*Hispania safi, karamu za mabao zatawala
England wameendeleza vyema kampeni yao ya kufuzu kwa michuano ya Euro 2016 kwa kuwatandika Lithuania 4-0.
Nahodha wa England, Wayne Rooney wa Manchester United alifunga bao la kwanza na mikwaju mingine miwili ikagonga mwamba.
Mshambuliaji wa Arsenal, Danny Welbeck alifunga moja na jingine likatiwa kimiani, likiwa ni la sita katika mechi tano alizocheza za Euro.
Mshambuliaji wa Liverpool, Raheem Sterling alifunga bao lake la kwanza kwa England na sasa Three Lions wametanua pengo la pointi sita kileleni mwa Kundi E.
Kane aliingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya Rooney dakika ya 72 na hakuchukua muda akacheka na nyavu. Ilikuwa mechi ya kwanza kwa mshambuliaji huyu wa Tottenham Hotspur.
Kiungo wa Arsenal, Theo Walcott alipata fursa ya kuchezea taifa lake baada ya kuwa nje muda mrefu kutokana na majeraha, na aliingia badala ya Welbeck dakika ya 77.
Katika Kundi E England wana alama 15, Slovenia tisa sawa na Uswisi, huku Lithuani wakiwa na alama sita, Estonia nne na San Marino moja.
HISPANIA WAPATA USHINDI MUHIMU
Hispania wameondokana na mzimu wa kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe la Dunia kwa kuwafunga Ukraine 1-0 kwenye mechi ya Kundi C.
Alikuwa mshambuliaji wa Juventus, Alvaro Morata alitefunga bao, likiwa ni la kwanza kwake tangu Kocha Vicente del Bosque amwite kikosini.
Hispania sasa wanashika nafasi ya pili kwenye kundi lao, ambapo Slovakia wanaongoza na Ijumaa hii walipata ushindi wa 3-0 dhidi ya Luxembourg.
Katika kundi lao, Slovekia wana pointi 15, Hispania 12, Ukraine tisa, Belarus nne, Macedonia tatu na Luxembourg moja.
MATOKEO MENGINE KUFUZU EURO 2016
Katika mechi nyingine zilizochezwa Ijumaa hii kwa ajili ya kutafuta timu zitakazofuzu kwa mashindano haya makubwa zaidi Ulaya, Macedonia walilala nyumbani baada ya kupigwa 1-0 na Belarus.
Slovenia waliwatandika San Marino 6-0, Uswisi wakawafunga Estonia 3-0, Liechtenstein wakiwa nyumbani wakazabwa 5-0 na Austria.
Mechi nyingine ilishuhudia Moldova pia wakiwa nyumbani wakilimwa 2-0 na Sweden.
Jumamosi hii kutakuwapo mechi tisa, ambapo kali zaidi zinatarajiwa kuwa baina ya Uholanzi na Uturuki, Croatia na Norway na pia Bulgaria dhidi ya Italia.