Kocha mtata Paolo Di Canio amekuwa wa kwanza kufukuzwa kazi miongoni mwa walimu 20 wa Ligi Kuu ya englans (EPL) msimu huu.
Di Canio (45) amefukuzwa kazi baada ya mechi tano tu za ligi hii, ambapo kwenye usajili alifanya mabadiliko kadhaa, wachezaji wengine wakiondoka naye akisajili wapya.
Katika mechi hizo tano, amepoteza nne kwa idadi kubwa ya magoli na kutoka sare moja. Alifungwa na Fulham, Arsenal, Crystal Palace, West Bromwich Albion na kutoka sare na Southampton.
Wadau wengi wa soka walishangazwa na uteuzi wake na hata kuchambua tabia, uwezo na mazingira ya kazi Uingereza.
Hata hivyo, alianza kazi yake vizuri kwa kuwaongoza Sunderland kuepuka kushuka daraja, japokuwa katika mechi za mwisho walifanya vibaya, ikabaki majaliwa tu kwa timu nyingine tatu kufanya vibaya zaidi yao.
Di Canio, mchezaji wa zamani wa Lazio, Juventus, Napoli, AC Milan na Cisco Roma za Italia na hapa Uingereza ametamba na Celtic, Sheffield Wednesdays, West Ham United na Charlton Athletic.
Katika vituko vya uwanjani na utovu wa nidhamu, Di Canio anakumbukwa kwa kumpiga mwamuzi, akamsukuma hadi kuanguka chini katika mechi dhidi ya Arsenal, baada ya kuoneshwa kadi nyekundu.
Alitozwa faini ya £10,000 mwaka huo wa 1998 baada ya kutiwa hatiani kwa kumsukuma badi kumwangusha mwamuzi Paul Alcock.
Di Canio amefukuzwa muda mfupi tu baada ya kutangaza mapinduzi makubwa, ambapo angebadilisha mfumo wa uchezaji huku akijaribu kutafuta uungwaji mkono kutoka kwa washabiki. Hata hivyo amefukuzwa kabla hatujaona mapinduzi yenyewe wala kujua yangekuwa vipi hasa.
Amewahi kukosana na wachezaji wake tangu msimu uliopita, akiwatuhumu mbele ya waandishi kwa ulevi na uchezaji kamari bila kuwasilikiza, na siku chache kabla ya kufukuzwa kazi alidai akili zao zina takataka.
Katika kuziba nafasi yake kwa muda, Sunderland imetangaza kwamba kocha Kevin Ball atasimamia kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Mwaka 2001 alipata tuzo ya kuonesha uanamichezo aliposhika mpira ili kusitisha mechi kumruhusu kipa wa Everton Paul Gerrard atibiwe.
Hata hivyo, mwaka 2005 alishambuliwa kwa maneno baada ya kutoa saluti ya kinazi wakati wa mechi ya Lazio.
Mwaka 2011 aliteuliwa kuwa kocha wa Swindon iliyokuwa katika League One nchini England, akadaiwa kutoa fedha zake ili wachezaji wasiondoke, kisha akajiuzulu akisema hakuelewana na uongozi.
Machi 2013 aliteuliwa kuchukua nafasi ya kocha
Martin O’Neill Sunderland ili aiepushe kushuka daraja.