Mchezaji wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo ameweka rekodi mpya kwa kuwa mfungaji wa mabao mengi zaidi katika historia ya Michuano ya Ulaya.
Ronaldo aliweka rekodi hiyo kwa bao aliloifungia Ureno dhidi ya Armenia, katika mechi ya kutafuta kufuzu kwa Euro 2016.
Mchezaji huyo wa Real Madrid alifunga bao hilo la 23 katika dakika ya 71 baada ya kuuhangaikia mpira, baada ya Ureno kuwa wamecheza muda wote huo wakihangaika jinsi ya kuzifumania nyavu ili watoke na ushindi.
Kwa bao hilo, sasa Ronaldo amempita raia wa Denmark, Jon Dahl na Mturuki Hakan Sukur waliokuwa na mabao 22 na walikuwa washika rekodi wenza wa Ronaldo ambaye amewapiku na kusonga mbele, akitarajia bado kuongeza mengine kadiri muda unavyokwenda.
Ureno wamepanda hadi nafasi ya pili kwenye Kundi I wakiwa na pointi sita kutokana na mechi tatu. Ukiacha bao hilo, Ronaldo ambaye pia ni mwanasoka bora wa dunia hakucheza vyema, ambapo alikwamisha mipira mitatu ya dhabu ndogo kwenye ukuta wa Armenia.
Ureno walitarajiwa wafanye vizuri dhidi ya timu hiyo dhaifu, lakini Armenia walikaribia kufunga, hasa pale mchezaji wa Borussia Dortmund, Henrikh Mkhitaryan alipompelekesha kipa Rui Patricio kuokoa bao kwa tabu katika dakika ya 14.
Kadhalika kiungo Kamo Hovhannisyan aliweza kuvuka na kumjaribu kipa huyo ndani ya nusu saa ya mwanzo. Beki wa pembeni wa Chelsea, Jose Bosingwa (32) amerudi kwenye timu ya Ureno baada ya kukosekana kwa miaka minne, huku pia Ricardo Carvalho (36) aliyekuwa Chelsea akiitwa na kucheza.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo, Denmark walitoka nyuma na kuwafunga Serbia 3-1. Matokeo ya mechi nyingine ni Ujerumani kuwachakaza Gibraltar 4-0, Georgia kulala kwa Poland 0-4 na Scotland kuwafunga ndugu zao Jamhuri ya Ireland 1-0.
Ugiriki walipata ushindi wmembamba pia wa 1-0 dhidi ya Visiwa vya Faroe, Hungaria wakawapiga Finland kwa idadi hiyo hiyo na Romania wakawapiga Ireland Kaskazini 2-0.