ILI Manchester United iweze kusonga mbele kwa mafanikio inahitaji kufanyiwa mabadiliko kwenye baadhi ya maeneo. Kikosi chake kimeondokewa na nyota wawili Marcus Rashford alikyekwenda kwa mkopo katika klabu ya Aston Villa, wakati Antony amekwenda Real Betis ya La Liga. Kocha Ruben Amorim amekuwa akipanga na kupangua kikosi chake mara kwa mara. Katika kuhakikisha anaibadilisha hali ya Manchester united kocha huyo amelazimika kuelekeza macho yake katika akademi ya timu hiyo.
Wakati kikosi chao kilipokuwa kinaelekea kupambana na Tottenham Hotspurs kilikuwa na wachezaji saba kutoka akademi. Kuitwa wa wachezaji hao kunatuma ujumbe kuwa kocha huyo ameanza kushika hatamu na anataka kuona matunda mazuri kwa kazi yake. Manchester United kama walivyo wapinzani wao Spurs wanahaha kusahihisha mambo magumu yanayowaelemea msimu huu.
Ruben Amorim amegeukia akademi ya Man United kama sehemu ya kuvuna vipaji vya kuita kikosi cha kwanza. Hadi sasa anaonekana kutoridhishwa na baadhi ya wachezaji klabuni hapo, pamoja na kukabiliwa na majeruhi wengi tangu alipochukua jukumu la kuinoa timu hiyo.
Mzigo wa majeruhi
Kocha huyo anakabiliwa na mzigo mzito wa wachezaji majeruhi kwenye kikosi chake cha kwanza. Wachezaji ambao hawatakuwa uwanjani kwa siku hivi karibuni pamoja na beki wa kati Lisandro Lopez, Luke Shaw (beki wa kushoto) Mason Mount (Kiungo mshambuliaji), Jonnh Evans (beki wa kati), Kobbie Mainoo (Kiungo mshambuliaji), Manuel Ugarte (kiungo wa kati), Toby Collyer (beki) na Amad Diallo (winga). Wachezaji hao wamekuwa nguzo katika vita ya kuepuka kushuka daraja msimu huu ambayo Man United wanakabiliana nayo. Hadi sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Rada yake akademi
Baada ya kuona majeruhi wamekuwa wengi, kocha Rube Amorim ameelekeza rada yake kwenye kikosi cha vijana cha klabu hiyo. Kuelekea mchezo wa Tottenham Hotspurs kocha huyo aliwaita wachezjai chipukizi saba ili kuungana na timu hiyo kwenye mpambana wa kukata na shoka ulioshuhudiwa na amelefu ya mashabiki wikiendi hii. Miongoni mwa chipukizi walioitwa ni pamoja na Sekou Kone (kiungo) na Jack Moorhouse (kiungo) ambao wana umri wa miaka 19. Golikipa Elyh Harrison (miaka 18), beki w akushoto Harry Amass (miaka 17) na mshambuliaji Chido Obi (miaka 17). Wengine ni kiungo Jack Fletcher (miaka 17) na beki Tyler Fredricson mwenye umri wa miaka 19 nao waliungana na chipukizi wenzao kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Inaaminika kuwa wachezaji hao wapo katika rada ya kocha huyo na huenda wakapata nafasi zaidi kuelekea mwisho wa msimu huu. Katika mechi kadhaa wanaweza kupangwa au kupewa dakika ili kuimarisha uwezo wao.
Jibu la mfumo wa Amorim
Mfumo anaotumia kocha Ruben Amorim unamlazimisha kuwa na wachezaji wenye kasi na uwzo mzuri wa kukokota mpira pamoja na ubunifu. Mbinu zao zinahitaji kuanzia mabeki wabunifu, viungo wakabaji wabunifu, viungo washambuliaji wenye ubunifu. Ni sawa na kuwa na kikosi cha wachezaji ambao wanaweza kumpa kitu cha ziada. Aina ya wachezaji hao ni wachache katika kikosi chake cha sasa. Amad Diallo ndiye mchezaji ambaye anaonekana kuingia kwenye mfumo wa Amorim kirahisi zaidi na ndiye silaha yake ya kwanza. Ili kumudu mfumo wa kocha huyo ni lazima awe na wachezaji wenye kasi na vijana ambao wanaweza kuungana na wale wazoefu kuleta manufaa zaidi. Katika kikosi chake anahitaji mabeki wa pembeni wa kuingia kwenye mfumo. Anahitaji beki wa kati wawili, viungo washambuliaji na washambuliaji wa daraja la juu ili kuimarisha kikosi hicho.
Kwa umri wa wachezaji hao, kwenye baadhi ya timu wapo waliopewa nafasi. Mfano katika klabu ya Real Madrid wachezaji wenye umri wa miaka 18, 19, 20, wanakuwa kwenye kikosi cha kwanza lakini Man United hali imekuwa tofauti. Hata Liverpool inao mabeki chipukizi wenye umri chini ya miaka 20 na wanacheza kikosi cha kwanza. Ruben Amorim amebaini matumizi mabaya ya vipaji vya Man United, kwani wengi wanasota bila kupewa nafasi. Ili kuunda timu mpya lazima wachezaji wenye ari mpya, kasi mpya na matumaini mapya ndiyo wataoweza kuipandisha ngazi timu hiyo. Lakini wakiigeuza kuwa sehemu ya wachezaji wa kula pensheni kama akina Carlos Casemiro au John Evans watakuwa wanatwanga maji kwenye kinu.