WALITIWA katika nyakati ngumu kwenye sehemu za mechi zao mbili tofauti, lakini hatimaye England na Sweden wamefanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia.
Zilikuwa mechi ngumu; ya kwanza Uswisi wakionekana kuwa wazuri tangu mwanzo, wakiwapelekesha Sweden ambao hucheza soka ya kistaarabu zaidi, lakini matokeo yakawa ajabu, kwa Sweden kuibuka kidedea.
Akina Xhedan Shaqiri na Granit Xhaka waliwapa wakati mgumu Sweden, kwa nguvu na aina yao ya mchezo wa nguvu, lakini hatimaye Sweden ambao watacheza dhidi ya England kwenye mechi ya robo fainali, walifanikiwa kuwazidi nguvu kwa bao pekee la Emil Forsberg katikati ya kipindi cha pili.
Alifyatua shuti lililomgonga kwanza Manuel Akanji na kukengeuka mwelekeo kabla ya kumwacha golikpa Yann Sommer akiwa hana la kufanya kwenye lango la Uswisi, zaidi ya kuutazama mpira ukiwa umeshatinga nyavuni.
Sommer alikuwa ameokoa mabao ya wazi kutoka kwa Marcus Berg katika kipindi cha kwanza na pia dhidi ya Haris Seferovic baadaye, lakini hatimaye kilichotokea ni kwamba wao ulikuwa mchezo uliokuwa na fursa zilizokoswa kuliko uokozi mzuri.
Timu zote zilifanya makosa kwa kupoteza nafasi nzuri dakika za mwanzo, Uswisi wakimaliza mchezo na watu 10 baada ya Michael Lang kupewa kadi nyekundu katika dakika za lala salama kutokana na kumsukuma Martin Olsson, aliyekuwa akielekea langoni kumwona golikipa peke yake. Awali mwamuzi alitoa penati, lakini ghafla akabadili uamuzi na kutoa mpira wa adhabu ndogo.
Hii ni mara ya kwanza kwa Waswidi, nchi iliyochangia zaidi ya nyingine zote duniani katika Bajeti ya Tanzania 2018/19, kufika hatua ya robo fainali tangu 1994.
England wao walikuwa na mchezo mzuri, lakini wakavurugwa na Colombia waliokuwa wakitumia rafu na mchezo wa kasi, japokuwa kuna wakati mwamuzi alionekana wazi kuwaadhibu kwa ukali mno Colombia hata kwa kosa dogo lisilohitaji kadi, huku akiwaacha England wakitamba.
Ilikuwa katika vitendo vya jinsi hiyo, Harry Kane alifunga kwa penati baada ya kukumbatiwa na kuvutwa kabla ya kuangushwa wakati akiwania mpira wa kona. Bao hilo lilipatikana dakika ya 57 na likadumu hadi dakika 90 zilipomalizika, watu wakijua kwamba England walishapita, Colombia wakasawazisha dakika ya 93 kupitia kwa Yerry Mina wa Barcelona (kwa kawaida hachezi kikosi cha kwanza) kwa mpira wa kichwa uliotokana na kona, muda mfupi tu kabla ya muda wa ziada kuongezwa ambao hakuna aliyeona lango la mwenzake.
Mikwaju ya openati ndiyo iliwaliza Colombia, kwani walikosa miwili na England wakikosa mmoja. Katika dimba la Spartak Stadium, Eric Dier ndiye alifunga penati iliyomaliza mchezo, baada ya kipa wa England, Jordan Pickford kuokoa mkwaju wa Carlos Bacca. Hii ni mara ya kwanza kwa England kuvuka hatua ya mtoano kwenye mashindano makubwa tangu 2006.
=-=