Menu
in , , ,

Clattenburg awavutia pumzi Chelsea

*Alikuwa achezese wiki hii akakataa

*Kibao chaweza kuwageukia Chelsea

Chelsea wanaweza kuwa katika wakati mgumu, ikiwa watashindwa kuthibitisha tuhuma zao nzito dhidi ya mwamuzi Mark Clattenburg.
Mwamuzi huyo hatachezesha mechi wiki ya pili mfululizo, lakini imefahamika kwamba wapangaji walikuwa tayari kumpa kazi, akawa na mawazo tofauti.
Chelsea wanadai alimrushia maneno ya kibaguzi John Obi Mikel, lakini wamefuta madai kama hayo kwamba alimrushia pia Juan Mata.
Wapo wachambuzi wa mambo na wadau wa soka wanaoona umefika wakati kwa mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich kuingilia kati, kwa madai kuwa klabu inaonekana kupoteza mwelekeo katika suala hili, tangu walipopata kipigo kutoka kwa Manchester United Oktoa 28 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka (FA) cha England, David Bernstein amesisitiza kwamba Clattenburg hataachwa mpweke wakati wa tuhuma hizi.
FA na polisi wanachunguza tuhuma za Chelsea, ambapo polisi wameingia baada ya kutumiwa maombi na Chama cha Wanasheria Weusi. Akitiwa hatiani, unaweza kuwa mwisho wa kazi yake.
Clattenburg hatashika kipenga katika raundi ya pili ya mechi za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), lakini Meneja Mkuu wa Chama cha Waamuzi wa Kulipwa (PGMOL), Mike Riley anasema haoni kwa nini asichezeshe.
Kwamba yeye (Riley) angefurahia kuona Clattenburg akichezesha mechi kama kawaida, lakini baada ya wawili hao kukutana na kujadiliana, alikubaliana na mawazo ya Clattenburg kukaa kando kwanza.
“PGMOL ilikuwa imejiandaa kabisa kumfikiria nafasi ya kuchezesha wiki hii, lakini baada ya kujadiliana naye, tumeona ni bora kwake wiki hii akae pembeni katika shughuli za uamuzi anapojiandaa kuisaidia FA na polisi kwenye uchunguzi wao,” anasema Riley wa chombo kinachotoa waamuzi wote wa EPL.
Wiki iliyopita, Chelsea walisema waliwasilisha rasmi madai yao baada ya kufanya uchunguzi wa kina unaodaiwa kutumia wanasheria wa nje na taarifa kutokana na mahojiano na wachezaji wao.
Mmoja wa wachezaji wanaodaiwa kusikia maneno hayo ni Ramires, ambaye hata hivyo ofisa mmoja wa zamani wa Chelsea anasema uelewa wake wa lugha ya Kiingereza ni mdogo sana, hivyo hawezi kutegemewa.
Clattenburg mwenye umri wa miaka 37, ni mmoja wa waamuzi wanaosifika nchini Uingereza na duniani, na yumo kwenye orodha ya awali ya watakaochezesha Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Kocha wa Manchester United, Alex Ferguson anasema hadhani kwamba mwamuzi huyo angeweza kutoa kauli ya kibaguzi kwa mchezaji yeyote.
Arsene Wenger wa Arsenal anasema Chelsea wamepotoka kwa kutoa madai hayo hadharani, kwani wangeweza kwenda nayo taratibu.
Ripoti ya Clattenburg katika mechi ambayo Manchester walishinda mabao 3-2, inadaiwa kuwa na taarifa za tukio lisilo la kawaida, linalotakiwa kutazamwa na FA.
Obi anadaiwa kumvamia Clattenburg kwenye chumba cha waamuzi akiwa na kocha Roberto Di Matteo na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chelsea, Sam Wallace baada ya mechi, wakimshinikiza awaombe radhi.
Obi anadaiwa kumtishia kumpiga buti, lakini Clattenburg alikataa madai hayo, na kushitushwa na taarifa kwamba alitoa lugha ya kibaguzi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version