*Manchester United wapunguzwa kasi
Wakati Arsenal dhaifu imepopolewa mabao 2-1 na Chelsea, Manchester United wamepunguzwa kasi na Tottenham Hotspurs.
Mashetani Wekundu walijeruhiwa kwa sare, kwani pengo kati yao na mahasimu wao, Manchester City sasa ni pointi tano.
Wakicheza nyumbani Stamford Bridge ambako wameshinda mara tatu tu msimu huu, Chelsea walitawala kipindi cha kwanza dhidi ya Arsenal na kupata mabao mawili ndani ya dakika 16 tu.
Vijana wa Rafa Benitez walimwepusha na zomea zomea nyingine, safari hii pakitokezea bango la kumsifu na kusema anawajali.
Walipata mabao yao kupitia Juan Mata, aliyefunga bao lililopatikana baada ya kiungo wa Arsenal Francis Coquelin kuumizwa na Ramires na kuachwa akigaagaa chini, na mwamuzi kusimamisha mchezo baada ya bao kukubaliwa.
Bao la pili lilifungwa na Frank Lampard kwa penati, baada ya mabeki wa Arsenal kuwa legelege na kutofanya ukabaji wa maana, hadi golikipa Wojciech Szczęsny kulazimika kumwagusha Ramires.
Nusura Arsene Wenger aondoke ugenini akicheka, baada ya Arsenal kurejea kipindi cha pili kwa ari na kasi, ambapo Theo Walcott aliyesaini mkataba mpya majuzi alifunga bao safi dakika ya 58.
Chelsea walijitahidi kuzuia shinikizo kali la Arsenal lililodumu kwa muda mwingi wa dakika za mwisho, na kubadili kabisa hali ya mchezo.
Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramoaavic alikuwa jukwaani kushuhudia mechi hiyo muhimu, ambapo Arsenal walikuwa wakitafuta ushindi kwa udi na uvumba.
Benitez alimwanzisha Mhispania mwenzake, Fernando Torres kama kawaida, lakini hakuwa na manufaa sana, akatolewa dakika ya 80 na Demba Ba kuingia, lakini hali ya mchezo haikubadilika sana.
Kwa ushindi huo, Chelsea wanabaki nafasi ya tatu, lakini wakiwa pointi sita nyuma ya Manchester City walio nafasi ya pili.
Arsenal wanabaki nafasi ya sita, wakifungana na Liverpool na West Bromwich Albion kwa pointi 34, wakiwa nyuma ya Everton na Tottenham Hotspurs wanaopigania nafasi muhimu ya nne.
Spurs kwa upande wao, walifanikiwa kuwapunguza kasi Manchester United, pale Mmarekani Clint Dempsey aliposawazisha bao katika dakika za majeruhi, na kufanya timu hizo zitoke sare ya 1-1.
Huku theluji ikimwagika kwa wingi dakika za mwisho za mchezo huo, United walishajihesabia ushindi wa ugenini White Hart Lane, ambao hawajaupata kwa muda mrefu.
Alikuwa ni Robin van Persie aliyewatanguliza Man U kwa bao moja mbele dakika ya 25, alipoweka kimiani kwa kichwa majalo ya Tom Cleverley kutoka wingi ya kulia na kumwacha kipa Mfaransa Hugo Lloris akiugulia.
Mechi ya Jumapili hii nusura isichezwe kutokana na wingi wa theluji, lakini ukaguzi uliofanywa wakiwapo makocha wa timu zote, Alex Ferguson na Andre Villas-Boas, uliruhusu mtanange kufanyika.
Washabiki wengi wa Spurs walishakata tamaa, lakini wachezaji walijituma, wakikosa mabao mengi kutokana na kazi nzuri ya golikopa Mhispania, David De Gea na mabeki wake, akiwamo Rio Ferdinand.
Hata hivyo shinikizo lilipozidi, United walisamu amri, na lilikuwa dakika ya tatu ya nyongeza na ya mwisho, Aaron Lennon alipompa pasi Dempsey ndani ya eneo la hatari, naye kutikisa nyavu kulia kwa De Gea.