*Chelsea waonesha jeuri ya fedha zaidi
*Berbatov aenda Monaco, Zaha Cardiff
*Fulham, Palace waleta wengi kujinusuru
Dirisha dogo la usajili limefungwa, ambapo klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) zimetumia kitita cha pauni milioni 130, ikiwa ni milioni 10 zaidi kuliko mwaka jana.
Usajili mkubwa zaidi pengine unaweza kusemwa umefanywa na Manchester United waliomsajili kiungo mchezeshaji wa Chelsea, Juan Mata kwa pauni milioni 37.1, Nemanja Matic wa Benfica ya Ureno kwa pauni milioni 21 na siku ya mwisho wakamnasa Kurt Zouma wa St Etienne kwa pauni milioni 12 lakini amerejeshwa huko kwa mkopo.
Kwa ujumla wake msimu wote, klabu kubwa za England zimetumia pauni milioni 760 zikichanganywa na usajili wa majira ya kiangazi.
Arsenal wameshindwa kupata mshambuliaji wa kati aliyedhaniwa anahitajika, lakini walau wamempata kiungo wa Sweden, Kim Kallstrom kutoka Spartac Moscow kwa mkopo hadi mwisho wa msimu.
Huyu atasaidia kuziba pengo kwenye sehemu ya kiungo ambamo Arsenal walikuwa na wachezaji wengi lakini ghafla wameishiwa, baada ya Aaron Ramsey kuumia na atakuwa nje kwa mwezi mmoja unusu, Mathieu Flamini kutumikia kifungo cha mechi tatu, Jack Wilshere pia ni hatihati huku winga Theo Walcott pia kuwa majeruhi mpaka mwisho wa msimu.
Siku ya mwisho ilitawaliwa na timu zilizo pabaya kwenye msimamo wa ligi kujaribu kusajili kuziba mapengo ambapo Fulham wameamua kufumua kabisa kikosi. Wamemwachia mshambuliaji wao Dimitar Berbatov kwenda Monaco na wakamsajili mshambuliaji wa kati wa Olympiakos, Konstantinos Mitroglou kwa pauni milioni 11.
Fulham pia wamemchukua pia kiungo wa Tottenham, Lewis Holtby kwa mkopo na mlinzi wa Everton, John Heitinga kama mchezaji huru na wachezaji wawili chipukizi wa Manchester United, Ryan Tunnicliffe na Larnell Cole kwa ada ambayo haikutajwa.
Crystal Palace nao walijitahidi kusajili wachezaji watano kwa sababu wanaelekea kuzama. Kwa hiyo wamewasajili winga wa Blackpool, Tom Ince kwa mkopo, kipa wa Wolves, Wayne Hennessey kwa pauni milioni tatu, pia wamemchukua kiungo wa Celtic, Joe Ledley na yule wa Southampton, Jason Puncheon, mlinzi wa Blackburn, Scott Dann.
Liverpool walitarajiwa kumsajili mshambuliaji wa Ukraine, Yevhen Konoplyanka kwa pauni milioni 15 lakini dili halikukamilika baada ya mmiliki wa Dnipro kushindwa kusaini nyaraka husika
Manchester City walitaka kusajili wachezaji wawili wa Porto ya Ureno, Eliaquim Mangala na Fernando lakini wakaachana nao kwa sababu klabu yao ilitaka zaidi ya pauni milioni 40 kuwaachia.
West Ham wanaochungulia kifo wamemsajili mlinzi wa Napoli, Pablo Armero kwa mkopo.
Sunderland wametoa pauni milioni tatu kumchukua kiungo wa Brighton, Liam Bridcutt.
Cardiff City wamempata kwa mkopo winga kinda wa Manchester United, Wilfried Zaha.
Yohan Cabaye wa Newcastle amekwenda Paris Saint Germain kwa pauni milioni 19.
Baadhi ya wachezaji wanatumika kuanzia leo kwenye mechi za EPL.