Chelsea wameshinda mechi yao ya kwanza ya ligi, huku wachezaji wake wapya, Diego Costa na Cesc Fabregas waking’ara.
Matajiri hao wa London walianza kupokea kichapo cha bao moja kutoka kwa timu iliyopanda daraja msimu huu, Burnley katika dakika ya 14 kupitia kwa Scott Arfield kwenye dimba la Turf Moor, lakini Chelsea wakasawazisha na kupiga mengine mawili kabla ya nusu ya kwanza kumalizika.
Alikuwa ni Diego Costa kutoka Atletico Madrid aliyesawazisha dakika ya 17, kabla ya Andre Schurrle kupiga la pili dakika nne baadaye, kisha beki Branislav Ivanovic kukomelea msumari kwenye jeneza la Burnley dakika ya 34 na kufungwa kwa kitabu cha mabao.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, alidai kwamba Barcelona hawakumtumia vya kutosha Fabregas aliyepata kuwa nahodha wa Arsenal, na kudai kwamba yeye atachota kila kinachowezekana kwake msimu huu, ambapo alitengeneza mabao mawili kati ya hayo matatu.
Hata hivyo, Costa alipewa kadi ya njano kwa kujirusha ili kupata lifti ya mpira wa adhabu dhidi ya adui zao, lakini mwamuzi Michael Oliver akaamua vinginevyo. Didier Drogba aliingia baadaye kipindi cha pili na nusura afunge bao.
Mourinho alimwanzisha kipa aliyekuwa Atletico kwa mkopo kwa misimu mitatu, Thibaut Courtois badala ya Petr Cech aliyekuwa chaguo la kwanza kwa miaka 10, na jana alikuwa benchi muda wote. Kuna timu zinataka kumnunua kipa huyo mkongwe.