juu chini ya orodha ya timu bora zenye viwango vya UEFA. Nafasi mbili za Ligi ya Mabingwa zitaamuliwa namna hiyo kuanzia mwaka 2024 chini ya mapendekezo mapya ya UEFA.

Tanzaniasports imefanya uchambuzi wa mapendekezo hayo kulingana na viwango vya timu mbalimbali vilivyotolewa na UEFA kwa misimu ya 2019-2020, 2018-2019 na 2017-2018. Kwa msingi huo timu zitakazonufaika na mapendekezo mapya ya Ligi ya Mabingwa Ulaya zitakuwa kama ifuatavyo;

Msimu wa 2019-2020; timu za Tottenham Hotspurs (ilimaliza nafasi ya sita RPL) na AS Roma (ilimaliza nafasi ya tano Ligi Kuu Italia).

Msimu wa 2018-2019; Timu ya Arsenal ilimaliza nafasi ya tano EPL, Sevilla ililazima nafasi ya sita La Liga.

Msimu 2017-2018; timu ya Arsenal ilimaliza nafasi ya sita EPL na Sevilla ilimaliza nafasi ya saba La Liga.

Uongozi wa EPL umepanga kuwataarifu wawakilishi wa Ligi mbalimbali za Ulaya,bodi ya wawakilishi kwa nafasi zao kuhakikisha wanapinga mapendekezo mapya ya UEFA.

Timu za Ligi Kuu barani Ulaya zinataka kuingia makubaliano na UEFA juu ya muundo wa mashindano, wakati mechi zikiwa zinacheza na namna nafasi za nyongeza zitakavyotekelezwa.

Mipango ya UEFA ni kuongeza thamani ya pauni bilioni 2.6 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na bila shaka yoyote ni kama kupambana na hatari ya kuanzishwa mashindano mengine ya European Super League.

Bodi ya UEFA inajaribu kusukuma mbele mabadiliko hayo kupanua Ligi ya Mabingwa na kuzifanya timu zitakazo shiriki kucheza mechi 10 katika hatua ya makundi kabla ya kwenda hatua ya mtoano, kwa kile kilichoitwa kutumia mtindo wa Uswisi.

Mabadiliko hayo yatamaanisha mechi za makundi zitachezwa mwezi januari na hivyo mashindano ya Ligi ya Mabingwa yachezwa kila mwezi ambao Ligi za ndani zitakuwa zinaendelea.

Inasemekana mapendekezo mapya yanatoa faida zaidi kwa vigogo vya soka baranimUlaya. Kwa kutumia vigezo vya UEFA ambavyo vinapanga viwango kutokana na mafanikio yake Ulaya, nafasi mbili za Ligi ya Mabingwa zinaachwa kwaajilia timu za viwango vya juu ambazo zimeshindwa kufuzu mashindano hayo.

Kivitendo hilo litamaanisha Arsenal,Tittenham,Manchester United au Chelsea zinaweza kubebwa na UEFA kutoka Europa League au hatua za awali za kufuzu makundi na kupelekwa Ligi ya Mabingwa hali ambayo itasababisha kuzitupa nje timu kama Leicester City au West Ham.

Aidha, hatua za kufuzu zitapelekwa kwa timu za Ligi ya Ufaransa, ambako timu iliyoshika nafasi ya nne ikiwa kwenye nafasi za juu ya viwango vya UEFA itafuzu moja kwa moja bila kukutana na timu yoyote kuamua mshindi.

Kwa mujibu wa viwango vya ubora vilivyotolewa na UEFA kwa msimu wa 2020-2021 hizo ndizo timu bora kwa sasa ; Bayern Munich, Barcelona, Juventus, Real Madrid, Atletico Madrid, Manchester City, PSG, Sevilla,Manchester United, Liverpool, Arsenal, Borussia Dortmund, Chelsea, Porto na Tottenham Hotspur.

Hii ina maana mshindi wa Ligi ya Uholanzi, ambaye mara nyingi ni Ajax itakuwa kwenye nafasi nyingi za kuwakilisha mashindano ya UEFA na kuzitekeleza baadhi ya timu.

Upo wasiwasi kuwa kupanuliwa kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa kutashusha thamani ya Ligi za ndani barani Ulaya kwa sababu mapato yanayotokana na matangazo yatakuwa makubwa zaidi hivyo kuwavutia wawekezaji zaidi. pia timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa huenda zikawa tajiri zaidi kuliko zingine zinazoshiriki Ligi ya ndani bila kufuzu mashindano hayo hivyo kuchangia mapato yao kuporomoka.

Majadiliano ya mapendekezo mapya yanahusisha vyama vya soka 55, Ligi Kuu za Ulaya na chama cha timu za soka. hata hivyo UEFA imepania kukamilisha mapendekezo hayo mapema kabla ya kufanikiwa mpango wa kuanzishwa kwa European Super League ambao unasimamiwa na Real Madrid.

Uamuzi wa mwisho utachukuliwa na Kamati Kuu ya UEFA ikiwemo wawakilishi wa vyama vya soka, klabu na umoja wa klabu za soka Ulaya. UEFA lilitegemea kuitisha mkutano wa Kamati Kuu wiki iliyopita kupitisha mapendekezo mapya, lakini limeshindwa hivyo kuchelewesha mipango yao.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version