Chelsea wamedhihirisha umwamba dhidi ya Manchester City, baada ya kufanikiwa kupata ushindi dakika ya mwisho ya mchezo.
Fernando Torres aliyeaminiwa na kocha Jose Mourinho kwa muda wote wa mchezo, alilipa baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 90.
Chelsea walianza kupachika bao hilo kutokana na kujichanganya kwa Manchester City kama ilivyokuwa kwa bao la kwanza lililofungwa na Schürrle dakika ya 33.
Man City walianza vizuri zaidi mpira, lakini ghafla Chelsea walionekana kuusoma vyema na kujibadili na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao moja, lakini Sergio Aguero alisawazisha dakika ya 49.
Man City watajichukulia kuwa bahati haikuwa yao Jumapili hii, lakini kujichanganya kwa safu yao ya ulinzi ndiko kuliwazawadia wapinzani wao.
Ilishachukuliwa kwamba mechi ingeisha kwa sare, lakini mawasiliano mabaya kati ya kipa wa kimataifa wa England, Joe Hart na mlinzi wa kati, Matija Nastasic kulimwezesha mviziaji Torres kupachika bao la ushindi.
Kocha mpya wa Sunderland, Gus Poyet alikuwa na furaha kubwa baada ya kupata ushindi wa kwanza tangu alipoanza kazi hapo.
Katika mechi ya mahasimu Sunderland na Newcastle United, walikuwa tena Newcastle waliolia katika mechi ya pili mfululizo, kwani msimu uliopita, Paolo Di Canio aliwaongoza Sunderland kuwaua Newcastle nyumbani kwao.
Walikuwa Sunderland waliotangulia kupata bao mapema dakika ya tano kupitia kwa Steven Fletcher lakini lilisawazisha kwa Mathieu Debuchy katika dakika ya 57 na kurejesha matumaini kwa kocha wa Newcaste, Alan Pardew.
Hata hivyo, kiungo aliye Newcastle kwa mkopo kutoka Liverpool, Fabio Borini alibadilisha hali ya mchezo dakika ya 84 kwa kupachika bao la ushindi lililowalipua maelfu ya washabiki wa Sunderland.
Huu ulikuwa ushindi wa kwanza msimu huu, kwani katika mechi zake tisa, wameshinda hii moja, kutoka sare tatu na kufungwa tano.
Tottenham Hotspur walipata kigugumizi lakini hatimaye wakaibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Hull, lililopatikana kwa njia ya penati kupitia kwa mshambuliaji wake mpya, Roberto Soldado katika dakika ya 80.
Kati ya ushindi wa mara sita wa Spurs kwenye Ligi Kuu ya England, mara nne wamepata bao moja tu.
Penati hiyo ilitolewa baada ya Ahmed Elmohamady kushika mpira uliokuwa umepigwa na mshambuliaji huyo huyo.
Kocha wa Spurs, Andre Villas-Boas alionekana kukosa raha katika mazingira ya mechi hiyo, kwa jinsi Hull walivyocheza vyema, hasa ukuta wake uliokuwa ukiundwa na watu watano.
Katika mechi nyingine, Swansea waliowakaribisha West Ham walishindwa kufungana na kumaliza dakika 90 kwa suluhu.
Maana ya matokeo ya mechi za Jumamosi na Jumapili hii ni kwamba Arsenal wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 22, wakifuatiwa na Chelsea na Liverpool wenye pointi 20 kila mmoja.
Spurs wamekwea hadi nafasi ya nne kwa pointi zao 19 wakati Southampton wenye pointi 18 sawa na Everton wanashika nafasi ya tano.
Manchester City wameshushwa hadi nafasi ya saba na jirani zao Manchester United wamebaki nafasi ya nane huku Swansea wakipanda hadi ya tisa na Hull wakishika ya 10.
Nusu ya chini ya msimamo wa ligi inaongozwa na Newcastle wenye pointi 11 wakifuatiwa na West Bromwich Albion, Aston Villa na Fulham wenye pointi 10 kila mmoja.
Nafasi ya 15 inakamatwa na West Ham wenye pointi tisa sawa na Cardiff wakati ya 17 wapo Stoke waliogangamala Jumamosi dhidi ya Man United lakini hatimaye wakakubali kufungwa 3-2.
Nafasi tatu za mwisho zinashikwa na Norwich wenye pointi nane, Sunderland na pointi zao nne wakati Crystal Palace sasa wamekabidhiwa nafasi ya mwisho kwenye msimamo wakiwa na pointi zao tatu na wameshaachana na kocha wao, Ian Holloway.