Menu
in , , ,

Droo ya UEFA Inawapa City Nafasi ya Kuandika Historia

Tanzania Sports

Manchester City wamepangwa kukutana na Real Madrid katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye droo iliyochezeshwa mchana wa leo. Kwingineko Atletico Madrid watamenyana na Bayern Munich.

City walifuzu kucheza nusu fainali za michuano hiyo mikubwa zaidi barani Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya kuwaondosha matajiri wa Ufaransa PSG kwenye hatua ya robo fainali siku chache zilizopita.

Ni jambo zuri kwa Manchester City kuepushwa kukutana na Bayern Munich ambao ni moja kati ya timu tishio zaidi Ulaya kwa sasa. Wababe hao wa Ujerumani ndio wanaopewa nafasi kubwa zaidi ya kuibuka mabingwa.

Isingekuwa taarifa nzuri kwa vijana wa Manuel Pellegrini ikiwa wangepangwa kucheza na timu hiyo ya Pep Guardiola ambayo ndiyo iliyopachika mabao mengi zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu ikiweka wavuni mabao 28.

Ingawa matokeo yao ya karibuni dhidi ya Juventus na Benfica yanaweza kukufanya uwaone wa kawaida lakini Bayern wametimia kila idara kuanzia eneo la ulinzi, kiungo mbaka safu ya washambuliaji. Mbinu za Pep Guardiola zinawaongezea makali zaidi.

Pia Atletico Madrid wangekuwa wapinzani wagumu zaidi kwa Manchester City endapo wangepangwa kucheza nao. Hakuna timu iliyokuwa tayari kukutana na Atletico kwenye hatua ya nusu fainali kufuatia waliyoyaonesha dhidi ya Barcelona.

Ni timu ngumu zaidi Ulaya kwa sasa linapokuja swala la ulinzi. Wameruhusu mabao 16 pekee kwenye Ligi Kuu Ya Hispania mbaka sasa kwenye michezo 32 wakati Barcelona wameruhusu mabao 27 na Real Madrid mabao 29.

Kwenye Ligi ya Mabingwa pia vijana hao wa Diego Simeone wana rekodi ya kushangaza ya ulinzi. Wameruhusu mabao 5 pekee kwenye michezo yote 10. Hayo ni mabao machache kuliko timu yoyote hata zile zilizoishia kwenye hatua za makundi.

Ingewapa wakati mgumu sana Manchester City kufunga mabao ambayo yangeweza kuwatosha kutinga fainali ikiwa wangekutana na safu ya ulinzi inayoundwa na Diego Godin na wenzie wakisaidiwa na viungo mahiri wakabaji kama Augusto Fernandez.

Real Madrid ndio wapinzani rahisi zaidi kwa wawakilishi hao pekee wa Ligi Kuu ya England. Halitakuwa jambo la ajabu kwa kiwango chochote kile endapo Manchester City watawaondosha vijana hao wa Zinedine Zidane.

Ingawa nao Real Madrid wamepata wapinzani rahisi zaidi kwenye nusu fainali kati ya waliokuwemo lakini Manchester City ndio kipimo chao kikali zaidi mbaka sasa kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu kwenye hatua za mtoano.

Walipata wapinzani rahisi mno walipopangwa na Roma ya Italia kwenye hatua ya 16 bora. Wakakutana na wapinzani dhaifu pia walipopangwa na Wolfsburg ya Ujerumani kwenye hatua ya robo fainali.

Ingekuwa habari ya kushangaza kama Real Madrid wangeondolewa kwenye michuano na AS Roma kwenye hatua ya 16 bora. Pia ingewashangaza wengi endapo Real wangeshindwa kupindua matokeo dhidi ya Wolfsburg na kusonga mbele.

Lakini kwa upande wangu haitashangaza kuwaona wawakilishi hao wa Ligi Kuu ya England wanatinga fainali kwa mara ya kwanza kwenye historia kwa kuwaondosha Real Madrid.

Nicolas Otamendi na wenzie wanao ubora unaotosha kuzuia madhara ya safu ya ushambuliaji ya Real Madrid na pia Sergio Aguero na wenzake wanao uwezo wa kufunga mabao yatakayowatosha kutinga fainali.

Naamini kocha Manuel Pellegrini amefurahishwa na droo hii ya UEFA. Ni wazi kuwa imewapa nafasi ya kutinga fainali kwa mara ya kwanza na kuandika historia mpya. Tusubiri.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version