Menu
in , ,

COURTOIS KUTWAA ‘GOLDEN GLOVE’ NI DHULUMA

Tanzania Sports

Golikipa wa Chelsea Thibaut Courtois ameshinda tuzo ya ‘Golden Glove’ kwenye msimu wa EPL uliomalizika Jumapili ambao timu yake waliibuka mabingwa. Tuzo hiyo ya ‘Golden Glove’ hupewa golikipa aliyecheza michezo mingi zaidi bila kuruhusu bao.
Mbelgiji huyo alicheza jumla ya michezo 16 ambayo hakuruhusu bao lolote huku Mfaransa Hugo Lloris wa Tottenham akiwa na michezo 15 aliyolinda lango lake pasipo nyavu zake kuguswa. Kwa lugha ya Kiingereza Courtois alikuwa na ‘clean sheets’ 16 huku Lloris akiwa nazo 15.

Magolikipa wengine waliomaliza na ‘clean sheets’ 10 au zaidi kwenye msimu huo wa EPL ni David De Gea wa Manchester United aliyekuwa nazo 14, Fraser Foster wa Southampton aliyemaliza na 14, na Petr Cech wa Arsenal mwenye 12.
Wengine ni Joel Robles wa Everton na Tom Heaton wa Burnley ambao kila mmoja wao alimaliza msimu na ‘clean sheets’ 10. Katika orodha hii ni Joel Robles aliyeruhusu mabao machache zaidi (20) kwenye michezo 20 aliyopata nafasi ya kucheza.
Lakini tunaweza kushirikiana kuitambua tuzo hii ya Thibaut Courtois kama dhuluma licha ya umahiri ambao tunafahamu anao. Unapolindwa na walinzi aina ya David Luiz, Gary Cahill, Cesar Azpilicueta na wengine ambao hupunguziwa kazi na shuguli nzito ya N’Golo Kante unakuwa salama mno.

Thibaut Courtois ameokoa mashuti 69 pekee kwenye michezo 36 aliyokaa langoni msimu huu. Ameokoa michomo hiyo kutoka kwenye jumla ya mashuti 99 yaliyolenga lango akiwa golini ambapo 2 kati ya hayo yalizuiliwa na walinzi.
Kuna michezo mitatu ambayo Courtois alikaa langoni bila kukutana na shuti lolote lililolenga lango ndani ya dakika zote 90. Hiyo ni michezo dhidi ya Burnley wa Agosti 2016, dhidi ya Leicester City uliopigwa Oktoba na dhidi ya Everton uliochezeka Novemba 2016.

Ipo michezo mitano mingine ambayo Courtois alipigiwa shuti 1 tu lililolenga lango ndani ya dakika zote 90. Hiyo ni michezo dhidi ya Southampton wa Oktoba 2016, dhidi ya Middlesbrough wa Novemba, dhidi ya Stoke City uliopigwa Machi, dhidi ya Bournemouth uliochezwa Aprili na dhidi ya Middlesbrough wa Mei.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa uwezo na mbinu nzuri za ulinzi za Chelsea zilimbeba mno Courtois. Mchezo ambao alipigiwa mashuti mengi zaidi yaliyolenga lango ulikuwa mchezo dhidi ya Manchester City wa Aprili 2017 aliopigiwa mashuti 7.

Tukimgeukia Tom Heaton tunapata picha tofauti. Nahodha huyo wa Burnley ndiye aliyeokoa mashuti mengi zaidi ya magolikipa wote wa EPL msimu huu. Ameokoa jumla ya mashuti 143 ambayo ni zaidi ya mara mbili ya mashuti 69 yaliyookolewa na Courtois.

Heaton anazo ‘clean sheets’ 10 akiwa amecheza michezo 35. Hakuna mchezo ambao golikipa huyo amecheza pasipo wapinzani kupiga shuti lililolenga lango. Ipo michezo mitatu aliyopigiwa mashuti 10 au zaidi yaliyolenga lango. Burnley hawakumlinda.
Muingereza huyo ameokoa zaidi ya asilimia 75 ya mashuti yaliyolenga lango la Burnley msimu huu wakati Thibaut Courtois ameokoa chini ya asilimia 70 za mashuti yaliyolenga lango la Chelsea akiwa golini msimu huu.

Kwa wastani Tom Heaton ameokoa mashuti 4 kwa kila mchezo aliocheza msimu huu wakati Thibaut Courtois ameokoa mashuti 1.9 kwa kila mchezo wa EPL aliowachezea mabingwa Chelsea msimu huu.

Takwimu hizo zinatufundisha kuwa kigezo cha idadi ya ‘clean sheets’ mara nyingi hakitendi haki kwenye kumtambua golikipa aliyefanya vizuri zaidi kwenye mashindano. Hii si kwa EPL tu, ni kwenye ligi zote. Ni salama kusema kuwa Courtois kutwaa ‘Golden Glove’ ni dhuluma.

Written by Kassim

Exit mobile version