*Timu za England zatenganishwa Europa
Hatimaye timu nane zilizovuka hatua ya 16 bora Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) zimepangiwa wa kuchuana naye.
Kwa mara ya kwanza tangu 1996, hapatakuwapo timu ya England kati ya hizo nane bora, baada ya Arsenal na Manchester United kuzifuata Chelsea na Manchester City.
Katika droo hiyo, Barcelona kutoka Hispania wenye mchezaji bora wa dunia, Lionel Messi watakwaana na Paris Saint-Germain (PSG) wa Ufaransa wenye David Beckham.
Droo hiyo inajumuisha timu zinazotoka mataifa matano tofauti, kwa vile kuna nchi zilizofanikiwa kupeleka zaidi ya timu moja.
Ni timu zilizosheheni utajiri wa vipaji vya aina tofauti, wachezaji wazoefu na vijana, hivyo hapana shaka robo fainali zote zitavutia.
Malaga kutoka Hispania watakwaana na Borussia Dortmund wa Ujerumani wakati Real Madrid wanaotoka Hispania pia watacheza na Galatasaray kutoka Uturuki.
Wajerumani wengine, Bayern Munich wamepangwa dhidi ya Wataliano, Juventus, kibibi kizee cha Turin.
Ligi ya Europa
Baada ya kukosa tambo kwenye UCL, klabu tatu za England zimefanikiwa kuingia robo fainali ya Europa League, baada ya kupigana kufa na kupona kwenye mechi za marudiano.
Chelsea waliohenyeshwa na Steua Bucharest kutoka Romani majuzi, watapambana na Rubin Kazan wa Urusi.
Tottenham Hotspurs waliotangulia kuwafunga Inter Milan mabao 3-0 London na kukung’utwa 4-1 Italia, walipenya kwa faida ya bao la ugenini na sasa watakwaana na Basel wa Uswisi.
Katika droo pekee isiyohusisha timu za England, Fenerbahce wa Uturuki watakwaana na Wataliano Lazio wakati Benfica kutoka Ureno wataoneshana kazi na Newcastle United.
Droo hii inakuja huku ikiiweka Chelsea katika msongamano mkubwa wa mechi, kutokana na kushiriki mashindano mengi, huku ikitakiwa kurudiana na Manchester United kupata atakayefuzu Kombe la FA.
Rafa Benitez, kocha wa muda wa Chelsea, amedai anafurahisha na hali hiyo, kwani inamaanisha wanafanya vyema na wanasonga mbele.