Bila shaka ukijinasibu kuwa soka ndio mchezo unaopendwa sana duniani,utakubalika na kuungwa mkono kwa asilimia kubwa. Nchini Tanzania mchezo wa soka ndio unaopendwa zaidi na pia kumekuwapo taasisi zilizo rasmi na zisizo rasmi zinazosimamia mchezo huo wa soka.
Peter Manyika Senior ambaye amewahi kuchezea Klabu ya Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania ameonesha taswira nyingine kabisa na tofauti katika soka ya hapa nchini kwa kuamua kuwa na kituo cha magolikipa tu kwa kuwafundisha mbinu za ugolikipa kuanzia chini katika mizizi kwa elimu yake japo kidogo aliyoipata.
Ukiacha kituo hicho, pia Manyika amezingatia umri kwa wachezaji wake hao kwani amechukua vijana wachanga ambapo anawafundisha wachezaji wenye umri wa kuanzia miaka 6,10,16 na 23 ambapo anaamini kuwa ni wenye uwezo wa kushika mafunzo kwa wepesi.
Nimejiuliza maswali mengi binafsi kuhusu hili alilolifanya Manyika; je ni kwa sababu anapenda sana mchezo wa soka? Je, ni kipi kilichomsukama? Je, kwa nini ameamua kuangalia nafasi ya makipa tu?
Katika maongezi yangu na Manyika alisema kuwa ameamua kuangalia upande wa makipa kwa sababu Tanzania kuna tatizo kubwa la magolikipa na akatolea mfano kuwa matatizo ya magolikipa wa ligi daraja la nne ni sawa na wale wa ligi kuu kwa sababu wa daraja la nne watawaangalia wa ligi kuu na kufuata yale makosa yao na kuingia katika makosa yale yale.
“Unajua Tanzania kuna tatizo la magolikipa na tatizo kubwa sana ni golikipa wa ligi kuu matatizo yake ni sawa na yule wa ligi daraja la nne kwa sababu anayafuata ya yule wa ligi kuu pale anapomuona,” alibainisha.
Manyika akasema kuwa matatizo yaliyopo kwa magolikipa wa Tanzania ni kutoweza kulinda lango kwa dakika 90 au zaidi, kushindwa kupanga safu ya ulinzi, kucheza mipira ya kutoka pembeni na pia kutokuwa na mbinu za kuikabili misukosuko wakati lango likishambuliwa.
Aidha, kituo chake hicho kimeweza kuonesha matunda yake baada ya kumtoa mtoto wake Manyika Peter Jr. ambaye ambaye amepitia mikononi mwake akiwa na timu kubwa na kongwe ya Simba iliyopo ligi kuu Tanzania bara.
Jambo alilofanya Manyika linapaswa kuungwa mkono na wadau, kwani ni la kizalendo na ni la kuutakia mema mchezo wa soka nchini, lakini pia ni la kuinua soka kwa miaka ijayo hivyo iwe shime kwa kumuunga mkono Manyika.
Kwa mwanzo huo Manyika amesema amepata kuungwa mkono na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kupewa uwanja na vifaa vya mazoezi; vilevile wadau wengine wamekuwa wakijitokeza kwa kumpatia vifaa na hata ushauri na ametoa mwito kwa wafadhili, wadhamini na wadau zaidi kumuunga mkono ili kuinua soka ya Tanzania.
“Natoa mwito kwa wafadhili, wadhamini na wadau zaidi kuniunga mkono ili kuinua soka ya Tanzania,” alisema
Magolikipa zaidi ya 26, wakiwamo wale wa ligi kuu, ligi daraja la kwanza na la pili wapo katika kituo hicho na wale ambao hawana timu ambao baadae huwa wanapata timu za kuchezea kwani huwa wameiva vizuri kimazoezi.
Kituo hicho kinachoendesha mafunzo yake katika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam kimewezesha kumpeleka golikipa Juma Mpongo ligi kuu nchini Oman na pia yupo aliyekuwa golikipa wa Yanga Juma Kaseja na golikipa wa Twiga Stars, Fatma Omary.
Mwisho.