Croatia wamechukizwa na uchezeshaji wa mwamuzi kutoka Japan, Yuichi Nishimura aliyewapa Brazil penati tata.
Kocha na wachezaji wa Croatia wanaona kwamba mchezaji wa Brazil, Fred, alijirusha ili kupata nafasi kwani hakuchezewa vibaya na mlinzi Dejan Lovren kwenye mechi ya ufunguzi.
Lovren anasema hiyo ni kashfa kubwa kwa mwamuzi kwenye mashindano hayo makubwa ambapo penati ilitolewa wakiwa 1-1 na kubadili kabisa mchezo ambao Croatia walikuwa wamewabana vilivyo Brazil.
Lovren anayechezea Southampton ya England anapendekeza mwamuzi huyo aondoshwe kwenye orodha ya kuchezesha michuano hiyo kwani ataharibu zaidi.
Wapo wachambuzi wanaoona pia kwamba Fred mwenye uzito wa kilogramu 85 alianguka kirahisi mno huku ikionekana mgusano bana ya wawili hao ulikuwa mdogo katika dakika hiyo ya 70.
“Hii ni kashfa, sijui mwamuzi huyu anafanya nini hapa. Ile haikuwa penati maana sikumgusa. Sasa unafanyaje unapocheza dhidi ya wachezaji 12?” anahoji Lovren.
Mlinzi mwenzake, Vedran Corluka anasema uamuzi huo unaudhi sana na mbaya zaidi ni katika mechi kubwa ya ufunguzi na kwamba Brazil hawakustahili kushinda.
Kocha wa Croatia, Niko Kovac alilaani kitendo cha mwamuzi huyo na kusema bora timu yake irudi nyumbani ikiwa uchezeshaji ni wa aina hiyo.
“Tunazungumzia heshima lakini Croatia hatukuheshimiwa hata kidogo, ikiwa ile ni penati basi hatuna haja ya kucheza soka tena, bora tucheze mpira wa kikapu, ni aibu kubwa.
“Tukiendelea hivi patakuwa na penati 100 kama ile. Nadhani watu bilioni 2.5 waliokuwa wanatazama waliona kwamba ile haikuwa penati,” akasema kocha huyo.
Hata hivyo, Kocha wa Brazil, Luiz Felipe Scolari anaamini mwamuzi alikuwa sahihi kutoa penati hiyo na kwamba kila mtu aliona uhalali wake na kwamba waamuzi lazima waheshimiwe kwani ndio waliopewa mamlaka ya kuamua.
Mchambuzi Phil Neville aliyekuwa mlinzi wa England miaka iliyopita anasema ilitolewa kirahisi mno pasipo sababu na kwamba mwamuzi akiangalia video ya tukio hilo atajilaumu kwani Fred alianguka kilaini mno.
Anasema penati ilitolewa wakati mgumu kwa Croatia, kwani licha ya Brazil kutawala mchezo, Croatia waliwakaba vyema na kulikuwa na dalili za mechi kumalizika kwa sare nzuri.