Wala usizitaje penati! Timu ya England 1990 yakumbukia mechi iliyobadili kila kitu
Kwa washabiki wengi wa England wa umri fulani, fainali za Kombe la Dunia 1990 nchini Italia ndizo zilizokuwa za mafanikio makubwa kwao.
Na kwenye nusu fainali dhidi ya Ujerumani Magharibi, wakipoteza kwenye changamoto ya mikwaju ya penati, hakika ilikuwa mechi kubwa zaidi.
Shilton, Parker, Walker, Wright, Butcher, Pearce, Platt, Gascoigne, Waddle, Lineker, Beardsley. Hiyo ni orodha ya wachezaji 11 walioanza mechi hiyo, japokuwa hawakuwa na majina makubwa kivile wala watu waliokuwa na vipaji vikubwa sana (ukiacha Paul Gascoigne).
Golikipa Peter Shilton alikuwa na umri wa miaka 40, David Plat hakuwa amepata kucheza mechi za kimataifa za kiushindani kabla, Gascoigne alitakiwa kuwajibika na kwenye mechi ile hapakuwapo kiungo aliyeonekana, lakini bado timu ilirejesha heshima ya soka ya England kiasi cha kukaribia kuwashinda timu bora kabisa ya taifa duniani.
Kipi kiliwafanya vijana wale wa 1990 kuwa maalumu kiasi hicho, nan i yapi wamefanya katika maisha yao ya baadaye? England waliingia kwenye mashindano hayo wakiwa na matumaini madogo sana. Wiki moja kabla, nusura wapoteze mechi dhidi ya Tunisia kabla ya kuimaliza kwa 1-1.
Vyombo vya habari viliwashambulia wachezaji hao, nao wakawagombea kama kujibu mapigo. England walifuzu kuvuka hatua ya mtoano, lakini haikuwa rahisi – sare mbili (dhidi ya Jamhuri ya Ireland na Uholanzi) na ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Misri, na kwa ujumla mabao mawili tu kwa jumla.
Lineker alikuwa mmoja wa wafunggaji, dhidi ya Ireland. Kwenye fainali zilizotangulia za Kombe la Dunia, alishinda Kiatu cha Dhahabu na akaishia kuwa mfungaji bora wa England tena, safari hii akiwa na mabao manne.
“Lilikuwa Kombe la Dunia jingine zuri kwangu. Kwa namna nyingine ilitisha,” alisema.
Hata hivyo, kulikuwa na tatizo pia, kwa sababu Lineker alikuwa akisumbuliwa na ugongwa – matatizo ya tumbo kabla ya mechi dhidi ya England, lakini hakumwambia yeyote maana alikuwa amedhamiria kucheza.
Ilikuwa ni miaka 20 baadaye, kwenye mahojiano na BBC 5, pale alipoweka bayana juu ya kipi hasa kilitokea. Leo, akiwa nyumbani kwake London, anacheka juu ya hilo.
“Nilikuwa nagugumia kwa maumivu katika kipindi cha kwanza, nikafaulu kujizuia na kuendelea, wakati wa mapumziko nikaenda uani, nikawaza ‘sasa nitakuwa sawa’. Kwenye dakika ya 15 kipindi cha pili nikaanza tena kugugumia. Nikajaribu kumtoka beki wao wa kulia na nikifanya hivyo ikawa prrffff. Ikawa kila mahali, name niko najiuliza nifanyeje?” akasema.
Kwa hiyo alifanya nini? “Gary Stevens alikuwa amesimama karibu yangu name nikamwambia: ‘Gary, nimejichafua’. Nilikuwa kwenye nyasi nikijaribu kuondoa (kinyesi) kwenye bukta yangu. Ilitisha. Niliendelea kucheza kidogo. Nikapata fursa zaidi baada ya hapo. Hakuna aliyetaka kukabiliana name! kwa bahati mvua kubwa ilinyesha kwa hiyo ikawa rahisi kuosha mikono yangu uwanjani pale lakini bukta yangu ilikuwa hovyo. Baadaye niliitupa kwenye pipa la taka.”
Lineker anasema amekuwa na bahati. “Siamini katika miungu, lakini nyakati fulani hudhani kwamba sie ni sehemu ya PlayStation (mashine inayotumika kwa michezo kwenye televisheni) ya mtu kwenye sayari nyingine, na yeyote anayecheza anayenichezesha yupo vyema kwa sababu nimepewa maisha yenye Baraka.
“Nakumbuka nilipofunga bao la nne dhidi ya Hispania kwenye uwanja wa Bernabéu na nikawa ninakimbia kurudi kati ya uwanja, Bryan Robson akiwa kando yangu akikimbia name, nikasema: ‘Robbo, kwa nini nina bahati hivi?’ Akasema: “Ah, kwenda zako!”
Ilikuwa ni kama muda huo huo alipoacha kucheza soka: “Nilipata kitu kingine kwenye mchezo huo huo kilichoniridhisha sawa na kucheza.”
Je, alidhani kwamba angeenda kwenye vyombo vya habari? “Aah, ndiyo. Jina langu la utani kwenye fainali zile za Italia 1990 lilikuwa Junior Des [kwa ajili ya Des Lynam], kwa sababu nilitumia muda kukaa na wanahabari. Shuleni nilizoea kuandika ripoti za mechi baada ya kila mechi ya Leicester. Wakati wote nilijua kipi nilikuwa nataka.”
Kati ya wachezaji wote waliokuwa kwenye kikosi cha 1990, yeye, kwa mbali, ndiye aliyeonekana kuuwa mwenye mafanikio zaidi. Ndiye mtu anayelipwa zadi BBC, akivuna pauni milioni 1.35 mwaka 2021 na ana mali zinazokadiriwa kuwa na thamani ya pauni milioni 26.
Je, anawaza kwamba wachezaji wenzake wa zamani wanafurahia kwamba amefanya vyema kwa ajili yake kiasi hicho hadi sasa? “Utatakiwa uwaulize. Wanaweza kufikiria hivyo, au wanaweza kuwaza; ‘mwanaharamu ana bahati’.”
Kwenye mechi ya pili ya England kwenye mashindano hayo, dhidi ya Uholanzi, Kocha Bobby Robson alimwingiza Paul Parker kuchukua nafasi ya Stevens kwenye beki ya kulia. Parker alishangaa.
“Nilikuwa najiuliza; ‘nafanya nini hapa?’ Miaka mitatu iliyopita nilikuwa ligi daraja la tatu na Fulham na sasa naanza kuchea fainali za Kombe la Dunia.”
Ninapouliza juu ya nyakati alizokuwa juu katika maisha yake, anasema ni kule kuja kuwa baba, babu, kutwaa ubingwa na Manchester United na kufika kwenye nusu fainali.
“Inashangaza jinsi bado watu wengi wanazungumzia juu ya fainali hizo za Kombe la Dunia. Je, ni watu wangapi wanazungumzia juu ya nusu fainali za 2018? “ Ana hoja. England walifika kwenye nne bora miaka minne tu iliyopita – ikiwa ni mara ya pili tu tangu 1966, lakini tofauti na fainali zile aza 1990, hili linajadiliwa mara chache sana.
Parker alikuwa mmoja wa wachezaji watatu tu weusi kwenye kikosi cha wanasoka 22. Wengine ni beki mwenzake, Des Walker na winga John Barnes. Tangu wakati huo mengi yamebadilika; leo asilimia 43 ya wcahzaji wa Ligi Kuu ni weusi.
Tangu Juni 2020, wachezaji wengi wamekuwa na mtindo wa kupiga goti moja kama njia ya kuunga mkono usawa wa rangi. Hata hivyo, kadhalika kuna mambo ambayo hayajabadilika; ni asilimia nne tu ya makocha ni weusi na baada ya England kupoteza kwenye michuano ya Euro mwaka jana, wachezaji watatu weusi waliopiga penati walibaguliwa mtandaoni kutokana na rangi yao nyeusi.
Mwaka 1990, wachezaji weusi walicheza huku wakibaguliwa, Parker anasema. “Kuna watu wachache ambao hawakupenda hili, lakini walikuwa wachache kuliko wa leo hii.”