Menu
in , ,

Drogba: Kama si ubingwa nisingeondoka Chelsea

*Amshukuru Abramovich, Mourinho na wazazi

Mchezaji nyota wa Chelsea, Didier Yves Drogba Tébily anasema huu ni wakati mwafaka kuondoka Stamford Bridge baada ya kutwaa ubingwa wa Ulaya.
Nahodha huyo na mfungaji bora wa jumla wa timu ya taifa ya Ivory Coast, anasema iwapo Chelsea haingetwaa taji hilo kubwa zaidi Ulaya, hangefikia uamuzi wa kuondoka.
Mshambuliaji huyo wa kati anaondoka Chelsea kama bingwa, mkongwe na maarufu klabuni hapo na mfano wa kuigwa kwa mamilioni kwa jitihada alizotia kwenye soka na kutokata tamaa ya kusaka taji hilo la heshima.

“Kama hatungetwaa Kombe la Ubingwa wa Ulaya ningebaki, tumefukuzana na taji hili kwa miaka minane. Tulifikia mahali kule Moscow tukaliona na kulikaribia kabisa, lakini tukashindwa hata kuligusa.
“Hii ilikuwa changamoto kwa wale waliokuwa Moscow, tukadhamiria kurejea kwa nguvu hadi tulipate na tukafanya kila kitu kwa ajili hiyo. Imetugharimu kwneye ligi lakini bora tu.
“Jumamosi nilikuwa kwenye mchezo wangu wa mwisho na Chelsea na nimefurahia sana miaka yangu minane hapa. Kumaliza nikiwa juu na Kombe la Ubingwa wa Ulaya lilikuwa jambo bora kuliko yote.
“Kwa siku mbili za mwisho nilikuwa najisikia kuwa na umri wa miaka 40 badala ya 24! Kucheza fainali ukiwa na miaka 34, tena ucheze muda wa ziada na kufanikisha kile nilichofanya, najivunia.
“Kuchezea Chelsea ndicho kitu kizuri zaidi ambacho kingeweza kutokea maishani mwangu, si kama mchezaji tu, bali pia kama mwanadamu.
“Nimejipatia rafiki wengi hapa, jambo ambalo kwa kawaida huwa ni gumu sana kwenye soka, na watabaki rafiki zangu maishani kwa sababu tumeweka historia hapa,” Drogba anasema akifurahia kutimiza ndoto yake hiyo.
Kipi kinafuata baada ya hapa? Drogba ana haya ya kusema: “Mjadala wa kubaki hapa au la haukujikita juu ya pesa kama watu wanavyodai. Siku zote nimefurahia ninachokuwa nacho kibindoni na mikataba yangu na familia ina furaha pia.
“Si kwamba hawanitaki hapa. Tulikaa pamoja sote na bosi (Roman Abramovich), Ron Gourlay (mtendaji mkuu) na kila mmoja kwenye bodi aliheshimu uamuzi wangu. Najua nilichowafanyia nao wanajua walichonifanyia.
“Nitajipa muda kwa ajili ya kufanya uamuzi sahihi. Mie na mke wangu tutakwenda kupumzika kidogo, japokuwa kuna michezo ya timu ya taifa. Sitachezea timu nyingine ya Uingereza.
“Naiheshimu sana na utii wangu upo kwa Chelsea damu yangu ni ya bluu, kwa kweli nitawakosa sana washabiki lakini daima watakuwa moyoni mwangu.”
Imekuwa inadaiwa kwamba huenda Drogba akaungana na mchezaji mwenzake wa zamani wa Chelsea, Nicolas Anelka katika klabu ya Shanghai Shenhua ya China.
“Ni dhahiri nimecheza naye (Anelka) kwa miaka mingi. Ilikuwa ngumu kuachana naye alipoondoka lakini hiyo ni sehemu ya soka na maisha. Anafurahia kule na anajitahidi vilivyo kuisaidia klabu. Lakini ukweli ni kwamba hakika nataka kuendelea kutafakari juu ya kilichotokea Jumamosi badala ya kuzungumza kuhusu China, Marekani na kwinginepo.
“Tangu nikiwa mtoto niliota kuhusu nyakati kama hizi, mazingira yalikuwa safi kabisa. Ni kama filamu vile.
“Mpaka leo nataka bado kuwa Munich kwenye uwanja ule wa mpira, nikishangilia na kusherehekea na washabiki. Ilipita mno haraka mara ya kwanza. ningependa ichukue muda mrefu zaidi.
Licha ya ushindi wa Jumamosi, Drogba anataja nyakati nyingine mbili za furaha: “Kutwaa taji la kwanza na Bolton (mwaka 2005) na goli bora zaidi lilikuwa kwenye Kombe la FA dhidi ya Manchester United (mwaka 2007), lile la kwanza kwenye uwanja mpya wa Wembley, nikilifunga katika muda wa ziada.”

Anajivunia kile anachokiacha, akisema: “Siwezi kusema sisi ndio tumeileta Chelsea, bali tumeleta zama mpya. Kwa kweli tumejenga kitu imara sana kiutambulisho.
“Sasa tunakwenda popote duniani na kila mtu anajua kuhusu Chelsea. Nenda Afrika, watu wanaizungumzia Chelsea. Naona watoto wanavaa fulana za Chelsea mitaani…india na kila mahali chapa inayotamba ni ya Chelsea.”
Chelsea inaweza kujiimarisha kwenye msingi wa ushindi dhidi ya Bayern Munich. “Bila shaka matarajio ya washabiki na mmiliki mwenyewe ni sambamba na kile tulichofanya Jumamosi.
“Sasa tumeshaweka kigezo ambacho akija mtu Chelsea, lazima akione kama kitu cha msingi cha kujaribu kufanikiwa, ni kuhakikisha unapata nafasi kufika kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya au kutwaa taji lenyewe.
“Hilo ndilo klabu inalotakiwa kufanya kwa kuwa kama Barcelona, AC Milan au Real Madrid barani Ulaya. Tuna kombe moja tu la Ubingwa wa Ulaya, na tunahitaji zaidi,” anajenga hali ya uendelevu wa kutaka mafanikio michezoni.
Je, Falcao wa Atlético Madrid ataweza kuvaa viatu vyake Chelsea?
“Najua ni mchezaji mzuri sana lakini hilo si langu kuamua. Kitu pekee ninachojua ni kwamba tayari tunao washambuliaji wazuri sana. Kila mtu anajua
Fernando (Torres) kuwa ni mchezaji mzuri. “Amekuwa na nyakati ngumu hapa na hii hutokea kwa kila mtu. Misimu yangu michache ya mwanzo ilikuwa migumu.
“Kitu kizuri ni kwamba tunamuunga mkono. Najua msimu ujao atafanya vizuri zaidi. Chelsea ipo katika mikono salama kwa kuwa na Fernando. Ni wazi tutahitaji washambuliaji wapya, lakini Torres ataifanya kazi,” anamsifu.
Katika kufanya maagano yake, Drogba anatoa shukurani:
“Hakuna kati ya haya ambalo lingewezekana bila bosi mkubwa, Roman Abramovich. Kwa hiyo njia bora zaidi ya kumlipa ni kushinda Kombe la Ubingwa wa Ulaya.
“Bosi alijitolea sana kwa ajili ya klabu hii. Kila mtu anazungumzia kuhusu kununua wachezaji ghali, lakini hakuna anayezungumzia kituo na vifaa vilivyopo Cobham, moja ya miundombinu bora zaidi duniani, na uboreshaji wa kituo cha michezo.
“Alisema anaelewa hisia zangu, akaheshimu chaguo langu nami nikamwambia ningebaki mchezaji wa Chelsea milele. Ni mtu mzuri sana.
“Alitoa kila kitu kwa familia yangu, akaiwezesha kupata fursa ya kufurahia maisha katika mitindo mikubwa ya aina yake. Kama mtakumbuka nilitoka Ivory Coast nikiwa sina vitu vyote hivi.
“Kombe hili la Ubingwa wa Ulaya ni kwa makocha wote waliopita hapa na ambao wamekuwa wakilifukuzia. Kila mtu anamjua aliyenipa nguvu na yule niliyejifunza mengi kwake ni Jose (Mourinho). Alinipa hii tabia ya kushinda, hamu ya kuweka historia. Yeye ni mshindi na tunayo kwenye DNA zetu sasa.
“Nazungumza kuhusu Jose kwa sababu alikuwa muhimu sana kwangu lakini aliyekuwa kocha kwa muda mfupi zaidi hapa ndiye ametwaa Kombe la Ubingwa wa Ulaya (Roberto Di Matteo).
“Huyu ni mtu maarufu kwa Chelsea, amefanya kazi kubwa sana ya kuweza kubadili mawazo na mwelekeo wa wachezaji, kwa sababu hatukuwa katika hali nzuri kifikra.”
Mambo hayakwenda vizuri chini ya Andre Villas-Boas. Drogba anamzungumziaje? “Andre ni rafiki. Ni ngumu. Inasikitisha kwamba ameondoka na hakutoa kwa Chelsea kile alichotaka kufanya hasa. Ikiwa timu haishindi ni rahisi kumnyooshea kocha kidole. Lakini ndani mwetu tunajua kwamba sisi ndio tunaowajibika.”
Hata hivyo, Drogba anatupilia mbali mawazo kwamba ‘wachezaji waandamizi’ wa Chelsea ndio wanaoiongoza klabu.
“Kocha anapokuja hapa, jua ameshakaa kitako na mmiliki, na bodi na wameshawekeana shabaha na malengo juu ya kile cha kufanikisha.
“Wasipofanya hivyo, wanatoa sababu kwa bosi kufanya kile anachotaka kufanya, lakini si mchezaji. Nisingependa wachezaji fulani kuwa na ushawishi juu ya kocha, si vizuri kwao,” anasema.
Di Matteo aliwarejeshea wachezaji hali ya kujiamini, na katika hili, Drogba anasema:
“Unaweza kumpanga mchezaji dimbani na kumpa hata michezo 30 lakini ikiwa hana ile hisia ya ushindi na kujiamini au mawasiliano si mazuri, hatakuwa na ufanisi.
“Robbie alizungumza nasi mmoja mmoja na pia kwa pamoja alipokabidhiwa ukocha, ndipo tukalazimika kufanya kila kitu kwa ajili ya kujiokoa kwenye msimu huu. Kila mtu alitakiwa kujitazama na kubadili tabia kwa ajili ya klabu.
“Robbie yumo katika mazingira kama yangu kwa sababu anakwenda kuzungumza na bodi na miliki na kuona kipi bora kwake na kwa klabu. Haijalishi kipi kitatokea sasa, ameweka historia.
“Iwe anabaki au anaondoka sasa, ni kwamba amezidi kuwa mkongwe na maarufu katika Chelsea. Kazi aliyoifanya ilikuwa kubwa na ya kipekee – kututoa kwenye msimu mbaya zaidi katika maisha yangu ya soka hadi kuwa mzuri kuliko yote.”
Drogba amekumbana na nyakati ngumu kama “tulipopoteza mchezo kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Liverpool kwenye msimu wa kwanza, goli la mzimu” mwaka 2005.
Anakiri kwamba kipindi kifupi cha kocha Luiz Felipe Scolari kati ya mwaka 2008 na 2009 “kulikuwa na nyakati chache kichwani mwangu nikiwaza itabidi niondoke.”
Drogba pia alijihisi vibaya juu ya mwamuzi wa Norway, Tom Henning Ovrebo baada ya ushindi tata wa Barcelona mwaka 2009.
“Ilikuwa ngumu kidogo kwake baada ya mchezo ule na ni soka tu. Wakati mwingine tunafungamanisha uzito mkubwa mno hapo kama nilivyofanya siku ile. Nilitaka kupata ushindi kwa nguvu hivyo kwamba mambo yalipokwenda vibaya, hisia zikaniteka,” anasema kwa masikitiko.
Drogba aliyezaliwa Machi 1978, amekuwa pia akikabiliwa na tuhuma za kujirusha ili apate penalti au mpira wa adhabu nyingine.
“Ninachohisi ni kwamba watu kwa kweli hawakufurahia Chelsea kuifunga Barca na walitarajia tushindwe mechi pale Nou Camp, ndiyo maana walikuwa wakijielekeza hivyo nilipoangushwa na kubaki pale chini.
“Tulistahili kushinda mechi ile, si kwa sababu tuliutawala mchezo – hatukuutawala – lakini hamu yetu ilikuwa nzito kuliko viwango vyao.
“Kidogo niliashangaa waliokuwa wanatukosoa, hata kama ni kweli nilijiangusha. Nilianguka baada ya kuguswa na mtu na kuna faulo zilifanywa lakini mwamuzi hakutoa adhabu,” anajitetea.
Anapoulizwa angependa kumuigiza kwenye filamu ya maisha yake, Drogba anajibu kwa utani: “Jupp Heynckes (kocha wa Bayern Munich) alisema mimi ni mwigizaji mzuri wa filamu, kwa hiyo labda mie!”
Drogba anaondoka Uingereza akiwa kweli mchezaji mwenye kuheshimiwa, kiasi cha kufikia kuomba kuubeba Mwenge wa Olimpiki katika maeneo ya Swindon, Kusini Magharibi mwa England.
“Sikitiko langu ni kwamba sitashiriki kwenye Olimpiki. Natamani ingewezekana Ivory Coast wakaja tukacheza na ingekuwa Wembley, nina uhakika tungeshinda!” anasema kwani amekuwa na kawaida ya ushindi kwenye uwanja huo.
Nyakati zote, Drogba amekuwa mnyenyekevu, akijaribu kuokoa maisha na kupunguza umasikini kwa mchango wake katika Umoja wa Mataifa.
“Nawashukuru wazazi wangu kwa jinsi walivyonifundisha na pia kwa rafiki zangu – rafiki zangu wa kweli. Hawanioni kama nyota,” anasema anapojiandaa kuondoka Uingereza kama bingwa wa Ulaya.
saria@tanznaiasports.com

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version