Menu
in , ,

Chile fainali Copa America

Wenyeji wa michuano ya Copa America, Chile, wamefika fainali baada ya kuwachapa Peru 2-1 katika mechi kali ya nusu fainali.

Hii ni mara ya kwanza kwa Chile kufika hatua hiyo katika kipindi cha miaka 28, hivyo jiji la Santiago likalipuka kwa shangwe kwa ushindi huo muhimu, ambapo Peru walimaliza mechi wakiwa na wachezaji 10.

Nusura Chile nao wapoteze mchezaji mmoja, kwani Arturo Vidal ambaye amekuwa muhimu kwenye michuano hii alionekana kurusha mkono usoni mwa Carlos Zambrano muda mfupi kabla ya mchezaji huyo wa Peru kugonga mwamba wa goli baada ya kutiliwa mpira wa kichwa na Jefferson Farfan.

Alikuwa ni Zambrano, mlinzi wa Peru, aliyekuja kuonja joto ya jiwe kwa kulambwa kadi nyekundu kutokana na kumkamata mchezaji wa Chile, Charles Aranguiz aliyekuwa anaelekea langoni kufunga.

Mabao ya Chile yalitiwa kimiani na mshambuliaji wa zamani wa Queen Park Rangers (QPR), Eduardo Vargas baada ya mshambuliaji wa Arsenal, Alexis Sanchez kugonga mwamba kwa shuti lake kali.

Vargas alifunga bao la kwanza dakika ya 42 lakini dakika 18 baadaye Peru walisaidiwa kusawazisha kwa bao la Chile kujifunga wenyewe kupitia kwa Gary Medel na kusababisha sononeko jukwaani.

Medel alijinyoosha sana kwa ajili ya kuunasa mpira uliokuwa umepelekwa kwake na beki wa kulia, Luis Advincula ili aondoe eneo la hatari, lakini alichofanya ni kuusindikiza kwenye nyavu a timu yake, huku kipa Claudio Bravo akishindwa kuuzuia kutokana na kushitukizwa
Vargas aliwapa washabiki kile walichotaka na timu kustahili baada ya kucheka na nyavu akiwa umbali wa yadi 25 katika dakika ya 64 na kumaliza ubishi.

Chile hawajapata kutwaa kombe hili kwa miaka 99 licha ya kufika fainali miaka 28 iliyopita, na sasa watajaribu bahati yao watakapocheza na ama Argentina au Paraguay Jumamosi hii.

Peru walionekana kulalamika kana kwamba wameonewa, kutokana na Vidal kutooneshwa kadi na pia bao la kwanza la Chile kukubaliwa ambapo baada ya Sanchez kugonga mwamba na Vargas kuuendea mpira na kufunga, ilionekana kama alikuwa ameotea.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version