MWANAMICHEZO na mfanyabiashara maarufu nchini, Azi m Dewji amekunwa na mafanikio ya timu ya Soka ya Taifa ya Zambia `Chipolopolo’, na jana alithibitisha furaha yake kwa kumpatia kila mchezaji wa timu hiyo kitita cha dola 500 za Kimarekani.
Kutokana na kiwango hicho cha fedha, Dewji amelazimika kutoka zaidi ya dola 13,000 (sh milioni 22.1 za Tanzania) kwa ajili ya wachezaji 23 na viongozi wa timu hiyo waliopo Gabon, moja ya nchi mbili zilizoandaa michuano hiyo mikubwa, yenye mvuto na utajiri mkubwa wa fedha miongoni mwa timu za taifa barani Afrika. Nyingine ni Ikweta ya Guinea.
Dewji, aliyeiwezesha Simba kucheza fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, alikabidhi kiasi hicho cha fedha kwa Rais wa Shirikisho la Soka Zambia (FAZ), Boniface Mwamelo katika ghafla fupi iliyofanyika jijini Lusaka, Zambia.
Akikabidhi, Dewji ambaye yuko nchini humo kwa shughuli za biashara, alisema ameguswa na mafanikio hayo yaliyorejesha heshima ya soka kwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika.
“Zambia ni majirani zetu, tunapakana nao. Lazima tujivunie mafanikio haya kwa sababu si ya Zambia peke yao, bali ya Ukanda huu wote,” alisema Dewji akiongeza kuwa, Zambia ni ndugu wa kweli na waliwahi kuwa wanachama wa CECAFA, Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati ambalo Tanzania ni miongoni mwa wanachama wake.
Pamoja na kuizawadia Zambia, alisema atakuwa tayari kufanya hivyo kwa timu yoyote itakayofanya vizuri, ikiwamo timu ya soka ya Tanzania `Taifa Stars’.
“Kama timu inatoka ukanda huu, sitabagua, nitawatuza kwa heshima wanayoileta. Hata Twiga Stars wamefanya vizuri hivi karibuni nimewazawadia, lakini si busara kutangaza kila kitu, hata kwa vitu vidogo…” alisema na kusema kwa kila hatua watakayopiga Zambia katika michuano ya mwaka huu, atawazawadia wachezaji.
Aidha, aliahidi kumwaga fedha zaidi kama wataifumua Ghana katika mchezo wa nusu fainali. Mchezo huo ulitarajiwa kufanyika jana usiku.
“Nitawapa fedha zaidi na pia nitawakumbuka kwa zawadi maalumu wajane wa wachezaji waliokufa katika ajali ya ndege Pwani ya Gabon mwaka 1993,” alisema Dewji, Mkurugenzi wa kampuni ya Simba Trailers inayounda bodi za magari makubwa, yakiwemo ya mizigo na ya abiria.
Zambia iliyopo Gabon chini ya nahodha Christopher Katongo, ilitua katika fainali za mwaka huu kwa kiapo cha kuwafuta machozi Wazambia ambao miaka 19 iliyopita walipoteza kikosi chote cha kwanza kilichokuwa gumzo wakati huo barani Afrika.
Rais wa sasa wa FAZ, Kalusha Bwalya alikuwemo katika kikosi, lakini alinusurika kwani alikuwa anatoka Ulaya alikokuwa akicheza soka ya kulipwa, akiamini angeungana na wenzake huko Dakar, Senegal ambako kikosi hicho kilikuwa kinakwenda kwa mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani.
Wachezaji waliokufa katika ajali hiyo ni Efford Chabala, John Soko, Whiteson Changwe, Robert Watiyakeni, Eston Mulenga, Derby Makinka, Moses Chikwalakwala, Wisdom Mumba Chansa, Kelvin “Malaza” Mutale, Timothy Mwitwa, Numba Mwila, Richard Mwanza, Samuel, Moses Masuwa, Kenan Simambe, Godfrey Kangwa, Winter Mumba na Patrick “Bomber”.