Menu
in , , , ,

Columbia wawaadhiri Ugiriki

 

Colombia wameanza vyema fainali za Kombe la Dunia katika Kundi C kwa kuwafunga Ugiriki 3-0.
Pablo Armero aliwainua washabiki wa Colombia dakika tano tu za mwanzo kwa bao zuri, ambapo beki huyo wa Napoli ya Italia aliunganisha wavuni mpira wa Juan Cuadrado.

Mshambuliaji wa Colombia, Teofilo Gutierrez aliyechukua nafasi ya nyota wao majeruhi, Radamel Falcao aligusa mpira wa kona wa James Rodriguez katika dakika ya 58 na kuandika bao la pili.

Bao la tatu lilifungwa na Rodriguez katika dakika ya 90 na kumaliza kazi nzito na muhimu, lakini mabao yangeweza kuwa manne iwapo Theofanis Gekas angelenga vyema mpira wa kichwa aliokuwa amepata katika nafasi nzuri.

Haya ni matokeo mazuri zaidi kwa Colombia kwenye historia ya Kombe la Dunia na kwa hakika walionesha kujiamini tangu mwanzo na wanapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kwenye timu 16 bora.

Walimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Argentina kwenye hatua za kufuzu kwa eneo la Amerika Kusini. Wameweza kuhimili shinikizo kwenye eneo la ushambuliaji baada ya Falcao aliyefunga mabao tisa katika mechi za kufuzu kuzikosa fainali hizi kwa sababu ya kuumia goti.

Hata hivyo, Falcao alikuwapo Brazil na aliwaunga wenzake mkono kisaikolojia kabla hawajatimkia dimbani kwa ajili ya kuanza kipute hicho.
Kadhalika Colombia wanaocheza karibu na nyumbani waliungwa mkono na washabiki wengi waliofika ambao walikuwa wakishangilia sana katika dimba la Estadio Mineirao jijini Belo Horizonte, wachezaji wakiwa chini ya kocha Jose Pekerman.

Ugiriki wameweka rekodi kwa kuruhusu bao katika dakika saba za mwanzo katika kila mechi za fainali kama hizi tatu zilizopita.
Timu hizi zipo kundi moja na Ivory Coast na Japan watakaocheza Jumapili hii.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version