BAADA ya timu ya soka ya Simba kuing’oa ES Setif ya Algeria katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, mfanyabiashara maarufu na mfadhili wa zamani wa klabu hiyo yenye makao yake makuu Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Azim Dewji ametangaza kuwamwagia wachezaji kitita cha sh milioni 15.
Simba, `wataalamu’ wa michuano ya kimataifa wa Tanzania, wameingia raundi ya tatu ya michuano ya mwaka huu, licha ya usiku wa juzi kufungwa 3-1 ugenini Algeria, kwani tayari ilishatengeneza akiba nzuri ya mabao kutokana na ushindi wa 2-0 jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Dewji, akiwa mwenye furaha alitamka jana kuwa, anawazawadia wachezaji hao kutokana na ushujaa wa kupigana kiume hadi kufanikiwa kuing’oa timu hiyo ngumu kutoka Kaskazini mwa Afrika.
Alisema kuwa, alitoa hiyo katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam na kwamba anachokifanya sasa ni kutimiza ahadi.
“Kwanza niwashukuru wachezaji kwa kuwapa raha WanaSimba na Watanzania kwa ujumla, name nakamilisha furaha yangu kwa kuwapa sh milioni 15 nilizoahidi.
“Nitakabidhi mara mashujaa hawa watakaporejea nchini kutoka Algeria. Hakika wametupa heshima kubwa sana,” alisema.
Mwanamichezo huyo aliyeiongoza Simba kufika fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, pia kuiwezesha Tanzania Bara kutwaa ubingwa wa Chalenji huko Kenya akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kuisaidia Taifa Stars mwaka 1994, alisema atazidi kusaidia kadri timu itakavyoendelea kufanya vizuri.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi, wachezaji na wanachama kuongeza mshikamano ili kila timu itakayokumbana na Simba katika michuano ya mwaka huu iishie kuangua kilio.
“Siri ya mafanikio ni mshikamano. Baada ya Setif tujipange kwa vita iliyopo mbele, naamini kwa nguvu za pamoja tutafika,” alisisitiza mfanyabiashara huyo ambaye hivi karibuni aliwajaza pesa wachezaji wa timu ya Taifa ya Zambia `Chipolopolo’ baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika usiku wa Februari 12 huko Libreville, Gabon ilikoizamisha Ivory Coast kwa mabao 8-7.