Mshambuliaji peke wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) anaecheza soka la kulipwa nchini Kuwait Dan Mrwanda hatoweza kuja hapa kuichezea timu hiyo kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu ya taifa ya Congo DRC
Mchezo huo utachezwa jumamosi hapa jijini Dar es salaam kwenye dimba la Taifa na timu ya Congo DRC inawasili leo jumatano jioni.
Katibu mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Fredrick Mwakalebela amesema wao waliandika barua kwa chama cha soka cha nchi hiyo kwenda kwenye timu anayochezea Mrwanda ili aweze kupata ruhusa ya kuja Tanzania kuichezea Taifa Stars ila hadi sasa bado hajapewa ruhusa hiyo
Pia Mwakalebela amesema pamoja na kukosa mchezo wa jumamosi dhidi ya DRC wao wanaendelea na mazungumzo ya kumtaka kuja hapa nchini kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya New Zeland utakaochezwa mwezi juni hapa nchini
Ili kuongeza muhimu wa mchezo huo TFF hivi sasa inataka pia kumshawishi yeye mwenyewe Mrwanda ili kuweza kuongeza changamoto kwa wakuu wa timu yake ili wamruhusu kuja kulitumikia Taifa lake
Mwisho kabisa Mwakalebela anasema wao wameandika barua kwa chama cha soka cha nchini Kuwait ili kuweza kumpata mshambuliaji huyo ila hadi sasa hawajapata majibu yeyote yale na wao bado wapo kimya hivyo hawajui nini kinaendelea
Kutokana na kumkosa Dan Mrwanda katika mchezo huo dhidi ya DRC kocha wa Taifa Stars Marcio Maximo atalazimika kuwatumia washambuliaji Jerry Tegete wa timu ya Yanga, Zahoro Pazi wa timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro pamoja na mshambuliaji mzoefu Mussa Hassan Mgosi wa timu ya Simba ya jijini Dar es salaam