Menu
in , ,

CHINA INAVYOPOTEZA NDOTO NA MAJINA

Tanzania Sports

Aliwahi kusema mwanahabari maarufu wa marekani Mignon McLaughlin kuwa sote tunazaliwa mashujaa, waaminifu na walafi lakini wengi wetu huwa tunabaki kuwa walafi. Ukisikia mchezaji yoyote ameenda kucheza China ujue huyo amefuata hicho cha mwisho akikwambia sijui timu alikuwa anaipenda na anaijua huyo ni mnafiki tu kwani wachezaji wangapi hata pale Ulaya huwa wanasema maneno hayo kila wakihamia timu mpya? Ndio maisha yalivyo bila unafiki hayaendi.

Kivutio cha kwanza China ni pesa yao. Ubora wa ligi yao ni mdogo, hata wachina wenyewe hawajazi viwanja hivyo wakati wa mechi na hio ikutoshe kuwa hawavutiki na ligi yao. Pesa za wachina zinawapoteza na zinaelekea kupoteza ndoto za watu pia. Leo hii hakuna anaetaka kujua kuhusu Oscar wala Hulk. Au hata mchango wao kwenye timu zao. Ikusaidie nini? Ligi ya China inataka ikue kwa kuleta majina makubwa ya soka kutoka Ulaya lakini yenyewe ndio inayapoteza majina hayo kwa sababu ligi yao haina mvuto na mwisho nyota hao pia wanakosa mvuto. Juzi hapa Oscar kaifungia magoli mawili matamu sana klabu yake ya Shanghai SIPG lakini ni wabongo wachache wanalijua hilo. Wachezaji kama huyu na wengine wenye majina makubwa kama huyu na umri mdogo wanapotezwa mapema.

Juzi hapa FC Barcelona ilimuaga Javier Mascherano baada ya miaka 7 ndani ya Nou Camp na alipokwenda China akaanza kujipa moyo kuwa ataitwa timu ya taifa ya Argentina na mwalimu Jorge Sampaoli. Akaulizwa unahisi atakuwa anakufuatilia ukicheza huku na alichojibu ni kwamba alimpigia simu na kocha akamwambia endapo atakuwa fiti kabisa na ataepukana na majeruhi basi nafasi ya kuitwa anayo.

Nilichogundua hapa ni kwamba hata walimu wa timu za taifa inaonesha hawana muda mkubwa wa kuwafuatilia nyota kutoka huko. Tayari mtu anaweza kushindwa kutimiza ndoto ya kwenda Urusi kwa sababu yuko huko China. Yani hivo tu. Unaweza ukawa mzima na ukawa fiti lakini kutokana na ubora mdogo wa ligi hiyo ukakuta mwalimu anakukataa.

Nilisikitika hapa juzi kati kumwona mtu kama Yannick Carrasco akienda China. Bado ni kijana mdogo ambae mwili wake unaruhusu sana lakini amekwenda kupotea China. China au Marekani panawafaa wale wachezaji wakongwe ambao uwezo wao kimpira unaisha na wanachokwenda kukifanya kule ni kuuza jina na kupiga pesa. Lakini na hivyo basi wengi huwa wanaona bora waende hata Marekani yani ilimradi tu sio kule mashariki ya mbali.

Kama ni mchumia tumbo basi China ndio mahala sahihi kwako lakini kama uko kwa kukuza jina na kutengeneza heshima basi mpira una nchi zake.

Written by haatimabdul

Exit mobile version