Visa vya mashambulizi ya virusi vya corona vimezidi kuogofya, ambapo baada ya shughuli mbalimbali, zikiwamo huduma za elimu kufungwa, sasa mechi zote za soka nchini Uingereza zimeahirishwa, walau hadi mwisho wa mwezi ujao wa Aprili.
Awali mechi moja ya Arsenal na Manchester City iliahirishwa kwa hofu hiyo, kisha raundi mbili zikafutwa kabla ya kuamuliwa kufuta mechi zote hadi Aprili 4, lakini sasa imeamuliwa hakuna mechi yoyote ya soka hadi mwisho wa Aprili.
Mechi zilizofutwa ni za Ligi Kuu ya England (EPL), Ligi ya Soka England (EFL), Super League ya wanawake na Championship ya Wanawake pia kote England, Uskochi, Wales na Ireland Kaskazini.
Chama cha Soka (FA) cha England pia kimeridhia kwamba msimu unaweza kuahirishwa kwa muda usiojulikana, kutegemeana na hali ya virusi hivyo hatari vilivyosababisha vifo vya watu zaidi ya 70 nchini Uingereza kuzidi kutishia Maisha kwa kuathiri watu na shughuli za kila siku.
Kwa kanuni za sasa, msimu huu wa soka wa 2019/2020 umepangwa kumalizika Juni mosi. Taarifa ya pamoja iliyotolewa na FA Bodi ya EPL na EFL imesema kwamba wanajitolea kutafuta njia mwafaka ya kuanza tena mechi ili kumaliza msimu kwa mechi za nyumbani lakini pia zile za Ulaya mapema kwa kadiri inavyowezekana lakini kwa usalama.
Wiki jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya EPL – West Ham, Karren Brady alipendekeza kwamba msimu huu utangazwe kuwa batili na kisha timu zishiriki mashindano ya kimataifa zilizoshiriki msimu uliopita, akimaanisha Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na Ligi ya Europa.
Mwenyekiti wa FA, Greg Clarke pia alieleza kusikitishwa kwake mambo yanavyokwenda na kwamba ulikuwapo uwezekano kushindwa kumaliza msimu huu wa soka kwa mechi zilizobaki kuchezwa.
Hata hivyo, Mtendaji Mkuu wa Brighton, Paul Barber alisema kwamba haingekuwa haki iwapo mabingwa ‘wateule’ Liverpool’ hawangepewa kombe ‘lao’ na ligi kufutiwa matokeo yote. Kadhalika anapendekeza kwamba timu za msimu ujao wa soka wa 2020/2021 ziongezwe kutoka 20 za sasa hadi 22.
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeunda kundikazi maalumu kwa ajili ya kushughulikia masuala yanayoigusa soka kama matokeo ya kusambaa kwa virusi hatari vya corona. Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo itatazama upya kalenda ya soka ya kimataifa na masuala yanayohusu mikataba ya wanasoka kwenye klabu zao. Kwa kawaida mikataba ya wachezaji kwa msimu husika humalizika Juni 30 ya kila mwaka, lakini kwa hali ilivuo, mechi zilizosalia zikianza kuchezwa huenda zisimalizike kabla au tarehe hiyo na hivyo kuweza kuathiri haki za wachezaji.
Kuahirishwa kwa michuano ya Euro 2020 iliyokuwa ifanyike kiangazi cha mwaka huu kunawezesha ligi za nyumbani kuendelea hadi Juni, japokuwa wachezaji watakuwa na muda mfupi wa kupumzika kabla ya kuanza msimu mpya.
Serikali ya Uingereza imezuia mechi kuendelea, ikiwa ni maelekezo ya kiafya na pia kuzuia mikusanyiko ya watu wengi hadi Aprili 30 watakapotazama tena suala hilo kulingana na matakwa ya wakati huo, kutokana na hali ya Covid-19 itakavyokuwa.
Huku wanaoshikilia haki za kurusha matangazo – Sky na BT wakiwa na haki ya kudai jumla ya pauni milioni 750 kama fidia ikiwa ligi haitaanza tena, Bodi ya Ligi Kuu imedhamiria kufanya kila linalowezekana kuhakikisha inaheshimu mikataba yao ya kibiashara ili kuepuka hasara ya kutoa kitita hicho.
Mmiliki wa Forest Green Rovers, Dale Vince anasema kwamba kusitisha au kuahirisha mechi za wachezaji wa kulipa tangu Machi 13 lilikuwa kosa kwa sababu katika hatua hiyo virusi vya corona havikuwa vimeiathiri nchi.
“Nafikiri kuahirisha mechi zote hadi Aprili 3 (na sasa hadi Aprili 30) lilikuwa kosa. Nadhani ulikuwa uamuzi usio sahihi. Katika hilo kuna kipindi cha wiki nne ambapo tungeweza kumaliza msimu kwa kuchea mechi kuanzia Jumamosi hadi Jumanne,” Dale anasema.
Kibopa huyu anasema kwamba badala ya kufunga na kuzuia mechi wangeongeza siku za mechi kwa wiki na kumaliza haraka kabla virusi havijaanza kushika kasi na kuleta matata kwa watu, wakiwamo wachezaji na makocha. Anasema kwamba kasi ya maambukizi ya virusi hivyo haiwezi kupungua au kuisha hata ndani ya miezi miwili, mitatu wala minne.
Forest Green wanashika nafasi ya 11 kwenye Ligue Two, wakiwa na alama tisa nje klabu zinazoweza kucheza mechi mbili za mtoano kwa ajili ya kupanda kuingia Ligue One ambayo ni saw ana Ligi Daraja la Pili.
Arsenal walio kwenye EPL wanaunga mkono uamuzi wa kuahirisha mechi zote hadi mwisho wa mwezi Aprili, baada ya kocha wao, Mikel Arteta kuambukizwa virusi vya corona. Tangu kubainika kuugua kwa Mhispania huyo, uwanja wa mazoezi wa Colney umefungwa na kila mchezaji anafanya mazoezi kwake kivyake.