Menu
in , , ,

David De Gea hatihati

*Schweinsteiger, Rojo nao kusubiri

Bado haijajulikana iwapo kipa namba moja wa Manchester United, David De Gea atabaki Old Trafford, hivyo ameachwa kwene orodha ya watakaokipiga kwenye mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya England (EPL) Jumamosi hii.

 

De Gea, 24, anayehusishwa na kuhamia Real Madrid ameachwa na kocha wake kwenye mechi dhidi ya Tottenham Hotspur, ikiwa pia ni baada ya kuonesha kiwango cha chini kwenye mechi za kujiandaa kwa msimu huu.

 

Inaelezwa kwamba De Gea mwenyewe anataka kuondoka lakini kocha Louis van Gaal amekuwa akijaribu kumzuia, ikiwa ni pamoja na kutaka iwapo ataondoka Madrid wampe beki wao wa kati, Sergio Ramos.

 

Van Gaal amedai kwamba uamuzi wake huo umetokana na ukweli kuwa huzingatia ubinadamu kuliko uchezaji na kwamba haamini De Gea anaweza kukabili mchezo huo.

 

Wakati bado haijulikani iwapo Ramos na De Gea watabadilishana klabu Van Gaal amesema kwamba kipa Anders Lindegaard, 31, au Sam Johnstone, 22 ndio watakaoanza mechi hiyo.

 

Wote walisafiri na United kwa ajili ya ziara nchini Marekani lakini hakuna hata mmoja aliyechezea klabu hiyo msimu uliopita.

 

Zipo habari za faraja kwa United, hata hivyo, kwamba Ramos bado hajakubali kusaini mkataba mpya na Madrid, japokuwa mwelekeo ulikuwa ame amemwaga wino.

 

United pia wanaye Victor Valdes, 33, aliyesajliwa kama mchezaji huru lakini kocha huyo anataka kumuuza kwa sababu alikataa kuchezea timu ya akiba.

 

De Gea aliyezaliwa Madrid amecheza mechi 175 tangu ajiunge na United kutoka Atletico Madrid 2011.

 

Katika hatua nyingine, winga wa United, Angel Di Maria ameandika barua ya wazi kwa washabiki wa United akiwaaga, kwani anatarajiwa kujiunga na Paris Saint-German (PSG) kwa kitita cha pauni milioni 44.3.

 

Di Maria, 27, raia wa Argentina amekiri kwenye barua hiyo kwamba msimu wake mmoja aliokaa Old Trafford haukuwa mzuri, lakini akasema kwamba hakwenda hapo kwa ajili ya majaribio.

 

“Nilijitahidi kwa kadiri nilivyoweza lakini soka si kama hisabati; mara nyingi mambo yaliyo nje ya uwezo wetu huathiri jinsi tunavyohisi na kufanya mambo.

 

Nasikitika kwamba mambo hayakwenda kama ambavyo ningependa kwenye klanu hii kubwa,” akasema Di Maria.

 

Kocha Van Gaal amenukuliwa akisema kwamba kundoka kwa Di Maria ni pigo kubwa kwa klabu yake, akiwa alinunuliwa kwa pauni karibu milioni 60.

 

Hata hivyo, amesema kwamba ingekuwa ngumu kwa Di Maria kumudu maisha ya EPL, akisema anataka washambuliaji zaidi wenye kasi na ubunifu kama alivyokuwa Di Maria.

 

“Alikuwa mmoja wa aina ya wachezaji hao lakini lazima wawe na kipaji cha kulandana na kasi ya England kitu ambacho ni kigumu.

 

“Hii ndiyo sababu baadhi ya wachezaji hawafanikiwi kwenye ligi hii – kasi ya mchezo na utamaduni wa soka ya England ni tofauti kabisa na kule Amerika,” akasema Van Gaal.

 

Hata hivyo, Di Maria alicheza vyema sana kwa muda aliokuwa Hispania akichezea Real Madrid hadi mwaka jana na pia alikuwa mzuri katika Timu ya Taifa ya Argentina iliyoshiriki michuano ya Kombe la Dunia.

 

Katika mechi ya Jumamosi hii, mchezaji mpya kutoka Bayern Munich, Bastian Schweinsteiger pia hatacheza kutokana na kile Van Gaal anachosema kwamba hana utimamu wa mwili.

 

Van Gaal alimlalamikia mchezaji huyo kwamba hakufanya vyema kwenye mechi za mwisho za ziara yao, lakini amesema atakuwa timamu baadaye, kwani alijiunga nao dakika za mwisho akitoka likizo.

 

Hata hivyo, kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola alitoa angalizo karibuni kwamba mchezaji huyo hajapata kuwa na utimamu kabisa wa mwili kwa miaka mitatu iliyopita.

 

Mlinzi kutoka Argentina, Marcos Rojo naye hatarajii kucheza kwa sababu kwanza hakujiunga na timu safarini Amerika lakini pia hajafanya mazoezi ya kutosha.

 

Alikosa safari hiyo kwa sababu alishindwa kuhuisha pasi yake ya kusafiria ndani ya muda.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version