Jumapili hii nilikuwa uwanjani Emirates, nikashuhudia klabu ya Arsenal ikicheza hovyo kwenye michuano ya Kombe la Emirates.
Alikuwa ni mshambuliaji wa Ivory Coast anayekipiga Galatasaray ya Uturuki, Didier Drogba aliyepeleka majonzi Arsenal kwa timu yake kushinda mabao 2-1 na kutwaa kombe hilo.
Arsene Wenger ni wazi anatakiwa kukaza buti kupata wachezaji nyota, baada ya vipaumbele vyake, Gonzalo Higuain kufutika na Luis Suarez kubaki nusu nusu, kwa kuwa Liverpool hawataki kumwachia, na wakimtoa wanataka aende nje ya Uingereza.
Arsenal walianza vyema mechi ile na kuongoza kupata bao kupitia kwa mchezaji wa timu ya taifa ya England, Theo Walcott katika hali iliyoonekana ilikuwa bahati hivi.
Hata hivyo, ngoma ilielekea kuwa ngumu katika kipindi cha pili baada ya Waturuki kuwaingiza injini mbili kali, Wesley Sneijder na Drogba.
Kama ilivyotarajiwa, Drogba hakufanya mzaha, na alitumia uzembe wa mabeki wa Arsenal kuhakikisha anapachika bao, ambapo sasa katika mechi 16 dhidi ya klabu hiyo ya London Kaskazini, Drogba amefunga mabao 15.
Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa kiungo Mhispania, Santi Cazorla kucheza, na pia mchezaji mpya Yaya Sanogo alikuwa dimbani, lakini haikuwa siku yao.
Ama kwa hakika, Sanogo alipata nafasi ya wazi kuandika bao katika dakika za mwanzo kutokana na makosa ya Felipe Melo lakini hakuweaza kutumbukiza bao kimiani.
Walcott kama kawaida alicheza kwa ari, na nusura afunge bao la pili baada ya kuachiwa pande na Aaron Ramsey, lakini winga huyo alipiga nje.
Ramsey alicheza vyema, na inaelekea atakuwa mchezaji muhimu msimu ujao kama alivyokuwa mwishoni mwa msimu uliopita, na pengine Sanogo atang’ara.
Drogba alifunga bao katika dakika ya 76, kufuatia timu kujengeka vyema tangu kuingia kwa
Sneijder na Drogba. Ilikuwa penati iliyotokana na mchezo mbaya wa Ignasi Miquel anayetakiwa kuondoka Arsenal.
Drogber hakufanya makosa mbele ya kipa wa Poland, Wojciech Szczesny, na tangu hapo Sneijder na Drogba waliendelea kuitesa ngome ya Arsenal.
Beki wa kati Mjerumani, Per Mertesacker alikaribia kuirejeshea heshima timu yake, lakini alipiga kichwa juu ya mtambaa wa panya.
Galatasaray hatimaye waliibuka washindi, baada ya Drogba kutundika mpira kambani, kufuatia pasi ya Sneijder, dakika chache tu kabla ya mechi kumalizika.