Menu
in , , ,

CR7 awabomoa Atletico

Tanzania Sports

Nyota wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ‘CR7’ amepeleka kilio kwa
mahasimu wao wakuu wa jijini Madrid, Atletico Madrid kwa kufunga
hat-trick iliyotoa matokeo ya 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Hispania
– La Liga.

Hiyo ni hat-trick ya 39 kwa Ronaldo na ushindi huo muhimu
umewaimarisha kileleni mwa ligi, wakiwa na pointi 30 kutokana na mechi
12, wakiwazidi mahasimu wao nchini humo, Barcelona wenye pointi 26 na
ambao walibanwa na Malaga kwa sare kabla ya mechi hiyo ya wababe wa
Madrid.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno alifungua kitabu cha mabao kwa
mpira wa adhabu ndogo uliokengeuka na kumzidi maarifa golikipa Jan
Oblak. Aliongeza bao la pili kwa penati kabla ya kumalizia la tatu
kutokana na majalo nzuri ya Gareth Bale.

Ronaldo (31) amefunga mabao nane kwenye La Liga kwa mabingwa hawa wa
Ulaya hivyo kuwa sawa na Lionel Messi na Luis Suarez wa Barcelona.
Kadhalika amemzidi kwa bao moja shujaa wa Madrid, Alfredo Di Stefano
aliyekuwa na mabao 17 aliyopata kufunga kwenye ‘Madrid Derby’. Ronaldo
angeweza kufunga mabao mengi zaidi kama si kwa Oblak kufanya kazi ya
ziada kuokoa mpira wa kasi wa kichwa wa Ronaldo wakati timu zikiwa
hazijafungana.

Matokeo hayo yanawaweka pabaya Atletico wanaofundishwa na Diego
Simeone, kwani sasa wapo pointi tisa nyuma ya vinara hao. Nafasi ya
tatu kwenye La Liga inashikwa na Sevilla wenye pointi 22 na Atletico
wakiwa wan ne na pointi zao 21.

Ronaldo sasa amefikisha jumla ya mabao 17 kwenye mechi 16 msimu huu na
ni majuzi tu alisaini mkataba mpya wa kubaki Madrid hadi Juni 2021,
huku akisema kwamba anaweza kuendelea kucheza hadi afikishe umri wa
miaka 40.

Ukweli ni kwamba katika mechi hiyo alionesha vitu adimu zaidi kwa
msimu huu na haonekani kwamba anakaribia kuchoka. Kocha Zinedine
Zidane alimpumzisha dakika saba kabla ya kumalizika kwa mechi, naye
alipokea hilo vyema, akionesha ‘kukua’,tofauti na alivyokuwa akifanya
siku zilizopita.

Baadhi ya washabiki wamekuwa wakimwita Zidane ‘kocha mwenye bahati’
lakini ukweli ni kwamba Mfaransa huyu ana mbinu nzuri za ukocha na
jinsi ya kupanga kikosi chake na mfumo wa kutumia, hivyo lazima naye
apate sifa kwa hali ya timu.

Tangu Zidane achukue timu kutoka kwa Raphael Benitez hajapoteza mechi
ya ugenini, ambapo amefunga mabao 44 na kufungwa 12.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version