*Dili la Costa bichi, Man U nao wamo
*Arsenal wakamilisha usajili wa kwanza
HARAKATI za kusaka wachezaji kwa usajili wa majira ya joto zimeanza lakini mchakato unaelekea kuwa mrefu.
Hata Diego Costa wa Atletico Madrid aliyedaiwa kwamba ameshasainiwa na Chelsea bado hajajua hatima yake, kwani klabu yake kwanza ilidai haikuwa na habari za yeye kwenda Chelsea.
Jumamosi hii wakuu wa Chelsea walieleza kusikitishwa kwao na mchakato wa usajili wake kusuasua, ambapo licha ya kupimwa afya yake Stamford Bridge na kurudi kwenye timu ya taifa, Atletico wamekaa kimya kana kwamba hakuna lolote walilojulishwa.
Chelsea wametimiza masharti ya kifungu cha mkataba wake, kwamba Costa (25) anaweza kusajiliwa kwa dau la pauni milioni 32 na kwamba mchezaji huyo ameshawajulisha Atletico juu ya Chelsea kumtaka na yeye kuridhia lakini wamekaa kimya. Arsenal walifikia matakwa ya kifungu cha kumsajili Luis Suarez msimu uliopita lakini Liverpool wakakataa kumtoa.
DROGBA KURUDI CHELSEA?
Tetesi zilizopo ni kwamba Chelsea wanataka kumsajili mpachika mabao wao wa zamani, Didier Drogba anayemaliza mkataba wake Galatasaray.
Kocha Jose Mourinho anaangalia uwezekano wa kumsajili Drogba (36) aliyewasaidia Chelsea kutwaa ubingwa wa Ulaya kabla ya kuondoka. Chelsea pia wanataka kumsajili mlinzi wa Atletico, Miranda.
MAN U WAMTAKA POGBA
Manchester United wanataka kumrejesha mchezaji wake wa zamani, Paul Pogba anayekipiga Juventus na ambaye hakupewa nafasi ya kung’ara chini ya Alex Ferguson.
Hata hivyo, Juventus wanadaiwa kutotaka kuuza mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umriw a miaka 21.
Kocha Louis van Gaal wa United anataka kuvamia Ujerumani na kusajili wachezaji watatu; Mats Hummels, Bastian Schweinsteiger naThomas Mueller.
ARSENAL NA USAJILI WA KWANZA, BALOTELLI
Wakati Arsenal wamekamilisha usajili wa mchezaji wao wa kwanza kwa msimu ujao, wanadaiwa sasa kuendelea na mchakato wa kuwapata Mario Balotelli wa AC Milan na Loic Remy wa Queen Park Rangers (QPR).
Inaelezwa kwamba AC Milan wanataka kuondokana na Balotelli, japokuwa anauzwa kwa dau kubwa la pauni milioni30 ili wanunue mchezaji mwingine mwenye nidhamu, na Arsenal wanaonekana ndio wenye kumhitaji katika kuboresha safu yao ya ushambuliaji.
Arsenal wamekamilisha usajili wa kinda la Kigiriki, Elias Chatzitheodoridis (17) baada ya kuwafurahisha makipa. Alikuwa akichezea klabu ya Mas Kallitheakos lakini pia alikuwa akifanya mazoezi na academia ya Arsenal iliyopo Ugiriki.