Menu
in , , ,

England na mfumo mpya wa ligi

*Ligi mpya kuanzishwa kwa ajili ya wazawa

Chama cha Soka (FA) nchini England kimebuni mpango wa kukuza soka kwa wazawa ili kuijenga timu ya taifa ambapo kinafikiria uanzishwaji wa ligi mpya kwa chipukizi wazawa tu.

Moja ya mapendekezo ni kuanzishwa ligi itakayoshirikisha vikosi ‘B’ vya timu za soka zilizo Ligi Kuu ya England (EPL) na Ligi Daraja la Kwanza, maarufu kama Championship.

Hayo ni mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Mwenyekiti wa FA, Greg Dyke katika jitihada za kukuza soka na kuisaidia timu ya taifa kuwa na wachezaji wazuri na kufanya vyema.

Mpango huu endelevu unatarajiwa kuanza kutoa matunda ndani ya muongo mmoja, ambapo wanaangalia pia uwezekano wa timu husika kucheza katika ligi itakayochezwa baina ya ‘League Two’ na ile inayojulikana kama ‘Conference’ kuunda ligi mbili tofauti katika eneo moja.

Klabu za Ligi Kuu (EPL) na Ligi ya Soka (FL) zinaelezwa kupendezwa zaidi na wazo la timu ‘B’ kuanzishiwa ligi yao, ambapo watakaocheza humo ni wanasoka wazawa tu lakini kuna wasiwasi wa jinsi itakavyopatiwa nafasi ili isiingiliane na ligi na mashindano mengine.

Bado kuna utata juu ya hadhi ya timu ‘B’ hizo, iwapo zikifanya vibaya mwisho wa msimu zitashushwa daraja au vipi na zitaweza vipi kupandishwa daraja zinapofanya vizuri, maana timu zao ‘A’ ndizo zipo EPL na FL sasa. Inaulizwa iwapo ligi hiyo itaanza itamaanisha timu za ‘League Two’ zote zitaporomoshwa hadi Conference kwa ajili ya kupisha timu ‘B’ kuanza ligi hiyo.

Licha ya wasiwasi huo, inaelezwa kwamba zaidi ya hojaji 300 zilizofanywa kwa klabu na wadau wengine, zikiongozwa na Mshauri Mwelekezi Peter Beverly, zimeonesha inakubalika yafanywe mabadiliko makubwa ili kuhakikisha timu za pili za klabu kubwa pamoja na chipukizi wa England wenye vipaji wanapata fursa zaidi za kucheza soka na kuonesha ushindani.

Wajumbe wa tume wanasema klabu za Hispania, Ufaransa na Ujerumani huchezesha vikosi vyao vya timu ‘B’ kwenye ligi za ushindani na kwamba kufanya hivyo kunadhaniwa ndiko kunasababisha vipaji vya kutoka huko kukuzwa.

Dyke anatarajiwa kuanzisha mjadala juu ya mfumo mpya wa soka na suala la mwelekeo wa soka ya taifa kabla ya Kombe la Dunia linaloanza Brazil Juni 12 mwaka huu. Mjadala huo utasaidia kufutilia mbali malalamiko yoyote hata kama timu ya taifa ya England inayonolewa na Roy Hodgson itafanya vibaya.

Hata hivyo, baadhi ya maofisa waandamizi ndani ya FA wanamtaka Dyke kutulia hadi mashindano hayo yaishe na pia tofauti zilizopo katika mapendekezo ya mfumo mpya wa soka zimalizwe.

Pamekuwa na malalamiko kwamba wachezaji wa England hawapati nafasi za kutosha kucheza soka ya ushindani kwenye klabu za ligi kuu, jambo linalodhaniwa linachangia kufanya vibaya kwa timu ya taifa ambayo kwa miaka mingi sasa haijavuka hatua ya robo fainali ya mashindano makubwa.

Ujerumani, Italia na Hispania zimekuwa na vikosi imara vya timu za taifa zinazoundwa na wazawa wengi wanaocheza soka ndani ya nchi zao, tofauti na EPL iliyotawaliwa na wachezaji wa kigeni. Timu ya taifa ya England inaundwa na wachezaji wanaocheza soka ndani ya nchi.

51.577725-0.124481

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version