Menu
in , , ,

Chelsea waua Mashetani Wekundu

*QPR wajiharibia mbele ya Fulham

Mabingwa watetezi wa Kombe la FA, Chelsea wamekata ngebe za Manchester United waliokuwa na ndoto za makombe mawili mwaka huu.
Bao la dakika ya 49 la Demba Ba lilitosha kumnyamazisha kocha Alex Ferguson, ambaye baada ya mechi alimpa mkono hasimu wake wa Chelsea, Rafa Benitez.
United wanaoukaribia ubingwa wa England, walikuwa wakijigamba kutwaa walau makombe mawili, lakini Chelsea wanatetea kombe walilotwaa baada ya kuwafunga Liverpool 2-1 Mei 5 mwaka jana.
Mechi ya Jumatatu hii katika dimba la Stamford Bridge ilikuwa ya marudio, baada ya kutoshana nguvu kwenye kipute cha awali Old Trafford.
Kwa ushindi huo, Chelsea watakabiliana na Manchester City kwenye nusu fainali uwanjani Wembley Aprili 14 mwaka huu. Wigan itacheza nusu fainali nyingine dhidi ya Millwall siku moja kabla uwanjani hapo hapo.
Ba alifunga bao kwa kuunganisha wavuni moja kwa moja majalo ya Juan Mata kabla Rio Ferdinand kupata mbinu za kumkaba, na kipa David Da Gea kushitukia nyavu zikitikisika.
Ferguson amewalaumu wachezaji wake, na kusema katika dakika zote 90, ni Anton Valencia pekee aliyefikia kiwango walichotarajiwa.
Alimpaka sifa kidogo kipa wake Da Gea, akamlaumu Robin van Persie kwa kukosa zaidi ya nafasi mbili, akisema moja ya kichwa alitakiwa kufunga dhahiri.
Kocha huyo alikiri kwamba kipa wa Chelsea, Petr Cech alikuwa kizingiti kwa kuzuia mpira uliokuwa ukiingia wavuni uliopigwa na Javier Hernandez ‘Chicharito’, na kusema hakuamini kilichotokea.
“Robin alipata nafasi ya kichwa, kwa hakika zilikuwa nafasi kadhaa, moja alitakiwa kufunga kabisa lakini alipaisha.
“Inaudhi kwa sababu sisi ni wazuri kuliko tulivyoonesha. Hatukucheza vizuri kama tulivyotakiwa kipindi cha pili,” alisema Ferguson.

QPR Wajivurugia Mechi

20130401-230703.jpg

Katika mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL), Queen Park Rangers (QPR) wameonesha udhaifu mkubwa, baada ya kukubali mabao ya kuzuilika na kubaki na pointi 23 mkiani mwa ligi.
Wakati washambuliaji walijaribu kujikokota kuweka msingi wa timu kuondoka nafasi ya 19 wanayoshikilia, mabeki, Christopher Samba na nahodha Clint Gill waliwaangusha.
Bao la kwanza lilitokana na Samba aliyesajiliwa kutoka Anzhi Makhachkala kwa pauni milioni 12.5 kushindwa kujipanga vyema, kucheza rafu na kusababisha penati iliyozaa bao lililofungwa na Dimitar Berbatov.
Bao la pili nalo lilitokana na uzito wa Samba katika kufanya uamuzi na kuchukua hatua, kwani alirudishiwa mpira akiwa eneo la hatari na kujaribu kuremba, akajikuta akinyang’anywa na Berbatov kuutia kimiani.
Bao la tatu lilikuwa la kujifunga, na ni baada ya Samba kuzidiwa maarifa kwenye kona ya goli, kisha mpira kufyatuliwa na kumparaza nahodha Hill kabla ya kunasa nyavuni, golikipa wa kimataifa wa Brazil, Julio Cezar akiwa hana la kufanya.
Adel Taarabt aliyerejea alifunga bao kwa juhudi binafsi kabla ya mapumziko, lakini baada tu ya kuanza kipindi cha pili, Loic Remy alishindwa kufunga penati baada ya Adel Taarabt kuchezewa vibaya eneo la hatari.
Hata hivyo, Remy alirekebisha makosa yake dakika ya 51 kwa kufunga bao zuri.
Fulham walicheza 10 dakika zaidi ya 15 za mwisho, baada ya Steve Sidwell kutolewa nje kwa mchezo mbaya. QPR walishindwa kutumia fursa hiyo, licha ya jitihada nyingi, huku Samba akisogea mbele kusaidia mashambulizi muda mwingi.
QPR sasa wana hali mbaya, wakihitaji pointi saba kufika usawa wa kuweza kuokoka kushuka daraja, na hiyo itategemea ikiwa timu zenye pointi 30, Aston Villa na Wigan hazitaongeza pointi zao katika mechi mizunguko saba iliyobaki kwa ligi hii. Wanakabiliana na Wigan mechi ijayo.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version