*Afyeka nyota 13 wa zamani
Kocha mpya wa Timu ya Soka ya Brazil, Dunga, ameanza kazi kwa kutema wachezaji kadhaa na kuchagua wengine kwa ajili ya mechi za kirafiki dhidi ya Colombia na Ecuador, akiweka msingi mpya wa kazi yake.
Dunga aliyechukua nafasi iliyoachwa na kocha aliyeachia ngazi, Luiz Felipe Scolari, amemwacha kipa wa siku nyingi, Julio Cesar, lakini pia beki wa kulia wa Barcelona, Dani Alves; Marcelo wa Reakl Madrid na Paulinho wa Tottenham Hotspur.
Makipa aliowaita ni Jefferson wa Botafogo na Rafael wa Napoli. Mabeki na majina ya timu zao kwenye mabano ni Maicon (AS Roma), Filipe Luis (Chelsea), Alex Sandro (Porto), Danilo (Porto), David Luiz (Paris Saint-Germain), Marquinhos (Paris Saint-Germain), Gil (Corinthians) na Miranda wa Atletico Madrid.
Viungo ambao Dunga ataanza nao ni Fernandinho (Manchester City), Luiz Gustavo (VfL Wolfsburg), Elias (Corinthians), Ramires (Chelsea), Everton Ribeiro (Cruzeiro), Ricardo Goulart (Cruzeiro), Oscar (Chelsea), Willian (Chelsea) na Philippe Coutinho wa Liverpool.
Kwenye safu ya ushambuliaji watakuwapo Hulk wa Zenit St Petersburg, Neymar wa Barcelona ambaye yupo fiti baada ya kuteguliwa vifundo vya mgongo kwenye mechi ya fainali za Kombe la Dunia na mshambuliaji mwingine ni Diego Tardelli kutoka Atletico Mineiro.
Coutinho ameitwa tena kwenye kikosi cha Brazil baada ya kuonesha mpira maridadi akiwa na Liverpool lakini nahodha Thiago Silva atakosa safari hii kutokana na kuwa majeruhi. Brazil walishika nafasi ya nne kwenye fainali za Kombe la Dunia, baada ya kuchapwa mabao saba na waliokuja kuwa mabingwa, Ujerumani.
Wakiwa wenyeji, raia wa Brazil ambao ni vichaa wa soka, waliona kwamba timu yao iliwaangusha na kocha akaamua mwenyewe kuachia ngazi, japokuwa kulikuwa na kila dalili kwamba angeondoshwa. Hii ni mara ya pili kwa Dunga kushika nafasi hiyo, ambapo amepata kuichezea timu hiyo ya taifa na kutwaa mataji nayo.